Tafuta

Cookie Policy
The portal Vatican News uses technical or similar cookies to make navigation easier and guarantee the use of the services. Furthermore, technical and analysis cookies from third parties may be used. If you want to know more click here. By closing this banner you consent to the use of cookies.
I AGREE
Toccata in do minore
Ratiba Podcast
Papa Francisko: Tarehe 24 Februari 2023, yaani mwaka mmoja uliopita, Urusi iliivamia Ukraine na huo ukawa ni mwanzo wa vita ya kipuuzi kabisa. Papa Francisko: Tarehe 24 Februari 2023, yaani mwaka mmoja uliopita, Urusi iliivamia Ukraine na huo ukawa ni mwanzo wa vita ya kipuuzi kabisa.  (ANSA)

Papa Francisko: Vita ya Urusi na Ukraine: 2022-2023: Madhara Yake:Kilio cha Amani

Tarehe 24 Februari 2023, yaani mwaka mmoja uliopita, Urusi iliivamia Ukraine na huo ukawa ni mwanzo wa vita ya kipuuzi kabisa, ambayo imesababisha mateso makubwa kwa watu wa Mungu nchini Ukraine. Baba Mtakatifu Francisko katika muktadha wa kumbukizi hii anasema, jambo la kujiuliza ni ikiwa kama kumekuwepo na juhudi za kutosha ili kukomesha vita hii? Kilio cha Amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tarehe 24 Februari 2023, yaani mwaka mmoja uliopita, Urusi iliivamia Ukraine na huo ukawa ni mwanzo wa vita ya kipuuzi kabisa, ambayo imesababisha mateso makubwa kwa watu wa Mungu ndani nan je ya Ukraine. Baba Mtakatifu Francisko katika muktadha wa kumbukizi hii anasema, jambo la kujiuliza ni ikiwa kama kumekuwepo na juhudi za kutosha ili kukomesha vita hii?  Si rahisi kuweza kujibu kwamba, diplomasia ya Kimataifa ilitia nia ya dhati kabisa ili kuhakikisha kwamba, vita inakoma, amani inatawala. Baba Mtakatifu anasema, hakuna ushindi wa kweli unaojengwa na kusimikwa juu ya vifusi na damu ya watu wasiokuwa na hatia. Takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wakimbizi milioni 5 wanaokimbia vita na baridi kutoka nchini Ukraine. Idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji hawa wamehifadhiwa nchini Poland, Ujerumani na Jamhuri ya Watu wa Czech. Lakini takwimu zinaonesha kwamba, wakimbizi na wahamiaji waliorodheshwa Barani Ulaya ni zaidi ya watu milioni 7.8. Kuna umati mkubwa wa watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao na hatimaye, kujikuta ni watu wasiokuwa na makazi maalum hata ndani ya nchi yao wenyewe na idadi yao ni zaidi ya watu milioni 14.

Vita kati ya Ukraine na Urusu imesababisha maafa makubwa
Vita kati ya Ukraine na Urusu imesababisha maafa makubwa

Takwimu zinaonesha kwamba, watu zaidi milioni 18 wanahitaji msaada wa dharura na kwamba, watu waliofariki dunia kutokana na vita hiyo kwa sasa wamefikia raia zaidi ya 8, 000 na huku wengine 13, 300 walibaki kuwa ni majeruhi. Katika vita hii isiyokuwa na macho kuna miji sita imeharibiwa vibaya sana kiasi kwamba, haifai kwa maisha ya binadamu. Kuna majimbo manne ambayo yamejitenga na kuwa ni sehemu ya Urusi. Inakadiriwa kwamba, vita hii imezalisha deni kiasi cha dola bilioni 108, deni la nje, litakalolipwa na Ukraine kwa kipindi cha miaka mingi ijayo. Wachambuzi wa mambo wanasema, tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia 1939-1945, hakuna nchi ya Ulaya iliyoivamia kijeshi nchi nyingine na kwa kiasi kikubwa ilionekana masuala ya kupigana vita yatabaki katika vitabu vya historia pekee. Kumbe, uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine umetia doa diplomasia na mahusiano ya Kimataifa. Urusi ilidai kwamba, uvamizi huu ulikuwa na lengo la kujiimarisha kimkakati upande wa Jeshi na pili ilikuwa ni kuondoa hatari za siasa za kibaguzi nchini Ukraine. Kimsingi vita hii imevunja makubaliano ya kuundwa kwa Jumuiya ya Nchi Huru, Mkataba wa nchi mbili kati ya Urusi na Ukraine, Mkataba wa mpaka unaotambulika kimataifa wa Urusi na Ukraine, Mkataba wa Umoja wa Mataifa, Sheria ya Helsinki ya 1975 pamoja na Mkataba wa Budapest.

