Vatican: Ndoa za Mashoga Na Wasagaji Ni dhambi Hakuna Baraka ya Kanisa Katoliki
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kardinali Luis Francisco Ladaria Ferrer, S.J., Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Askofu mkuu Giacomo Morandi, Katibu mkuu wa Baraza kunako tarehe 15 Machi 2021 walitoa angalisho kuhusu wasiwasi juu ya kubariki “ndoa” ya watu wa jinsia moja kwa kusema ni marufuku kubariki “ndoa ya watu wa jinsia moja” kwa sababu si mamlaka ya Kanisa. Na hapa hakuna ubaguzi wala maamuzi mbele kuhusiana na mielekeo ya watu hawa kijinsia. Hili ni jibu makini la wasiwasi kuhusu uwezekano wa Kanisa kubariki “ndoa ya watu wa jinsia moja” “Responsum ad dubium.” Ni katika muktadha huu, Mapadre au wahudumu wa Sakramenti ya Ndoa, hawana ruhusa ya kubariki “ndoa” ya watu wa jinsia moja wanaotaka mahusiano yao yaweze kutambuliwa rasmi na Kanisa Katoliki. Baba Mtakatifu Francisko aliridhia angalisho hili na kutaka lichapwe na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume: “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, kifungu cha 250 anasema: “Kanisa linaiga kwa dhati kabisa msimamo wa Bwana Yesu, ambaye kwa upendo usio na mipaka amejitoa afe kwa ajili ya kila mtu bila ubaguzi. [275] Pamoja na Mababa wa Sinodi niliangalia hali za familia ambapo ndani yake wapo watu wenye mwelekeo wa ushoga, hali ambayo ni ngumu kwa upande wa wazazi na wa watoto pia. Tungependa kwa mara nyingine tena kusisitiza kuwa, pasipo kujali mwelekeo wake wa kijinsia, kila mtu anastahili kupewa heshima kwa utu wake na anastahili kupokelewa kwa heshima na hivi “kila hali ya ubaguzi usio haki” [276] iepukwe, na hasa kila aina ya mashambulizi na ukatili. Familia za namna hii lazima zipewe kwa heshima huduma za kichungaji, ili wale wenye mwelekeo wa mapenzi ya jinsia moja wapate msaada wanaouhitaji ili katika maisha yao wayatambue na kuyatekeleza kikamilifu mapenzi ya Mungu. [277]”
Ikumbukwe kwamba, baraka ni sehemu ya Sakramenti ya Ndoa na ni tendo la Liturujia ya Kanisa kwa ajili ya kumtukuza Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. “Ndoa” ya watu wa jinsia moja ni kinyume cha mpango wa Mungu uliofunuliwa katika kazi ya uumbaji. Ndoa kimsingi inaundwa kwa ukubaliano kati ya bwana na bibi. Umoja, kutovunjika na uwazi kwa uzazi ni hali ya lazima ya ndoa. Tofauti na uelewa huu kuhusu Sakramenti ya Ndoa ni kwenda kinyume cha kanuni maadili na mafundisho ya Kanisa. Kumbe, baraka ya Kanisa inatolewa tu kwa bibi na bwana wanaofunga ndoa kadiri ya mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, katika maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 10 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki tarehe 13 Machi 2013, aliwaambia waandishi wa habari kwamba, maamuzi yaliyofikiwa na Sinodi ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani ya kuanza kubariki “Ndoa za watu wa jinsia moja, kuanzia mwezi Machi 2026” ni batili na kwamba, yanakwenda kinyume cha kanuni maadili, utu wema, nidhamu na mafundisho tanzu ya Kanisa.
Ndoa za watu wa jinsia moja ni dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu. Sinodi ya Maaskofu Katoliki wa Ujerumani tangu mwanzo wake, imekuwa na utata, lakini ilikuwa na washiriki 176. Ni Sinodi ambayo imeendelea kugubikwa na utata, kwani imepitisha pia maamuzi ya kuanza kutoa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa wanandoa waliotengana, waliotalakiana na hatimaye kuamua kuoa au kuolewa tena. Ni katika hali na mazingira kama haya, Baba Mtakatifu Francisko alikwisha kutoa angalisho kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani kuhusu mwelekeo na msimamo tenge wa maamuzi yao mintarafu: nidhamu ya useja kwa mapadre, upadrisho wa wanawake na baraka ya ndoa kwa watu wa jinsia moja. Lakini, yote haya hayakupewa uzito unaostahili na kwamba, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Ujerumani hayakupata baraka zake za kitume kwani yaliendeshwa zaidi kiitikadi na kupokwa na “wajanja wachache.” Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anapenda kukazia mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, diplomasia ya upendo na huruma ya Mungu; haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi; majadiliano katika ukweli na uwazi.