Papa Francisko Sayansi Halisi Izingatie Kanuni Maadili na Utu Wema
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jumuiya ya Max Planck ya Kuendeleza Tafiti za Kisayansi isiyo ya Kiserikali “The Max Planck Gesellschaft” ilianzishwa kunako mwaka 1911 huko nchini Ujerumani kama “Jumuiya ya Kaiser Wilhelm” na baadaye kunako mwaka 1948 ilibadilishwa jina na kuitwa “Jumuiya ya Max Planck” kwa heshima ya Rais wake wa zamani, Mwanafizikia wa kinadharia Max Planck. Taasisi hii imewawezesha watafiti binafsi na kutoka katika taasisi nyingine kuweza kujikita katika maendeleo ya kisayansi, katika maeneo maalum ya tafiti zao kwa kuzingatia viwango vya juu vya kisayansi bila kuingiliwa na mafao yenye asili ya kisiasa au kiuchumi. Hili ni jambo muhimu sana kwa watafiti tangu pale wanapoanza kuzama hadi wanapochapisha tafiti zao na jinsi ambavyo tafiti hizi zinatumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Matumizi ya Sayansi yanapaswa kuchukuliwa kuwa ni sehemu ya mafao ya wengi na “Jumuiya ya Max Planck” inaweza kuchangia dhamana hii kwa ufanisi mkubwa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu, Alhamisi tarehe 23 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na “Jumuiya ya Max Planck” katika hotuba yake amekazia umuhimu wa Sayansi kujikita katika kanuni maadili na utu wema pamoja na kanuni ya kiufundi inayowajibisha na hivyo kuondoa kabisa uwajibikaji wa kimaadili unaotambua kipi chema cha kufuata au kibaya cha kuacha, bali kuangalia tu matokeo ya mwisho.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika ulimwengu mamboleo kuna haja ya kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, Sayansi inakuwa ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maendeleo makubwa ya Sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa kidigitali, yamesaidia maboresho makubwa katika matumizi ya “Artificial Intelligence” yaani “akili bandia” katika sekta mbali mbali za maisha ya mwanadamu, iwe kwa mtu binafsi au jamii katika ujumla wake. Mapinduzi haya makubwa ya teknolojia yanawawezesha watu kujifahamu sanjari na kuufahamu ulimwengu unaowazunguka, kiasi hata cha kuathiri maamuzi, uwezo wa kufikiri na kutenda katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Leo hii utashi wa mwanadamu unaathiriwa kwa namna ya pekee na matumizi ya “akili bandia” kutokana na mchango wake mkubwa!
Baba Mtakatifu Francisko anaonya kwamba mwingiliano wa utambuzi wa akili ya mwanadamu na mashine unaweza kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya mwanadamu “Homo Sapiens” bila ya kutambua makusudi na lengo lake la jumla. Kimsingi ni jambo la kimaadili lisilo kubalika la kutenganisha uwezo wa kutenda na akili kwa makusudi mazima, matokeo yake ni kanuni maadili na utu wema itashindwa kufanya kazi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, “Jumuiya ya Max Planck” itaweza kuchangia kwa ufanisi mkubwa katika mjadala huu tete. Katika ulimwengu mamboleo, kumeibuka kanuni ya kiufundi inayowajibisha na hivyo kuondoa kabisa uwajibikaji wa kimaadili unaotambua kipi chema cha kufuata au kibaya cha kuacha, bali kuangalia tu matokeo ya mwisho. Hapa kinachopewa kipaumbele cha kwanza ni utendaji wake bila kuangalia madhara yake kimaadili. Kanisa haliwezi kukubali mwelekeo huu na badala yake, kuna haja ya kurejea tena katika utamaduni unaowajibika katika ulinzi na tunza ya wengine, inayozingatia madhara na wala si kwa kusoma matokeo yaliyopatikana. Ikumbukwe kwamba, binadamu anawajibika kwa kila anachokifanya, kile kijacho na uamuzi wake.