Afya ya Papa Francisko Inaendelea Kuimarika: Amepumzika, Amesali na Amepokea Ekaristi Takatifu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano Alasiri, tarehe 29 Machi 2023 alipelekwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma kufanyiwa uchunguzi na kubainika kwamba, alikuwa anakabiliwa na changamoto katika mfumo wa hewa na kwamba, huu si Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Madaktari wamelazimika kumlaza Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya uchunguzi wa kiafya na matibabu zaidi, zoezi linalohitaji siku kadhaa na muda wa mapumziko. Taarifa kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu amepata mapumziko ya kutosha na anaendelea na matibabu na kwamba, anawashukuru wale wote wanaoendelea kumsindikiza kwa sala na sadaka zao, kama kielelezo cha uwepo wao wa karibu katika kipindi hiki, Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Juma Kuu, muda wa kutafakari kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu uletao wokovu! Taarifa ya kitabibu iliyotolewa Alhamisi tarehe 30 Machi 2023 inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alipata wasaa wa kulala vyema usiku na hali yake inaendelea kuimarika polepole. Baada ya kifungua kinywa na sala ya asubuhi, amejipatia nafasi ya kusoma baadhi ya magazeti na kuanza shughuli zake, akiwa hospitalini hapo. Kabla ya chakula cha mchana, amejitenga kwa sala binafsi na baadaye akapokea Ekaristi Takatifu.
Katika siku za hivi karibuni, Baba Mtakatifu alianza kuhisi maumivu kwenye mfumo wa hewa na hii ikawa ni sababu muhimu ya kwenda kumfanyia uchunguzi wa kina, Jumatano tarehe 29 Machi 2023. Hadi wakati huu, uchunguzi na taarifa za madaktari zinasema kwamba, Baba Mtakatifu anaendelea vyema na wala hakuna sababu za msingi za kuhofia afya yake na kwa sasa anahudumiwa katika Idara ya Sayansi ya Magonjwa ya Moyo kwa kushirikiana na Idara nyingine kwa ajili ya uchunguzi wa kina, ili kuhakikisha kwamba, afya ya Baba Mtakatifu Francisko inatengamaa na hivyo kurejea tena katika maisha na utume wake. Itakumbukwa kwamba, Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 29 Machi 2023 imenogeshwa na sehemu ya Maandiko Matakatifu inayoonesha kiri ya Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anayethibitisha kuhusu wito wake akisema: “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1: 22-24. Huu ndio ushuhuda wa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, akionesha shauku ya uinjilishaji na bidii ya kitume, baada ya kutubu na kumwongokea Kristo Yesu. Kutoka katika Torati akaikumbatia Injili; Yeye ambaye ambapo mwanzo alitaka kulidhulumu na kulibomoa Kanisa, sasa anakuwa ni shuhuda wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu, yaani Kanisa, kiasi kwamba, sasa anataka kujisadaka kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu.
Wakati wote wa Katekesi, Baba Mtakatifu alionekana kuwa mchangamfu isipokuwa pale aliponyanyuliwa ili kuketishwa kwenye kiti cha wagonjwa, alionekana kuhisi maumivu makali. Baadaye alipelekwa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, kwa gari la wagonjwa na kulazwa kwenye ghorofa yak umi, ambako kwa sasa macho na vyombo vya mawasiliano ya jamii vimejielekeza zaidi. Ni katika muktadha huu, shughuli zote za Baba Mtakatifu Francisko zilizokuwa zimepangwa zimefutwa hadi pale taarifa nyingine itakapotolewa. Uchunguzi uliofanywa na madaktari hadi sasa unaonesha kwamba, moyo wake unaendelea kufanya kazi vyema na kiasi cha oksijeni kwenye mzunguko wa damu kiko vyema. Madaktari walijielekeza zaidi kuangalia changamoto ya mfumo wa hewa pamoja na moyo. Matokeo yanaridhisha. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, limemtumia salam Baba Mtakatifu Francisko na kumhakikishia kwamba, watu wa Mungu nchini Italia, wanamwombea na kwamba, wanapenda kumzamisha kwenye huruma ya Mungu ili juhudi za madaktari na wauguzi ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa kwake binafsi pamoja na wagonjwa wengine wote. Wakati huo huo, familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma, inapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala kwa Baba Mtakatifu Francisko ambaye amelazwa na hivyo kumwombea neema, baraka na huruma ya Mungu ili aweze kumponyesha haraka, na kuwajalia pia nafuu na hatimaye uponywaji wagonjwa wote wanaoteseka hospitalini na majumbani, sehemu mbalimbali za dunia.
Wakati huo huo, Balozi Georgios F. Poulides, Dekano wa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican yapatayo 183, katika salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu anasema kwa niaba yake na wanadiplomasia wote wa Vatican, wanamtakia uponywaji wa haraka. Ni matumaini ya wanadiplomasia kwamba, Mwenyezi Mungu ataweza kumjalia afya njema na hatimaye, kurejea tena mjini Vatican, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na uzuri wa imani. Taarifa ya kuugua na hatimaye, kulazwa kwa Baba Mtakatifu Francisko zimeenea kwa haraka sana sehemu mbalimbali za dunia. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 4 Julai 2021 majira ya jioni alilazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma kwa ajili ya kufanyia operesheni kubwa kwenye utumbo mpana. Operesheni hiyo ilifanywa na Prof. Sergio Alfieri. Kabla ya kwenda kufanyiwa operesheni kubwa, Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili alisali na kutafakari na waamini pamoja na mahujaji waliofika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuhusu “Kashfa ya Fumbo la Umwilisho.” Kwa sasa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaalikwa kumkumbuka na kumwombea, ili kazi hii ya madaktari ipate kibali na hitimisho lake kwa baraka za Mwenyezi Mungu! Radio Vatican itaendelea kukujuza hali ya Baba Mtakatifu Francisko kadiri taarifa zitakavyokuwa zinatolewa na Hospitali ya Gemelli. Historia inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko na Mtakatifu Yohane Paulo II ndio viongozi wakuu wa Kanisa katika miaka ya hivi karibuni kulazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, kiasi kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema kwamba, Hospitali ya Gemelli kwake ni Ikulu Ndogo ya Tatu, ya Pili kwa wakati ule ilikuwa ni Castel Gandolfo ambayo kwa sasa imegeuzwa kuwa ni eneo la kitalii.