Papa katika sala ya Kiekumene Sudan Kusini:Msiwe na hofu mtaona wokovu wa Bwana
Na Angella Rwezaula; – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko ametoa hotuba yake katika sala ya kiekumene katika Jumba la Makumbusho la John Garang, Jumamosi jioni tarehe 4 Februari 2023, akiwa katika ziara yake nchini Sudan Kusini kwa siku ya pili. Uwanja huo ulikuwa umejaa watu wengi sana, na alikuwa amemaliza hata hivyo kufanya mkutano na wahamiaji wa ndani ya nchi hiyo, wanaokadiliwa kuwa milioni 4 na ambao wamerundikana katika makambi matatu: Juba, Bantiu na Malakal. Akianza hotuba hiyo amesema katika ardhi hiyo pendwa iliyopigika wamemaliza kuinua sala nyingi mbinguni: sauti tofauti zilizoungana, kwa kutengeza sauti moja tu. Kwa pamoja na Watu watakatifu wa Mungu, wamesali kwa ajili ya watu hao waliojeruhiwa. Kama wakristo kusali ndilo jambo la kwanza na muhimu ambalo wameitwa kufanya ili kuweza kutembea vyema na kuwa na nguvu ya kutembea. Kusali, kuhudumia na kutembea pamoja ndiyo maneno matatu ambayo Baba Mtakatifu Francisko amependa kuyatafakari jioni hiyo. Akianza na neno kusali, amebainisha kwamba juhudi kubwa ya jumuiya ya kikristo katika kuhamasisha binadamu, katika mshikamao na katika amani ingekuwa bure bila sala. Kiukweli hatuwezi kuhamasisha amani bila kumwomba Yesu “Mfalme wa amani (Is 9,5). Kile ambacho kinafanyiwa wengine na kushirikishwa na wengine kwanza ni zawadi ya bure ambayo inapokelewa na mikono mitupu kutoka Kwake. Ni neema iliyo safi kabisa. ni wakristo kwa sababu wamependwa bure na Yesu, Papa Francisko amebainisha.
Akikumbuka hotuba yake aliyotoa awali wakati wa kuanza siku yake akiwa na viongozi wa Kanisa, maaskofu, mapadre, watawa, mashemasi na waseminari amebainisha alivyoongozwa na sura ya Musa na sasa katika muktadha wa sala, amependa kukumbusha tukio moja thabiti la Musa na watu wake, lililoneshwa mbele yake wakati akianza mchakato wa safari ya kuwasindikiza watu wake kuwa huru. Walipofika katika bahari ya Shamu, lilijiwakilisha mbele ya macho yake na wale waisraeli tukio moja kwani mbele yao kulikuwa na kizingiti cha maji; na wakati nyuma yao wanafuatiliwa na jeshi la adui na ngamia na magari yao. Papa ameongeza: Je “Tukio hilo halirejeshi labda, hatua za Nchi hiyo ambalo ilikumbwa na maji ya kifo, kama yale ya majanga ya mafuriko hata vurugu za kisilaha? Kwa hiyo katika hali ngumu ya wasiwasi, ule Musa aliwambia watu kuwa “Msiwe na hofu! Muwe na nguvu na mtaona wokovu wa Bwana” (Kut 14,13). Baba Mtakatifu ameongeza kusema akijiuliza, Je uhakika huo wa Musa ulitokea wapi, wakati watu wake walikuwa wanaendelea kulalamika kwa kuogopa? Nguvu hiyo ilikuwa inatoka katika kusikiliza Bwana, ambaye alikuwa amewahidi kumuonesha utukufu wake. Umoja na Yeye, imani katika Yeye ilikuzwa katika sala, ilikuwa siri ambayo Musa aliweza kuwasindikiza kutoka katika ukandamizwaji hadi kufikia uhuru.
