Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani tarehe 11 Februari 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Mtunze”: Huruma kama zoezi la Sinodi ya Uponyaji.” Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani tarehe 11 Februari 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Mtunze”: Huruma kama zoezi la Sinodi ya Uponyaji.”   (Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani 11 Februari 2023: Mtunze!

Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani yananogeshwa na kauli mbiu “Mtunze”: Huruma kama zoezi la Sinodi ya Uponyaji.” Papa anakazia umuhimu wa kutenda kadiri ya mtindo wa Mungu; kwa kufuata mfano wa Msamaria mwema, ili kuondokana na upweke hasi na hali ya kutelekezwa. Kanisa liwe ni hospitali, lijenge ushirikiano na udugu katika huduma kwa wagonjwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Wagonjwa Duniani ni nafasi ya kutafakari kanuni maadili na utu wema; sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wagonjwa na wazee, tayari kusoma alama za nyakati kwa kusikiliza na kujibu kilio cha wagonjwa na wale wanaoteseka. Hii ni siku maalum kwa ajili ya kukoleza uragibishaji na maadhimisho yanayokusudia kuwasaidia waamini kusali na kushiriki mateso ya wagonjwa; na kwa wagonjwa wenyewe kutolea mateso na mahangaiko yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu na hatimaye, kuwaonjesha wagonjwa kuwa ni sura na ufunuo wa Kristo Yesu, anayeteseka kati pamoja nao. Siku ya Wagonjwa Duniani, ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 13 Mei 1992 na kuadhimishwa kwa mara ya kwanza kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes nchini Ufaransa kunako tarehe 11 Februari 1993. Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani tarehe 11 Februari 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Mtunze”: Huruma kama zoezi la Sinodi ya Uponyaji.” Baba Mtakatifu katika ujumbe wake anakazia umuhimu wa kutenda kadiri ya mtindo wa Mungu; kwa kufuata mfano wa Msamaria mwema, ili kuondokana na upweke hasi na hali ya kutelekezwa. Kanisa liwe ni hospitali katika uwanja wa mapambano, kwa kujielekeza zaidi katika ushirikiano na udugu wa kibinadamu katika huduma kwa wagonjwa. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wafanyakazi katika sekta ya afya kwa huduma na tafiti zao. Huu ni mwaliko kwa jumuiya za Kikristo kujipambanua katika huduma kwa wagonjwa.

Mtunze: Huruma kama zoezi la Sinodi la Uponyaji
Mtunze: Huruma kama zoezi la Sinodi la Uponyaji

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kushirikiana na kushikamana, ili kutokana na mang’amuzi ya udhaifu wa binadamu na magonjwa yanayomwandama, watende kadiri mtindo wa Mungu unaofumbatwa katika ukaribu, huruma na mapendo. Mwenyezi Mungu katika Maandiko Matakatifu anasema “Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo wangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU. Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliotangatanga, nitawatibu waliojeruhiwa, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.” Eze 34: 15-16. Mchoko, magonjwa na udhaifu wa mwili ni sehemu ya vinasaba vya safari ya maisha ya mwanadamu, vinavyohitaji ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika mfano wa Msamaria mwema, ili kuganga kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini, ili kuwaokoa na kuwasaidia wale wanaotelekezwa kwenye vipaumbele vya jamii kama ilivyokuwa kwa yule Msamaria mwema kwani upendo ni njia ya uzima wa milele. Waamini wanapaswa kusimama kidete kulinda maisha, utu na heshima ya binadamu. Kuna ukosefu mkubwa wa haki msingi za binadamu unaopelekea kukosekana kwa usawa na hasa zaidi kutokana na vita pamoja na mambo mengine, kiasi kiwamba, mateso na mahangaiko ya binadamu yanatendeka katika muktadha wa utamaduni.

Ni wakati wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Msamaria mwema
Ni wakati wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Msamaria mwema

Kuna watu wanaoishi katika upweke hasi na hali ya kutelekezwa, wanaoweza kusaidiwa kwa kuwajali, kuwaonesha upendo na hivyo kuwaondolea hali yao, kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, ambaye alitenda tofauti na sasa ni mfano bora wa ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu. Upweke hasi unaweza kumpelekea mtu hata kushindwa kuona thamani ya maisha yake na hivyo kuonekana kuwa kama “mzigo” kwa jirani zake. Kumbe, hata katika mateso na mahangaiko ya watu, Mama Kanisa hana budi kuwa ni “Hospitali katika uwanja wa mapambano” kwani historia inaonesha kwamba, utume wake unasimikwa katika huduma, mwaliko kwa waamini kusimama na kutafakari, na hatimaye kuchukua hatua, kuganga na kuponya na hatimaye, kuwashika mkono walioelemewa na udhaifu pamoja na magonjwa ili kuwainua tena. Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani ni mwaliko wa sala na ujirani mwema, tayari kugeuza vipaumbele vya viongozi wa kiuchumi, kitamaduni na kisiasa na hivyo kuanza kujielekeza katika mchakato wa ushirikiano na mshikamano unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu, kwa watu kukutana mubashara, hali inayoweza kupanuliwa na kuingizwa katika huduma bora zaidi ya afya inayowashirikisha wafanyakazi katika sekta ya afya na ustawi wa jamii;  wanafamilia pamoja na watu wa kujitolea, wanaoweza kuwa ni ushuhuda angavu kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na mapambano dhidi ya maovu yanayotendeka kila siku katika uso wa dunia.

Papa anawapongeza wahudumu na watafiti katika sekta ya afya
Papa anawapongeza wahudumu na watafiti katika sekta ya afya

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi katika sekta ya afya na tafiti mbalimbali ambao wameendelea kujipambanua kama mashujaa. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 umeibua utaalam na mshikamano ambao umefunua udhaifu na mapungufu makubwa katika miundo mbinu ya sekta ya afya, changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha serikali mbalimbali zinatenga bajeti ya kutosha, ili kuhakikisha kwamba, walau watu wanapata haki zao msingi katika huduma ya afya. “Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na chochote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.” Lk 10:35. Huu ni ushuhuda kwamba, jumuiya ya waamini na watu wenye mapenzi mema inaweza kujenga mahusiano na mafungamano yanayowatambulisha na wagonjwa pamoja na wadhaifu, kiasi cha kujenga jamii shirikishi, kwa kuwanyanyua wadhaifu na wagonjwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kielelezo cha upendo na utandawazi unaojali na kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuyaelekeza mawazo yao kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes katika Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2023, ili kujifunza somo la kinabii ambalo Mama Kanisa amekabidhiwa katika nyakati hizi za kisasa. Si watu wazima na wale wanaofanya shughuli zao barabara ndio wanaopaswa kupewa kipaumbele. Kinyume chake na kwa hakika wagonjwa wako katikati ya watu wa Mungu na Mama Kanisa anasonga mbele pamoja nao kama ishara ya ubinadamu ambamo kila mtu anathamani kubwa mbele ya Mungu na wala hakuna anayepaswa kutelekezwa au kuachwa nyuma. Bikira Maria Mwenye Moyo Safi, awasaidie kuwaombea furaha na ujasiri katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi.

Ujumbe Wagonjwa 2023
09 February 2023, 16:46