Maadhimisho ya Siku ya Tisa ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu tarehe 8 Februari 2023 Maadhimisho ya Siku ya Tisa ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu tarehe 8 Februari 2023  

Mt. Bakhita: Siku ya 9 ya Sala na Tafakari dhidi ya Biashara ya Binadamu

Kumbukumbu ya Mtakatifu Josefina "Fortunata" Bakhita yanakwenda sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Tisa ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu tarehe 8 Februari 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Kutembea katika utu.” Siku hii ilianzishwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015 dhidi ya ubidhaishaji wa viungo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko akitoa neno la mwisho kuhitimisha hija yake ya 40 ya Kitume nchini DRC na Sudan ya Kusini kuanzia tarehe 31 Januari hadi tarehe 5 Februari 2023 amewashukuru watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini kwa sadaka na majitoleo yao ili kuhakikisha kwamba, anafanikisha hija ya 40 ya Kitume Barani Afrika na kwa namna ya pekee kabisa Sudan ya Kusini. Amewashukuru wale wote waliotoka ndani na nje ya Sudan ya Kusini ili kushiriki katika hija uekumene wa amani na matumaini, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Josefina Bakhita, “Mwanamke wa shoka” aliyebahatika kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu kugeuza mateso na mahangaiko yake yote kuwa ni chemchemi ya Injili ya matumaini iliyogeuka hatimaye na kuwa ni mbegu ya matumaini. Mtakatifu Josefina Bakhita “Fortunata” maana yake “Bahati” alizaliwa kunako mwaka 1868 huko mjini Darfur, Sudan Kongwe. Akatekwa nyara na “watu wasiojulikana” akauzwa utumwani, na hatimaye, akanunuliwa na Balozi wa Italia mjini Khartoum aliyempeleka mjini Venezia. Akafundishwa katekesi na hatimaye, kubatizwa. Baadaye alijiunga na Shirika la Mabinti wa Upendo wa Mtakatifu Madgalena wa Canossa akijitoa sadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma. Alifariki dunia tarehe 8 Februari 1947 huko Schio, Italia. Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza Josefina Bakhita kuwa Mwenyeheri tarehe 17 Mei 1992, na hatimaye, akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe Mosi Oktoba, mwaka 2000 katika maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo.

Biashara ya binadamu inadhalilisha utu wa binadamu
Biashara ya binadamu inadhalilisha utu wa binadamu

Katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, kunako mwaka 2015, Kanisa likaanzisha Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari ili kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo inayoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni muda muafaka kwa ajili ya kusali na kuwaombea waathirika wa ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu. Maadhimisho ya Siku ya Tisa ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu tarehe 8 Februari 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Kutembea katika utu.” Huu ni mwaliko hasa kwa vijana kusaidia kuragibisha maadhimisho haya dhidi ya ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu na kama sehemu ya maandalizi ya Kumbukizi ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Siku hii hapo tarehe 8 Febuari 2024 kwa utashi na busara za kichungaji za Baba Mtakatifu Francisko. Ni katika muktadha huu, kwa muda wa juma zima kumekuwepo na maadhimisho haya katika ngazi mbalimbali ndani na nje ya Italia na kilele chake ni Dominika tarehe 12 Februari 2023 kwa kushiriki kusali na Baba Mtakatifu Francisko Sala ya Malaika wa Bwana kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Tarehe 8 Februari: Siku dhidi Biashara ya Binadamu
Tarehe 8 Februari: Siku dhidi Biashara ya Binadamu

Kauli mbiu ya mwaka 2023 “Kutembea katika utu” mwaliko wa kutembea bega kwa bega na waathirika wa ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu sehemu mbalimbali za dunia na hasa wahamiaji na wakimbizi kama mahujaji wa utu na matumaini ya binadamu. Ni kwa njia ya umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, biashara haramu ya binadamu inaweza kukomeshwa, ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni muda muafaka wa kuwaunga mkono wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwaokoa, kuwalinda na kuwahudumia waathirika wa biashara hii, ili kuwapatia tena matumaini katika mahangaiko yao ya ndani, daima wakijiaminisha katika ulinzi na nguvu ya Mwenyezi Mungu inayoponya na kuokoa. Uchumi unapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sheria, kanuni na taratibu za uchumi fungamani zihakikishe kwamba, haki na usawa vinatendeka sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kanisa linapenda kuweka utu, heshima na haki msingi za wanawake kuwa ni kiini cha tafakari hii, kwani wanawake, wasichana na watoto ndio waathirika wakubwa wa ubidhaishaji maumbile ya binadamu “human trafficking.”

Mtandao wa mapambano dhidi ya ubidhaishaji wa viungo vya binadamu
Mtandao wa mapambano dhidi ya ubidhaishaji wa viungo vya binadamu

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo ni “donda ndugu” linalosababishwa na utafutaji wa aibu wa maslahi ya kiuchumi bila kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kuna umati mkubwa wa wanawake na wasichana wanaoendelea kutumbukizwa kwenye biashara ya ngono na ukahaba barabani; wanaoshinikizwa kujiuza barabarani na fedha inayopatikana, inachukuliwa na wafanyabiashara ya binadamu. Wasipoleta kile kiwango kinachotakia, cha moto wanakiona! Baba Mtakatifu anasema, haya ni matukio yanayotendeka kwenye barabara za majiji na miji mingi duniani, jambo ambalo watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kulitafakari kwa makini na hatimaye, kuchukua hatua stahiki. Hii ni kashfa dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuonesha uchungu na masikitiko yake makubwa na hivyo kuwataka viongozi wanaohusika kutenda kwa haraka, ili kuzuia na hatimaye, kukomesha biashara haramu ya binadamu pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo, unaodhalilisha na kuwatweza kwa namna mbaya zaidi wanawake na wasichana. Wanawake ambao ni waathirika wakuu wa biashara haramu ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo wanao mchango mkubwa katika mchakato wa kuleta mabadiliko katika sekta ya uchumi, ikiwa kama watajengewa utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Utu, heshima na haki msingi za wanawake na wasichana zilindwe
Utu, heshima na haki msingi za wanawake na wasichana zilindwe

Wanawake wenye umri kati ya miaka 24-54 wanachangia asilimia 90% ya nguvu kazi katika uzalishaji. Lakini takwimu zinazonesha pia kwamba, kuna wasichana asilimia 30% hawajui kusoma wala kuandika; na wengi wao hawana fursa za ajira. Itakumbukwa kwamba, “Talita Kum” ambao ni Mtandao wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa unatekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi 77 sehemu mbalimbali za dunia, tarehe 8 Februari 2023 umeandaa Siku ya Sala na Tafakari kuhusu athari za biashara haramu ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Mtandao wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa, ukipewa ushirikiano wa dhati na vyombo vya ulinzi na usalama kitaifa na kimataifa, uhalifu dhidi ya ubinadamu unaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Kumbe kuna haja kuwatambua waathirika, kuwasaidia pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatendewa haki, ili wahusika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na sheria iweze kuchukua mkondo wake. Hapa kuna haja ya kujikita katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato kwa kutoa elimu makini; kwa kuendesha kampeni za uragibishaji sanjari na kuwalinda watu ambao wanaweza kutumbukizwa katika mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. #PrayAgainstTrafficking."

Bakhita 2023

 

07 February 2023, 15:48