Kwa hiyo ndivyo ilivyo hata sisi katika kusali kunatupatia nguvu ya kwenda mbele, ya kushinda hofu, kutarajia, hata katika giza, wokovu ambao Mungu anauandaa. Zaidi ya hayo sala inavuta wokovu wa Mungu juu ya watu. Sala ya maombi, ambayo ilikuwa tabia ya maisha ya Musa (Kut 32, 11-14) ndiyo ambayo wanayoalikwa hasa wao kama Wachungaji wa Watu watakatifu wa Mungu. Na ili Bwana wa amani aweze kuingilia kati mahali ambapo watu hawawezi kuijenga, inahitajika sala; shauku ya maombi ya sala yasiyo katika. Baba Mtakatifu Francisko ameomba kusali katika hilo, katika tofauti za imani, na wahisi kuungana kati yao kama familia moja, na kuhisi kuwajibika kusali kwa ajili ya wote. Katika maparokia yote, makanisa yote, mikutano ya ibada na sifa ni kusali bila kuchoka na maelewano (Mdo 1,14),kwa sababu Sudan Kusini, kama watu wa Mungu katika Maandiko matakatifu, “iweze kufikia Nchi ya ahadi” , kwa utulivu na kwa usawa ardhi yenye rutuba na tajiri waliyonayo na kujazwa na ile amani iliyoahidiwa lakini ambayo kwa bahati mbaya bado haijafika.
Kutokana na sababu ya amani, wote wanaalikwa, katika nafasi ya pili kuwa wahudumu. Hii ni kwa sababu Yesu anapenda kuwa wahudumu wa amani ( Mt 5,9), anataka kuwa Kanisa lake lisiwe tu ishara na chombo cha umoja wa kina na Mungu, lakini hata la umoja kwa ajili ya binadamu wote (Lg1). Kristo kiukweli kama anavyokumbusha Mtume Paulo: “ Yesu ni amani yetu”, kwa usahihi alisema:“Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga (Waef 2,14). Kwa hiyo amani ya Mungu na sio tu mapatano kati ya migogoro lakini umoja wa kidugu ambao unawafikia, sio kutoka katika kunyonya, bali wa kusamehe, sio kutokana na kuzidi nguvu, lakini ni kutoka katika kuridhiana, na sio kushurutisha. Shauku ni kubwa sana ya amani kutoka Mbinguni, ambaye ilitangazwa tayari wakati wa kuzaliwa kwa Kristo: “ Amani duniani, na amani kwa watu wenye mapenzi mema( Lk 2,14). Na uchungu ulikuwa mkubwa wa Yesu kwa sababu ya kukataliwa zawadi aliyokuja kuileta ambaye Yeye mwenyewe alilia Yerusalemu, akisema: “Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako”.
Baba Mtakatifu Francisko amewaomba kwa maana hiyo, kufanyia kazi bila kuchoka kwa ajili ya amani ambayo Roho wa Yesu na Baba anatoa mwaliko wa kuijenga; amani ambayo ni fungamani katika utofauti, na ambayo inahamasisha umoja katika wingi. Hii ni amani ya Roho Mtakatifu ambaye analeta maelewano katika tofauti, wakati Roho wa adui wa Mungu na mtu analeta utofauti wa kugawanya. Kuhusiana na hilo, Maandiko matakatifu papa ameongeza yanasema: “Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake” (1Yh 3,10). Kwa hiyo anayesema kuwa ni mkristo lazima achague ni sehemu gani ya kukaa. Anayemfuata Kristo anachagua amani daima; anayesababisha vita na vurugu anasaliti Bwana na kukana Injili yake. Mtindo ambao Yesu anatufundisha huko wazi ni wa kupenda wote, kwa sababu wote wamependwa kama wana wa Baba mmoja ambaye yuko mbinguni.
Upendo wa kikristo sio tu kwa walio karibu, lakini kwa kila mmoja kwa sababu kila mtu katika Yesu ni jirani yetu, kaka na dada hadi yule adui (Mt 5,38-48): kwa sababu hiyo wale wote ambao wanahusika kuwa watu wetu, hata kama ni kabila tofauti “Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi” (Yh 15,12): hiyo ni amri ya Yesu, ambayo inapingana na kila maono ya kikabila. Na kuwa wote wawe kitu kimoja (Yh 17,21): Na hiyo ni sala ya Yesu kwa Baba yake kwa ajili yetu waamini. Ombi la Baba Mtakatifu na msisitizao kwa hiyo ni kuifanyia kazi amani, kwa ajili ya umoja kidugu kati ya wakristo na kusaidiana ili ujumbe wa amani upate njia katika jamii, kueneza mtindo usio na vurugu wa Yesu, dhidi ya utamaduni unaojikita juu ya roho ya kulipiza visasa; kwa sababu Injili isiwe hotuba tu ya kidini lakini iwe ya unabii ambao unageuka kuwa hali halisi katika historia. Vile vile amesisitiza kuifanyia kazi amani na kuisuka amani na kuishona, lakini kamwe isikatwe na kuichana. Papa ameomba wamfuante Yesu nyuma yake huku wakipiga hatua ya pamoja katika njia ya amani (Lk 1,79).
