Alhamisi Kuu, Karamu ya Mwisho: Injili ya Huduma Katika Udugu na Upendo wa Kibinadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ekaristi Takatifu ni sadaka ya Mwili na Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni karamu ya Bwana, kusanyiko la Kiekaristi, Ukumbusho wa mateso, kifo na ufufuko wa Bwana na Sadaka Takatifu ya Misa. Ekaristi Takatifu ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo na ni karamu ya Pasaka inayowakusanya waamini ili kusikiliza Neno la Mungu na kuumega mkate, kumbe hili ni kusanyiko la Kiekaristi, Liturujia Takatifu, Sakramenti Takatifu sana ya Altare na Komunyo Takatifu. Ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo waamini humpokea Kristo Yesu na roho zao hujazwa neema na kupewa amana ya uzima wa milele, tayari kushiriki ujenzi wa Kanisa la Kisinodi (Rej. KKK 1322–1323, 1409). Ekaristi ni kitovu na kilele cha maisha ya Kanisa, kwa kuwa kwayo Kristo anachagamana na Kanisa lake na waamini wake wote na sadaka ya sifa na shukrani iliyotolewa mara moja Msalabani kwa Mungu Baba. Kwa sadaka hii anamimina neema za wokovu kwa mwili wake ambao ni Kanisa (Rej. KKK 1407). Papa Leo XIII anasema; “Ekaristi Takatifu ni roho ya Kanisa” (Denz.3364). Ni Sakramenti ya umoja na upendo. Kimsingi, Ekaristi ni kiini kamili katika Kanisa, na Kanisa haliwezi kitu pasipo hiyo, kwa sababu ni Kristo Yesu mwenyewe anayejitoa kweli kama sadaka kwa ajili ya Kanisa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na ni katika Ekaristi Takatifu Kanisa hufikia uhalisia wake wa juu wa asili yake, yaani, kuwa linaonekana, la daima, na alama wazi ya neema ya wokovu ya Mungu iliyopo duniani kupitia kwa Kristo Yesu. Ekaristi ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo.
Katika maadhimisho ya Alhamisi Kuu, Karamu ya Mwisho, Mama Kanisa anafundisha kwamba, Kristo Yesu aliwapenda watu wake upeo na alipokuwa anakaribia “Saa yake” ili kutoka hapa ulimwenguni na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, Siku ile ya Alhamisi kuu, walipokuwa wakila, aliwaosha Mitume wake miguu yao na kuwapatia Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma ya upendo, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 6 Aprili 2023 ameadhimisha Karamu ya Mwisho kwenye Gereza la Watoto watukutu la "Casal del Marmo" lililoko mjini Roma na kuwaosha miguu vijana 12. Lengo ni kuragibisha utu, heshima na haki msingi za wafungwa magerezani, ili serikali na taasisi zinazohusika zijielekeze zaidi katika mchakato wa maboresho ya maisha ya wafunga na magereza yenyewe. Ibada ya kuwaosha vijana hawa miguu ni kielelezo cha unyenyekevu wa kibinadamu, ushuhuda wa upendo na ujirani mwema kwa kuwakumbusha watu wateule wa Mungu kwamba, wote ni ndugu wamoja, hata katika shida na mahangaiko ya ndani. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha waamini waliohudhuria Ibada hii ya Misa Takatifu gerezani hapo kwamba, kitendo cha kuwaosha watu miguu ni kazi iliyofanywa na watumwa enzi za Yesu!
Kwa Kristo Yesu, huu ulikuwa ni ushuhuda wa Injili ya huduma inayomwilishwa katika unyenyekevu pasi na makuu na kwamba, Ijumaa kuu, angeyamimina maisha yake kama “Mtumwa” kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, angekufa kifo cha aibu kwa kutundikwa Msalabani. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna watu wanapenda kujinufaisha kwa shida za jirani zao, changamoto kwa watu wateule wa Mungu ni kujenga mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu ili kusaidiana kwa hali na mali, hatimaye, dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Kristo Yesu anawapenda waja wake, kiasi cha kuwaosha miguu yao, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huduma ya upendo. Baba Mtakatifu anasema, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, lakini kuna watu ambao wananyonywa na kunyanyasika kwa kulipwa ujira “kiduchu” na kwamba, kuna umati mkubwa wa watu ambao hawana fursa za ajira, kiasi kwamba, watu kama hawa hawawezi kumudu gharama ya maisha hata kwa mambo msingi, hali inayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho ambalo linafikia utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa wafu, Kristo Yesu amekuja kuwaomboa binadamu na kuwatangazia Injili ya huruma na mapendo yanayomwilishwa kwa namna ya pekee kwa maskini na wale wote wanaosukummizwa pembezoni mwa jamii.
Baba Mtakatifu anasema, tendo la kuoshwa miguu iwe ni changamoto kwa watu wa Mungu kukumbuka kwamba, Kristo Yesu amewaosha miguu na wao wanapaswa kuhudumiana kama utambulisho na ushuhuda wa Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma. Mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu, Karamu ya Mwisho, Baba Mtakatifu amezindua Kikanisa cha Gereza la Watoto Watukutu, kilichojengwa kwa heshima ya Mwenyeheri Pino Puglisi, aliyejisadaka kwa ajili ya huduma kwa watoto na vijana katika maisha yake. Uongozi wa Gereza la Watoto watukutu la "Casal del Marmo" umempongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya ushuhuda wa Injili ya upendo na huruma inayobubujika kutoka katika sakafu ya moyo, utume na maisha yake. Huu ni ushuhuda unaowatia shime ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu licha ya magumu na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika huduma kwa wafunga gerezani. Mambo msingi ambayo wanaendelea kujifunza kutoka kwa Baba Mtakatifu ni huduma inayomwilishwa katika upendo, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Jumuiya hii imeahidi kwamba, itaendelea kumsindikiza Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na wataendelea pia kusali kwa ajili ya amani, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia.
Na habari kutoka Jimbo Katoliki la Kigoma, Tanzania zinasema kwamba, kama sehemu ya Maadhimisho ya Juma kuu, Askofu Joseph Roman Mlola ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Kigoma, akiwa amesindikizana na waamini wa Kanisa kuu, Parokia ya Bikira Maria Mshindi, Jimbo Katoliki Kigoma, wamekwenda kuwatembelea na kuwafariji wafungwa wanaotumikia adhabu zao katika Gereza la Bangwe, Kigoma. Wametoa msaada wa vifaa mbalimbali yakiwemo magodoro na mablanketi, kama sehemu ya ushiriki wao katika maboresho ya maisha ya wafungwa magerezani, wito na changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, Parokia ya Mtakatifu Augustino, Salasala, Jimbo kuu la Dar es Salaam nayo imewatembelea na kuwafariji wafungwa katika Gereza la Segerea, kielelezo cha Injili ya upendo unaomwilishwa katika ushuhuda wa imani tendaji.