Mfuko wa Papa: “Papal Foundation” ni Shirika pekee la hisani kutoka nchini Marekani ambalo limejizatiti kwa ajili ya kusaidia juhudi za Khalifa wa Mtakatifu Petro  kugharimia miradi ya maendeleo. Mfuko wa Papa: “Papal Foundation” ni Shirika pekee la hisani kutoka nchini Marekani ambalo limejizatiti kwa ajili ya kusaidia juhudi za Khalifa wa Mtakatifu Petro kugharimia miradi ya maendeleo.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Huduma ya Kanisa Kwa Watu wa Mungu: Umoja, Ukweli na Uwazi

Dhamana na utume huu, umekuwa ukirithishwa na kuchangiwa na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro anatekeleza vyema dhamana na wajibu wake barabara. Mfuko huu wa Papa una mchango na nafasi yake maalum katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amekazia mambo makuu mawili; uwajibikaji wa ujenzi wa umoja; ukweli na uwazi katika huduma inayotolewa na Mama Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa Papa: “Papal Foundation” ni Shirika pekee la hisani kutoka nchini Marekani ambalo limejizatiti kwa ajili ya kusaidia juhudi za Khalifa wa Mtakatifu Petro kugharimia mahitaji ya Kanisa la Kristo! Mfuko huu ulianzishwa kunako mwaka 1988 na tangu wakati huo, zaidi ya dola za Kimarekani milioni 200 zimetolewa kama msaada au ruzuku pamoja na kugharimia miradi 2, 000 chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko, Benedikto XVI pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II. Fedha hii imetumika kwa ajili ya kugharimia ujenzi wa Makanisa 358; ufadhili wa masomo, malezi na majiundo kwa Majandokasisi 170; Ujenzi wa nyumba za Mapadre, Konventi za watawa na Monasteri 404. Mfuko pia umegharimia ujenzi wa Shule 273 pamoja na Hospitali 104. Huu ni ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 21 Aprili 2023 amekutana na wajumbe wa Mfuko wa Papa waliofika mjini Vatican kumtembelea pamoja na kuwakilisha mchango wao kwa ajili ya shughuli za maendeleo zinazosimamiwa na kuendeshwa na Papa Francisko kwa sasa. Kwa hakika, amewapongeza kwa kutembelea Makao ya Khalifa wa Mtakatifu Petro aliyekabidhiwa Siku ile ya Alhamisi Kuu, kuwaimarisha ndugu zake na hivyo kuwa ni chombo cha umoja na mshikamano wa Kanisa. Dhamana na utume huu, umekuwa ukirithishwa na kuchangiwa na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro anatekeleza vyema dhamana na wajibu wake barabara. Mfuko huu wa Papa una mchango na nafasi yake maalum katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amekazia mambo makuu mawili; uwajibikaji wa ujenzi wa umoja; ukweli na uwazi katika huduma inayotolewa na Mama Kanisa.

Mfvuko wa Papa: Umoja, ukweli na uwazi
Mfvuko wa Papa: Umoja, ukweli na uwazi

Mfuko wa Papa umekuwa na ushiriki mkubwa katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwanza kabisa ni kwa ajili ya kujenga na kuimarisha umoja, ambao umejeruhiwa kutokana na migawanyiko ya kisiasa pamoja na tabia ya kutaka kujimwambafai hata katika masuala ya imani. Huu ndio mpasuko na migawanyiko anayozungumzia Mtakatifu Paulo akisema, kuna watu wanaojidai wakisema kwamba, wao ni “Wa Apolo, au wa Paulo” na kusahau kwamba, wao ni wafanyakazi tu pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu. Rej. 1Kor 3:1-9 na Rum 16: 17-18. Baba Mtakatifu anawashukuru wajumbe wa Mfuko wa Papa kwa kuvuka migawanyiko na mipasuko hii na hivyo kunogesha mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa kwa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu. