Siku ya 27 ya Kuombea Watawa Duniani kwa Mwaka 2023: Kauli mbiu: "Ndugu Katika Utume" Siku ya 27 ya Kuombea Watawa Duniani kwa Mwaka 2023: Kauli mbiu: "Ndugu Katika Utume" 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya 27 ya Watawa Duniani: Udugu Katika Utume

Siku ya Kuombea Watawa kwa Mwaka 2023 ilinogeshwa na kauli mbiu “Ndugu Katika Utume.” Tangu mwanzo kabisa, Kristo Yesu Mfufuka alitaka Kanisa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, chini ya usimamizi na maongozi ya Roho Mtakatifu. Watu watakatifu wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanashiriki pia: Ukuhani, Unabii na Ufalme.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1997 alianzisha Siku ya Kuombea Watawa Duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Februari sanjari na Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni. Sikukuu hii inaadhimishwa Siku 40 tangu Mama Kanisa alipoadhimisha Noeli ya Bwana, siku ya kutolewa Bwana Hekaluni na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu mintarafu sheria, kanuni na taratibu za Kiyahudi. Lakini katika ukweli wake wa ndani, hii ni Sikukuu ambayo Kristo Yesu alikuwa anakutana na watu wake waliokuwa wanamsubiria kwa kwa imani na matumaini. Wakiongozwa na Roho Mtakatifu Mzee Simeone na Nabii Ana Binti Fanueli wanamtambua Kristo Yesu kuwa ni Mkombozi wa Ulimwengu, kwa furaha, imani na matumaini wakamtolea ushuhuda. Leo hii, waamini wanaitwa na kutumwa kumtolea ushuhuda Kristo Yesu kwa: Neno, Sakramenti za Kanisa, Huduma makini kwa jirani, Historia ya maisha yao pamoja na maisha adili na matakatifu. Watawa wawe ni mashuhuda wa furaha ya Injili inayowakutanisha watu na hivyo kuwa tayari kuweza kuwapelekea wengine mwanga wa Injili na Upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake. Huu ni ushuhuda na utume wa Kinabii. Lengo la Siku ya Kuwaombea Watawa ni kumshukuru Mungu kwa ajili ya watawa ambao wanajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani kwa kufuata mashauri ya kiinjili.

Watawa wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili
Watawa wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili

Hii ni fursa kwa watawa kupyaisha tena wito, maisha na utume wao, tayari kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu na kuendelea kumtumainia Mungu katika safari ya maisha yao licha ya changamoto na fursa mbalimbali wanazokumbana nazo katika maisha. Wito wa kitawa ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo Yesu. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, hii ni siku ambayo inapaswa kuwasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutambua na kuwaenzi watawa wanaoshiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa njia ya utume wa kufundisha, kuihubiri na hatimaye, kuishuhudia Injili, ili watu wote wapate imani na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa njia ya imani, Ubatizo pamoja na kuzishika Amri za Mungu ambazo Kristo Yesu amezitolea muhtasari wa kukazia upendo kwa Mungu na jirani. Sikukuu hii kwa Mwaka huu imeadhimishwa wakati wa Hija ya 40 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 3 Februari 2023 iliyonogeshwa na kauli mbiu “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Baba Mtakatifu Alhamisi tarehe 2 Februari 2023 alikutana na kuzungumza na makleri, watawa na majandokasisi, kama sehemu ya maadhimisho ya Sikuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya 27 ya Kuombea Watawa Duniani kwa Mwaka 2023. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu aliwaalika watu wa Mungu kuwaombea watawa na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa idadi kubwa ya miito kutoka nchini DRC.

Watawa wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili
Watawa wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili

Viongozi wa Kanisa wawe ni kielelezo cha huduma na mashuhuda wa upendo wa Mungu, alama ya uwepo angavu wa Kristo Yesu na upendo wake usiokuwa na kifani. Watawa wanatakiwa kujenga utamaduni wa maisha ya sala, kushinda kishawishi cha kumezwa na malimwengu na kuishi maisha ya wakfu juu juu bila kuzamisha mizizi katika Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Mafundisho tanzu na ushuhuda amini kwa Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika muktadha wa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Kardinali Joao Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume na mahubiri kutolewa na Askofu mkuu Jose' Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Ibada ya Misa Takatifu ilitanguliwa na tafakari ya kina kuhusu Sala ya Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya ukombozi. Mkazo ni watawa kuhakikisha kwamba wanakuwa ni mashuhuda wa wahudumu wa Injili ya upendo kwa maskini wa hali na kipato na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wanapaswa wawe ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti na wahanga wa ukosefu wa haki msingi za binadamu.

