Papa Francisko: Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Maji 2023: Maji Chemchemi ya Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Uhaba wa maji safi na salama unaweza kuwa ni chanzo cha migogoro, kinzani na vita kwa siku za usoni, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitasimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza vyanzo vya maji pamoja na kutambua kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Kumbe, huduma bora za maji safi na salama ni kichocheo kikuu cha maisha na afya bora zaidi. Dhana ya maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu ni agenda iliyoibuliwa hivi karibuni, lakini inaendelea kushika kasi kubwa sana katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na unyeti wake unaofungamanishwa na maisha ya binadamu. Ndiyo maana kuna haja ya kuwa na miundo mbinu ya kisheria, kiufundi, kijamii na kisiasa ili kuanzisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa utunzaji bora wa vyanzo vya maji. Kwa njia hii, amani duniani inaweza kuimarishwa kwa kuzuia vita, kinzani na migogoro inayoweza kufumbatwa katika mafao ya kisiasa na kiuchumi kwa kubeza: haki msingi, utu, heshima na maisha ya binadamu. Ikumbukwe kwamba, bila maji, hakuna maendeleo, na bila maendeleo fungani ni vigumu sana kupambana na umaskini duniani. Baba Mtakatifu Francisko anasema maji safi na salama ni amana na utajiri mkubwa unaopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa. Maji ni muhimu sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maendeleo fungamani ya binadamu kwa siku za mbeleni yatategemea kwa kiasi kikubwa jinsi ambavyo Jumuiya ya Kimataifa itaweza kuyatunza na kuyatumia maji kwa ajili ya: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Afya bora, maji safi na salama pamoja na mazingira bora ni mahitaji msingi ya binadamu, lakini pia yana umuhimu wake kwa viumbe wote wanaoishi duniani. Kumbe, kuna umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na maboresho makubwa yatakayowawezesha walimwengu kufaidika na haki hii msingi katika maisha yao. Huduma ya afya bora, maji safi na salama ni wajibu wa Serikali husika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwani huu ni wajibu wa watu wote, ili kusaidia mchakato wa kijamii na maendeleo fungamani ya binadamu. Kumbe, maji safi na salama hayawezi kugeuzwa kuwa sawa na bidhaa nyingine yoyote kwa sababu ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, uratibu wa maji unaunganishwa na wajibu wa kijamii kwa kuwa na mwelekeo sahihi wa kiikolojia sanjari na ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu miongoni mwa nchi mbalimbali duniani. Kwa njia hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kufanikiwa kuwa na matumizi bora zaidi ya maji safi na salama pamoja na kudumisha utunzaji bora zaidi wa vyanzo vya maji. Baba Mtakatifu Francisko anasema, changamoto mbalimbali zinazomwandamana mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, zinahitaji umoja, ushirikiano na mshikamano, kwa kuendelea kutafuta njia bora na rafiki zitakazomsaidia mwanadamu kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuka katika uso wa dunia. Ni katika muktadha huu wa maadhimisho wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Maji kwa Mwaka 2023 ambao umefunguliwa rasmi tarehe 22 Machi, Siku ya Maji Duniani kwa Mwaka 2023 huko New York, Marekani, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua waandaaji na washiriki wa mkutano huo, akikazia maji kuwa ni chemchemi ya matumaini katika kukabiliana na changamoto mamboleo sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.
Huu ni mkutano unaowashirikisha wadau wa maji duniani, ili kuunda Jukwaa Jipya la kuunganisha takwimu na habari zinazohusiana na maji, ili kuendeleza usimamizi endelevu na angavu wa maji duniani sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Pamoja na mambo mengine, mkutano huu unajadili kuhusu: Maji kwa ajili ya hali ya hewa, Ustahimilifu na mazingira. Chanzo cha Bahari, Bioanuwai, Hali ha hewa, Ustahimilivu wa kupunguza hatari za maafa duniani, kwa kuongeza thamani ya ardhioevu kama suluhu asilia katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kichocheo kikubwa cha maendeleo fungamani ya binadamu, licha ya tofauti zao msingi. Hii ni haki ambayo tangu mwaka 2010, Umoja wa Mataifa umeendelea kuifanyia kazi kwa tafiti za kisayansi na elimu makini; kwa kukazia kanuni maadili na utu wema katika matumizi ya rasilimali maji. Ni katika mazingira haya, Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa hakika huu ni mkutano wenye kuleta matumaini makubwa katika kukabiliana na changamoto, matatizo na fursa zinazojitokeza mintarafu maji safi na salama. Maamuzi yatakayofikiwa yatekelezwe kwa dhati kabisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jukwaa la Maji Duniani, liwe ni fursa ya kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya wadau mbalimbali kutoka katika sekta ya maji duniani. Huu ni wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuunganisha nguvu na kufanya kazi kwa kushirikiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, washiriki wa mkutano huu, wataweza kuibua suluhu ya changamoto za maji safi na salama, ili kuhakikisha kwamba, kweli maji safi na salama inakuwa ni sehemu haki msingi za binadamu na matumaini kwa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Maji kwa ajili ya afya: Upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na usafi wa mazingira. Maji kwa maendeleo fungamani ya binadamu; umuhimu wa kuthamini maji, mkakati wa maji-nishani-chakula na maendeleo ya kiuchumi na ukuaji wa miji duniani. Maji kwa ajili ya mabadiliko ya tabianchi, mnepo na mazingira; Chanzo cha Bahari, Bayoanuwai; hali ya hewa, mnepo sanjari na kupunguza hatari za maafa. Mashi kwa ushirikiano, huu ni ushirikiano unaovuka mipaka; ushirikiabo mtambuka wa kisekta na maji katika Ajenda ya Mwaka 2030. Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) lilianzishwa kunako mwaka 1972. Hii ni mamlaka ya kimataifa inayoweka ajenda ya mazingira, inawezesha utekelezaji wa vipengele vya mazingira vya maendeleo endelevu kwenye mfumo wa Umoja wa Mataifa, na hufanya kazi kama mtetezi na msimamizi mkuu wa mazingira duniani. Dhima ya UNEP ni kutoa mwongozo na kuwezesha ushirikiano wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa kuhimiza, kuelimisha na kuwezesha Jumuiya ya Kimataifa na watu katika ujumla wao kuimarisha maisha yao bila kuathiri yale ya vizazi vijavyo. UNEP inafanya kazi ilikuleta mabadiliko chanya kwa watu na mazingira kwa kuangazia chanzo cha changamoto tatu duniani za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira na uharibifu wa bayoanuai, na uchafuzi na taka. UNEP inatumia programu ndogo saba zilizoingiliana kuchukua hatua: Kushughulikia Mazingira, Kushughulikia Kemikali na Uchafuzi, Kushughulikia Asili, Sera ya Sayansi, Kusimamia Mazingira, Mabadiliko ya Kifedha na Kiuchumi na Mabadiliko ya Kidigitali.