Kardinali Karl-Josef Rauber Mjenzi wa Umoja wa Watu wa Mungu: 1934-2023
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa majonzi makubwa taarifa ya kifo cha Kardinali Karl-Josef Rauber kilichotokea tarehe 26 Machi 2023, akiwa na umri wa zaidi ya miaka 88 huko Jimbo Katoliki la Rottenburg-Stuttgart lililoko nchini Ujerumani. Katika salam za rambirambi alizomtumia Askofu Peter Kohlgraf wa Jimbo Katoliki la Mainz, anasema, Mtumishi mwaminifu wa Mungu Kardinali Karl-Josef Rauber ameitupa mkono dunia na sasa amekwenda kwenye maisha ya uzima wa milele. Zawadi ya maisha, wito na utume wake ameutumia kwa ajili ya huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Maaskofu, kila mmoja peke yake, ni chanzo na msingi unaoonekana wa umoja katika Makanisa yao faridi, yaliyowekwa kwa mfano wa Kanisa lote zima, na katika hayo na kutokana na hayo lipo Kanisa Katoliki lililo moja na pekee. Kwa sababu hiyo kila Askofu huwakilisha Kanisa mwenyewe, na Maaskofu wote pamoja na Baba Mtakatifu, huwakilisha Kanisa lote katika kifungo cha amani, upendo na umoja, LG 23 Kardinali Karl-Josef Rauber katika maisha na utume wake, alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kujenga na kudumisha umoja wa watu wa Mungu, tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 28 Februari 1959 hadi alipong’atuka kutoka madarakani kunako mwaka 2009.
Tarehe 18 Desemba 1982 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni Askofu mkuu na hatimaye, kumweka wakfu tarehe 6 Januari 1983 na kutumwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Uganda hadi alipong’atuka kutoka madarakani tarehe 18 Juni 2009. Amefariki dunia, akiwa amelitumikia Kanisa kama Padre kwa muda wa miaka 64. Kama Askofu amefundisha, akaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa muda wa miaka 40 na kama Kardinali, Mshauri wa Baba Mtakatifu kwa muda wa miaka 8. Kauli yake ya Kiaskofu ilikuwa ni: “Caritas Christi urget nos; ('The Love of Christ compels us'): Upendo wa Kristo Unatuwajibisha.” Baba Mtakatifu anasema kwa hakika Kardinali Karl-Josef Rauber alikuwa ni Mchungaji mwaminifu wa Kanisa, aliyewashirikisha jirani zake upendo wa Kristo katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu anasema, sasa mwishoni mwa maisha yake hapa duniani, aendelee kumsifu na kumtukuza Mwenyezi Mungu kutokana na upendo wake wenye huruma. Mwishoni mwa salam zake za rambirambi, Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume wale wote ambao wameguswa na kutikiswa kwa msiba huu mzito na wale watakaoshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Kardinali Karl-Josef Rauber aliyezaliwa tarehe 11 Aprili 1934 na kunako tarehe 14 Februari 2015 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa na kumsimika kuwa ni Kardinali.