Kauli mbiu; Ndugu katika utume
Kauli mbiu; Ndugu katika utume

Huu ni mwaliko kwa watawa kuendelea kujikita katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, ili kweli katika familia kubwa ya binadamu wote watambuane kama ndugu wamoja, licho ya tofauti zao msingi. Siku ya Kuombea Watawa kwa Mwaka 2023 ilinogeshwa na kauli mbiu “Ndugu Katika Utume.” Tangu mwanzo kabisa, Kristo Yesu Mfufuka alitaka Kanisa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, chini ya usimamizi na maongozi ya Roho Mtakatifu. Watu watakatifu wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanashiriki pia: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo, kumbe hata wao wanatumwa kutangaza, kushuhudia na kuyatakatifuza malimwengu kwa tunu msingi za Kiinjili. Watawa kwa namna ya pekee kabisa wanapaswa kujikita katika Mashauri ya Kiinjili yaani: Utii, Ufukara na Usafi kamili, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake pamoja na huduma kwa watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu unatajirishwa na karama za Mashirika mbalimbali ya Kitawa na Kazi za Kitume na hivyo Kanisa linakuwa na uwezo wa kutangaza Injili katika medani mbalimbali za maisha ya waamini.

Udugu katika huduma kama ushuhuda wa Uinjilishaji
Udugu katika huduma kama ushuhuda wa Uinjilishaji

Askofu mkuu Jose' Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume katika mahubiri yake aliwataka watawa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, Kristo Yesu akipewa kipaumbele cha kwanza katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kama zawadi safi kutoka kwa Mungu. Changamoto kubwa kwa watawa katika ulimwengu mamboleo ni kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa udugu wa kibinadamu, dhamana inayowataka watawa kujifunga kibwebwe kwelikweli! Watawa wajitahidi kujenga na kudumisha ushirika; kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa kuwashuhudia ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu. Kristo Yesu akiwa ni kiini cha maisha ya watawa, awasaidie katika kutekeleza mchakato wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu wateule wa Mungu, huku taa zao za matumaini zikiwa zinawaka ili kushuhudia uzuri wa kumwamini na kumfuasa Kristo Yesu katika maisha na utume wao hadi miisho ya dunia.

Karama za Mashirika mbalimbali ni  zawadi za Roho Mt.
Karama za Mashirika mbalimbali ni zawadi za Roho Mt.

Naye Ndahani Lugunya anasema, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya, O.F.M. Cap. wa Jimbo kuu la Dodoma, katika Maadhimisho ya Sikukuu hii, amekazia umuhimu wa watawa kujikita katika kumwilisha Mashauri ya Kiinjili katika uhalisia wa maisha yao kwa ajili ustawi, maendeleo ya Mashirika na Kanisa katika ujumla wake. Wawe ni watu wa kiasi na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu kwa uchu wa mali na madaraka. Wajisadake bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Watawa waboreshe maisha yao kwa: Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Sala na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Wajenge utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu, ili kuimarisha mafungamano yao na Kristo Yesu, tayari kumtangaza na kumshuhudia kwa watu wa Mataifa. Watawa wajitahidi kuunganisha mateso, mahangaiko na changamoto za maisha na Mateso ya Kristo Yesu Msalabani, ili waweze hatimaye, kuwa ni baraka kwa watu wa Mungu. Kwa mfano wa maisha na utume wao, watawa wawe ni mashuhuda wa hamasa ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa na hususan wito wa maisha ya kuwekwa wakfu na upadre. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa la Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska, Kiwanja cha Ndege, Jimbo kuu la Dodoma.

Watawa Duniani

 

13 February 2023, 15:18