Ni majeraha makubwa yanayowasonga Watoto walionyanyaswa kijinsia. Ni majeraha makubwa yanayowasonga Watoto walionyanyaswa kijinsia.  (Copyright Marlon Lopez MMG1design. All rights reserved.)

Nyanyas,Papa Francis:watoto wawe salama zaidi katika Kanisa

Ujumbe wa Papa kwa washiriki wa Kongamano la II la Amerika ya Kusini kuhusu mada "Tunza,habarisha na uwasiliane:vipengele muhimu vya udhibiti bora wa kesi za unyanyasaji wa kijinsia",linaoendelea huko Asuncion,Paraguay:tendo lililofichwa na maaskofu na wakuu wa mashirika limeacha jeraha lisilofutika kwa watu wengi.

Angella Rwezaula, - Vatican.

Kongamano ambalo ni dhihirisho zaidi la nia ya Kanisa letu ya kutaka mabadiliko, ambapo unyanyasaji wa kijinsia na mapadre na kufichwa kwake na maaskofu na wakuu wa mashirika kumeacha jeraha lisilofutika kutokana na madhara yaliyofanywa kwa watu wengi.  Na pia ni kielelezo cha mchakato wa sinodi ya kukutana, kusikiliza, kutafakari na kusaidiana katika kujaribu kutekeleza na kupima dhamira yetu ya kuzuia unyanyasaji katika Kanisa letu. Ndivyo anavyoandika Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe alioutuma katika fursa ya Kongamano la II la Amerika ya Kusini juu ya kuzuia unyanyasaji, kwa kuongozwa na mada kuhusu “Kushughulikia, kuhabarisha na kuwasiliana: mambo muhimu katika usimamizi mzuri wa kesi za unyanyasaji wa kijinsia, linaloendelea huko Asuncion, Paraguay, tangu tarehe  14 hadi 16 Machi  2023.

Kuthibitisha utoshelevu wa hatua za kinga

Papa Francisko katika ujumbe huo  anasisitiza kwamba viongozi wa kanisa wamefanya mengi kukabiliana na uovu huo na kuzuia kutokea tena na kuhimiza ushirikiano kuhusu  matukio mengine kama mkutano huu, lakini, pia lazima “tuweze kuona matokeo ambayo watoto wako salama katika Kanisa letu”. Kwa sababu hiyo, anakumbusha jinsi alivyoomba Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto “kusimamia na kuthibitisha utoshelevu wa sera na matendo ya kutosha katika Kanisa zima na kuandaa Ripoti inayoonesha maboresho ambayo bado yanahitajika”.

Mitume wa kuzuia nyanyaso

Papa Francisko aidha amepongeza uzinduzi wa Kituo kipya cha Mafunzo juu ya Utu wa Binadamu na Kuzuia Unyanyasaji, ambacho kitakuwa kitovu cha kitaifa kinachojitolea kwa madhumuni haya na mitume wa kuzuia. Na kwa washiriki waliokusanyika katika siku hizi, kwa ajili ya  Kardinali Adalberto Martinez, Askofu mkuu wa Asuncion,  na kutoka nchi mbalimbali za Amerika ya Kusini na Ulaya amesema kwamba “kazi yenu ya ulinzi wa walio hatarini zaidi ni ya dharura na muhimu”.

Juhudi za kukuza hatua za ulinzi

Katika ujumbe wake, Papa anasisitiza umuhimu wa hatua mbele katika kazi hii ya ulinzi katika ngazi ya Makanisa mahalia. Kazi ya kuweka taratibu za wazi za ulinzi wa watu walio katika mazingira magumu katika Kanisa lazima iwe sehemu muhimu ya kazi na kipaumbele katika kila Kanisa la mahali, kwa msaada wa Curia Romana. Papa anakumbuka kuwa aliomba Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto kusimamia utekelezaji sahihi wa motu proprio Vos estis lux mundi, (pamoja na kanuni za kitaratibu za kupinga unyanyasaji wa kijinsia katika Kanisa, iliyochapishwa  mnamo Mei 2019), ili watu walionyanyasika hasa  wanawake wawe na njia wazi na zinazoweza kupatikana za kutafuta haki. Makanisa yale ya mahalia ambayo juhudi za kukuza hatua za kutosha za kuzuia bado ziko katika hatua za awali kwa sababu ya ukosefu wa rasilimali, zinahitaji umakini maalum. Kwa hakika, kulingana na Papa, kutokuwa na usawa katili unaoathiri jamii zetu lazima pia kuathiri Kanisa letu.

Ni kazi chungu lakini ni ya lazima

Hatimaye,  Baba  Mtakatifu Francisko katika ujumbe huo  anakumbuka mkutano wa miaka minne iliyopita, wa mnamo Februari mjini Vatican  wa maaskofu na wakuu wa mashirika ya kitawa  kutoka duniani kote pamoja na wajumbe wa  Curia Romana kushughulikia tatizo linaloonekana la usimamizi mbaya wa unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto na uongozi wa kanisa. Kwa hiyo Papa amesema kwamba  mtu yeyote ambaye anapunguza matokeo ya historia hii  au kupunguza hatari ya sasa kuwavunjia heshima wale ambao wameteseka sana  ni kuwahadaa wale wanaodai kuwahudumia. Unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa na mtu yeyote ndani ya Kanisa, popote ulipotokea ni hatari ya wazi na iliyopo kwa ustawi wa watu wa Mungu na upotovu wake utaendelea kudhalilisha Injili ya Bwana machoni pa watu wote. Na amekabidhi kwa maombezi ya Mama Yetu wa Kupalizwa, mlinzi wa Paraguay, juhudi za wale wote wanaojishughulisha na kazi hiyo  ya lazima lakini chungu ya huduma ya Kanisa.

15 March 2023, 10:32