Mateso ya watu wasiokuwa na hatia.
Mateso ya watu wasiokuwa na hatia.

Vita hii imepelekea kupanda zaidi kwa bei ya nishati ya mafuta na hivyo kuibua mnyororo wa kupanda kwa bei za uzalishaji, usafirishaji na ugavi wa bidhaa. Tatizo kubwa zaidi kiuchumi ni kwamba sasa nchi nyingi zimelazimika kutumia fedha nyingi zaidi za kigeni kuagiza nishati ya mafuta kuliko kawaida na hili limeathiri akiba ya fedha za kigeni ya nchi husika na kupunguza matumizi ya fedha ambazo zingetumika kwenye mambo mengine muhimu. Urusi na Ukraine ni wazalishaji na wasambazaji wakuu wa ngano na mazao mengine ya nafaka duniani. Vita hii imeongeza gharama ya mazao ya nafaka na hivyo kupelekea baadhi ya nchi kukosa uhakika na usalama wa chakula. Nchi zile zilizokuwa zinafanya biashara ya moja kwa moja na Urusi pamoja na Ukraine zinajikuta zikiwa na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na vita kupamba moto. Baba Mtakatifu Francisko katika kumbukizi ya mwaka mmoja tangu kuzuka kwa vita kati ya Urusi na Ukraine, anatoa wito wa nguvu kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti kikamilifu ili kuhakikisha kwamba, vita hii inafikia ukomo, ili hatimaye, kuanza majadiliano ya amani katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kamwe amani haiwezi kujengwa kwenye vifusi na damu ya watu wasiokuwa na hatia!

Vita imesabisha majanga makubwa kwa watu na mali zao
Vita imesabisha majanga makubwa kwa watu na mali zao

Kwa upande wake, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa, anasema Kanisa bado lina ndoto ya haki, amani na maridhiano kati ya Urusi na Ukraine. Litaendelea kuwa karibu na watu wote wa Mungu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita. Vatican kwa kutumia diplomasia ya Kimataifa, inaendelea kuwahamasisha wadau mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, vita inakoma, amani inarejea tena kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ubalozi wa Vatican umeendelea na shughuli zake nchini Ukraine licha ya hatari kubwa iliyoko, kama kielelezo cha mshikamano wa udugu wa kibinadamu na uwepo angavu wa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu wanaoteseka nchini Ukraine. Baba Mtakatifu ameendelea kuwasha moto wa ndoto ya amani kila mara alipobahatika kupata nafasi ya kuzungumza. Anasema, kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, vita kamwe si suluhu ya shida, changamoto na matatizo yanayoikabili Jumuiya ya Kimataifa. Haya ni maneno ya kinabii, lakini daima duniani kutakuwepo na “viongozi wababe” wanaopenda kujimwambafai kwa kutumia mtutu wa bunduki “kuwashikisha wengine adabu.” 

Jumuiya ya Kimataifa  haijafanya juhudi za kutosha kukomesha vita
Jumuiya ya Kimataifa haijafanya juhudi za kutosha kukomesha vita

Baba Mtakatifu anasema “dhana ya vita ya haki na halali” kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Vita ni kielelezo cha kushindwa kwa siasa na utu na inabaki kuwa ni aibu kwa Jumuiya ya Kimataifa. Mtakatifu Paulo VI tarehe 4 Oktoba 1965 alipokuwa analihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alikemea sana vita, akaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa haki na amani. Mtakatifu Yohane XXXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” uliochapishwa tarehe 11 Aprili 1963 anasema, amani inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu: utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya amani sehemu mbalimbali za dunia, licha ya shida, matatizo na changamoto mbalimbali zinazoendelea kujitokeza kwenye uso wa dunia. Ndoto ya matumaini na amani ni muhimu kwa ajili ya ujenzi mpya wa Ukraine unaosimikwa katika mchakato wa haki, amani na upatanisho.

Papa Vita Ukraine
24 Februari 2023, 15:20
Prev
March 2025
SuMoTuWeThFrSa
      1
2345678
9101112131415
16171819202122
23242526272829
3031     
Next
April 2025
SuMoTuWeThFrSa
  12345
6789101112
13141516171819
20212223242526
27282930