Papa Francisko Asikitishwa na Athari za Majanga Asili na Vita Duniani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wataalamu wa jiolojia wanasema, majanga ya asili ni matukio ambayo hutokea bila kuingilia kati kwa binadamu ambayo huleta maafa makubwa kwa maisha ya binadamu ambayo husababishwa na hali mbaya ya hewa, michakato ya geomofolojia, sababu za kibaolojia au hali ya anga. Mara nyingi, wanadamu wanawajibika kwa athari za maovu ya kiufundi, uzembe, au matokeo ya mipango mibaya. Jeshi la Polisi nchini New Zealand linasema hadi kufikia Dominika tarehe 19 Februari 2023 watu zaidi 6, 431 hawajulikani mahali waliko kutokana na kuathiriwa na Kimbunga Gabrielle. Kimbungu hiki kimesababisha mafuriko makubwa, upepo mkali uliokuwa ukivuma na kwenda kwa kasi kubwa na hivyo kusababisha kuibuka kwa mawimbi mazito Baharini. Ni katika muktadha wa janga hili asili, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 19 Februari 2023 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, amewakumbuka na kuwaombea waathirika wote wa Kimbunga Gabrielle. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuonesha huruma na upendo kwa kuwasaidia wale wote wanaoteseka kutokana na majanga asili, si kwa maneno, bali upendo huu, umwilishwe katika matendo!
Baba Mtakatifu amesema kwamba, upendo wa Kristo Yesu, unawawajibisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwasaidia wale wote wanaoteseka huku Bondeni kwenye machozi kutokana na vita, magonjwa, majanga asili, kutoweka kwa uhuru au kutokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wao na hasa nchini Siria na Uturuki, ambazo hivi karibuni zilikumbwa na tetemeko la ardhi ambalo limesababisha watu zaidi ya 45, 000 kupoteza maisha na wengine wengi bado hawajulikani mahali waliko. Sehemu kubwa ya majengo yameharibika na hayafai tena kwa matumizi ya binadamu. Umoja wa Mataifa umebainisha kwamba, kunahitajika zaidi ya dola za Kimarekani bilioni moja kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi huko Uturuki na kiasi cha Dola milioni 400 zinahitajika kwa ajili ya kuwasaidia waathirika nchini Siria. Baba Mtakatifu pia amewakumbuka na kuwaombea wananchi wa Ukraine wanaoendelea kuteseka kwa sababu za kivita, kinzani, madhulumu na nyanyaso mbalimbali. Wizara ya Ulinzi nchini Uingereza inasema kwamba, zaidi ya watu 60, 000 wamekwisha kufariki dunia, baada ya Urusi kuivamia Ukraine, mwaka mmoja uliopita. Lakini madhara yake ni makubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia.