Dominika ya Matawi, tarehe 2 Aprili 2023 ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Dominika ya Matawi, tarehe 2 Aprili 2023 ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.  (Vatican Media)

Juma Kuu Mjini Vatican Kwa Mwaka 2023: Maana Yake Katika Maisha na Utume wa Kanisa

Dominika ya Matawi ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu. Alhamisi kuu, Kanisa linaadhimisha Kumbukumbu ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na huduma ya upendo katika unyenyekevu. Ijumaa kuu, Mama Kanisa anakumbuka mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Jumamosi kuu, Kanisa linasubiria ushindi wa Kristo Yesu Mfufuka! Maadhimisho ya Juma Kuu ni kiini cha Mwaka wa Liturujia ya Kanisa. Ni muda wa sala, toba na wongofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dominika ya Matawi, tarehe 2 Aprili 2023 ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Alhamisi kuu, Kanisa linaadhimisha Kumbu kumbu ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Ijumaa kuu, Mama Kanisa anakumbuka mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Jumamosi kuu, Kanisa katika majonzi makubwa, linasubiria ushindi wa Kristo Yesu Mfufuka! Maadhimisho ya Juma Kuu ni kiini cha Mwaka wa Liturujia ya Kanisa. Ni muda muafaka kwa watu wa Mungu kusali kwa ajili ya kuombea amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu.

Dominika ya Matawi Mmwanzo wa Maadhimisho ya Juma Kuu
Dominika ya Matawi Mmwanzo wa Maadhimisho ya Juma Kuu

Tarehe 2 Aprili 2023 DOMINIKA YA MATAWI itaadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4:00 Asubuhi kwa saa za Ulaya sawa na saa 5: 00 Asubuhi kwa Saa za Afrika Mashariki. Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu, alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu, ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana. Ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu akiwa amepanda Mwana punda na kushangiliwa na Watoto wa Wayahudi wakiwa wamebeba matawi ya mitende mikononi mwao kama kielelezo cha amani na unyenyekevu wake. Matawi yatakayobarikiwa yatatunzwa na waamini kama visakramenti majumbani mwao, kuwakumbusha ushindi wa Kristo Yesu wanaouadhimisha kwa kuandamana, huku wakiwa wamebeba matawi ya mitende mikononi mwao. Kamati ya Liturujia iwaandae vyema waamini ili kuweza kutajirishwa kiroho kutokana na maadhimisho haya! Sherehe hii ni mwanzo wa Maadhimisho ya Juma kuu, au kwa wengi, Juma Takatifu linayotangaza pia Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Kristo Yesu ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Kuingia kwa Kristo Yesu mjini Yerusalemu kunaonesha ujio wa Ufalme wa Mungu: Wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ufalme wa haki, mapendo na amani.

Domina ya Matawi Yesu anaingia Yerusalemu kama Mfalme na Masiha
Domina ya Matawi Yesu anaingia Yerusalemu kama Mfalme na Masiha

Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu. Yeye ni Bwana wa historia na viumbe vyote na hatima ya yote haya ni ufalme wa Kristo aliyedhalilishwa kwa kukamatwa, kuteswa na hatimaye kufa Msalabani kana kwamba, alikua anawania madaraka ya kisiasa, yaani, kuwa ni mfalme wa Wayahudi! Ni kutokana na wasi wasi huu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Pilato alimuuliza Yesu mara mbili, ikiwa kama kweli Yeye ni mfalme. Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa Juma Kuu. Mji wa Yerusalemu kimsingi ni kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa. Yerusalemu ni Mji Mtakatifu unaoheshimiwa na waamini wa dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislam. Kumbe, kwa waamini wa dini hizi, huu ni Mji mkuu wa maisha ya kiroho na kitovu cha majadiliano ya: kiekumene, kidini, kitamaduni, upatanisho na amani huko Mashariki ya Kati! Ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu, kuna haja pia ya kuzingatia maoni ya viongozi wa kidini badala ya kujikita katika maamuzi ya kisiasa peke yake! Utakatifu, Asili na Tunu msingi za Mji wa Yerusalemu zinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wengi.