Neno la tatu ambalo Papa amefafanua amesema baada ya kusali na na kufanyia kazi, kuna haja ya kutembea pamoja. Kwa maana hiyo amesema katika Sudan Kusini kwa miongo kadhaa, jumuiya za Kikristo zimejitolea sana kukuza njia za upatanisho. Kwa hiyo amependa kuwashukuru kwa ushuhuda huo mzuri wa imani, uliozaliwa kwa utambuzi sio kwa maneno tu, lakini kwa vitendo na kwamba kabla ya migawanyiko ya kihistoria kuna ukweli usiobadilika: kwa sababu wao ni Wakristo na wa Kristo. Ni jambo zuri kwamba, katikati ya migogoro mingi, imani ya Kikristo haijawahi kuwasambaratisha watu, lakini imekuwa, na bado ni sababu ya umoja. Urithi wa kiekumene wa Sudan ya Kusini ni hazina ya thamani, sifa kwa jina la Yesu, tendo la upendo kwa Kanisa mchumba wake, kielelezo cha ulimwengu kwa njia ya umoja wa Kikristo. Ni urithi unaopaswa kuhifadhiwa katika roho ile ile: migawanyiko ya kikanisa ya karne zilizopita haiwaathiri wale wanaoinjilishwa, lakini hupandaji wa Injili unachangia kueneza umoja zaidi. Kwa hiyo ukabila na ubinafsi unaochochea ghasia nchini husiathiri mahusiano baina ya dini; badala yake ushuhuda wa umoja wa waamini umiminwe kwa watu.
Katika mantiki hiyo Papa Francisko amependa kupendekeza maneno mawili muhimu kwa ajili ya mwendelezo wa ziara hiyo kwamba, iwe mchakato wa safari ya kumbukumbu na bidii. Kumbukumbu ni kwamba hatua za mchakato wanazochukua zifuate nyayo za watangulizi wao. Wasiogope kutokuwa na uwezo, kinyume chake wahisi kusukumwa na wale waliwatengenezea njia, kwa mfano kama katika mbio za kupokezana vijiti, kuchukua kijiti ili kuharakisha kufikia lengo la ushirika kamili na unaoonekana. Baba Mtakatifu aidha amesema neno jingine la kujitolea kwa bidii kwamba , ni kutembea kuelekea umoja wakati upendo ni thabiti, na wakati kwa pamoja wanasaidia wale walio pembezoni, wale waliojeruhiwa na kukataliwa. Tayari wanafanya hivyo katika nyanja nyingi, kwa mfano amefikiria hasa juu ya huduma ya afya, elimu, upendo na kwamba ni msaada mingapi ya haraka na ya lazima wanayoitoa kwa idadi ya watu!
Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru kwa hilo. Amewaomba waendelee na kamwe wasishindane, lakini wawe kama wanafamilia; kaka na dada ambao, kwa kuwahurumia wanaoteseka, wapendwa wa Yesu, wanamtukuza Mungu na kutoa ushuhuda wa umoja anaoupenda. Baba Mtakatifu aidha ameeleza kuwa wamewafika wakiwa wanahija katikati yao, Watu watakatifu wa Mungu wakiwa katika mwendo. Hata kama wako mbali kimwili, watakuwa na karibu kiroho kila wakati. Waanze upya kila siku kwa kuombeana wao kwa wao na kwa wengine, kwa kufanya kazi pamoja kama mashuhuda na wapatanishi wa amani ya Yesu, kwa kutembea katika njia moja, kuchukua hatua madhubuti za upendo na umoja. Katika kila jambo, wapendane kwa dhati, na kwa moyo wa kweli (1 Pt 1:22).