Tamko la Viongozi wa Kidini Kuhusu Mji Mtakatifu wa Yerusalemu
Tamko la Viongozi wa Kidini Kuhusu Mji Mtakatifu wa Yerusalemu

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Morocco, tarehe 30 Machi 2019 pamoja na Mfalme Mohammed VI wa Morocco walitia saini kwenye Tamko la Mji Mtakatifu wa Yerusalemu Kuwa ni Mahali Pa Kuwakutanisha Watu! Viongozi hawa wanatambua utakatifu, ukuu na umuhimu wa Mji wa Yerusalemu katika maisha ya kiroho, kiutu na kiimani ya waamini wa dini hizi tatu zinazomwabudu Mungu mmoja. Yerusalemu ni mji wa wa amani, amana na urithi wa binadamu wote, hususan waamini wa dini hizi tatu. Ni mahali pa watu kukutana na kwamba, Yerusalemu ni mji wa amani, mahali ambapo watu wanapaswa kuishi kwa utulivu, kwa kuheshimiana na kuthaminiana ili kukuza na kudumisha majadiliano. Ni katika muktadha huu wa maisha ya kiroho na utambulisho wa kitamaduni, Mji Mtakatifu wa Yerusalemu unapaswa kulindwa na kuendelezwa. Ni matumaini ya viongozi hawa kwamba, Mji Mtakatifu wa Yerusalemu, utakuwa huru kwa waamini wa dini hizi tatu kuwa na uhakika wa kuendesha Ibada zao, ili Sala na sadaka zinazotolewa mahali hapa ziweze kumfikia Mwenyezi Mungu, Muumbaji, kwa ajili ya amani na ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu.

Ibada ya Misa Takatifu Kubariki Krisima ya Wokovu
Ibada ya Misa Takatifu Kubariki Krisima ya Wokovu

Tarehe 6 Aprili 2023 ALHAMISI KUU: Ni Sherehe ya Kubariki Mafuta ya Krisma ya Wokovu. Ibada hii itaadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 3:30 kwa saa za Ulaya, sawa na Saa 4:30 kwa Saa za Afrika Mashariki. Kiongozi wa Ibada kwa niaba ya Baba Mtakatifu ambaye ndiye Askofu wa Jimbo la Roma atabariki: Mafuta ya Wakatekumeni, Mafuta ya Wagonjwa pamoja na Krisma ya Wokovu; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo na wanapowekwa wakfu kuwa Mapadre na Maaskofu. Hii ni Siku ya Ufunuo wa Kanisa, Fumbo la Mwili wa Kristo. Wakristo wanapakwa mafuta na kuwekwa wakfu kwa njia ya Roho Mtakatifu kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu baada ya kubatizwa Mtoni Yordani. Kumbe, kwa njia ya Ubatizo na Kipaimara waamini wanatumwa kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kukuza na kudumisha: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, kwa hakika wao wanashiriki pia: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na chombo cha amani, maridhiano na upatanisho. Hii ni Sikukuu ya Mapadre na fursa ya kurudia tena utii kwa Maaskofu mahalia.

Alhamisi Kuu ni Siku Pia ya KUbariki Mafuta ya Krisma ya Wokovu
Alhamisi Kuu ni Siku Pia ya KUbariki Mafuta ya Krisma ya Wokovu

Na kwa Maadhimisho ya Ibada ya Kubariki Krisma ya Wokovu, Mama Kanisa anafunga rasmi kipindi cha Kwaresima na kuanza kujiandaa kuzama zaidi katika Mafumbo ya Kanisa. Mama Kanisa anafundisha kwamba, Kristo Yesu aliwapenda watu wake upeo na alipokuwa anakaribia “Saa yake” ili kutoka hapa ulimwenguni na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, Siku ile ya Alhamisi kuu, walipokuwa wakila, aliwaosha Mitume wake miguu yao na kuwapatia Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma ya upendo, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Akataka pia kuwapatia amana ya upendo huu na kuendelea kubaki kati yao na kuendelea kuwashirikisha Fumbo la Pasaka, aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kielelezo cha sadaka, shukrani, kumbu kumbu endelevu na uwepo wake kati yao katika alama ya Mkate na Divai! Kumbe, Ekaristi Takatifu ni kumbukumbu endelevu ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu inayoadhimishwa na Mama Kanisa hadi Kristo Yesu atakaporudi tena kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho! Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni Sakramenti Pacha na Daraja Takatifu ya Upadre. Mapadre hutekeleza kazi takatifu hasa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, wakitenda kwa nafsi ya Kristo, wakitangaza fumbo lake pamoja na kuyaunganisha maombi ya waamini pamoja na sadaka ya Kristo Msalabani inayoadhimishwa katika Ibada ya Misa Takatifu.

Injili ya Upendo inayomwilishwa katika huduma na unyenyekevu
Injili ya Upendo inayomwilishwa katika huduma na unyenyekevu

Tarehe 7 Aprili 2023 IJUMAA KUU: Kumbukumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ibada ya Ijumaa kuu inatarajiwa kuanzia saa 11:00 jioni majira ya Ulaya sawa na Saa 12: 00 za Jioni kwa Saa za Afrika Mashariki kwa kuongoza na Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, Kuabudu Msalaba pamoja na Ibada ya Komunio Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kuanzia saa 3:15 Usiku kwa saa za Ulaya, Sawa na Saa 4:15 Usiku kwa Saa za Afrika Mashariki, kutakuwa na Adhimisho la Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo.  Fumbo la Pasaka la Msalaba na Ufufuko wa Kristo Yesu ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu ambayo Mitume na Kanisa wanaendelea kuitangaza na kuishuhudia, kama utimilifu wa Mpango wa wokovu kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu uletao wokovu. Mababa wa Kanisa wanasema, imani inaweza kujaribu kutafuta mazingira ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu yaliyotajwa kiaminifu katika Injili na kutangazwa na kushuhudiwa na chemchemi nyingine za historia kusudi iweze kujua zaidi maana ya ukombozi. Rej. KKK 571-573.

Ijumaa Kuu: Mateso na kifo cha Kristo Msalabani.
Ijumaa Kuu: Mateso na kifo cha Kristo Msalabani.

Tarehe 8 Aprili 2023 JUMAMOSI KUU majira ya saa 1:30 Usiku kwa Saa za Ulaya, kutakuwa na “Kesha la Pasaka” kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican itakayo anza kwa kubariki “Moto wa Pasaka” na kufuatiwa na maandamano kuingia kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na baadaye itaimbwa “Mbiu ya Pasaka” inayosimulia “Sifa ya Mshumaa wa Pasaka”, kielelezo cha Kristo Mfufuka. Kutakuwa na Ibada ya Neno la Mungu, Liturujia ya Ubatizo na hatimaye, Liturujia ya Ekaristi Takatifu.

Mkesha wa Pasaka ni Mama wa Mikesha Yote ya Kanisa: Fumbo la Wokovu.
Mkesha wa Pasaka ni Mama wa Mikesha Yote ya Kanisa: Fumbo la Wokovu.

DOMINIKA YA PASAKA YA BWANA tarehe 9 Aprili 2023 saa 4:00 asubuhi majira ya saa za Ulaya, Sawa na Saa 5: 00 za Asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki, kutakuwa na Ibada ya Misa Takatifu na baadaye baraka za kitume kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake kama zinavyojulikana kwa lugha ya Kilatini kama: “Urbi et Orbi.” Uwepo na ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Juma Kuu kwa Mwaka 2023 unategemea kwa kiasi kikubwa na hali yake ya afya sanjari na ushauri wa madaktari. Itakumbukwa kwamba, ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo Yesu ambayo waamini wa Kanisa la Mwanzo uliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; wakauendeleza kama msingi wa Mapokeo ya Kanisa na kuuthibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya, wakauhubiri na kuushuhudia kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka sanjari na Fumbo la Msalaba: Kristo amefufuka kwa wafu. Kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti; wafu wamepata uzima. Rej. KKK 636-658.

Juma Kuu
30 March 2023, 16:37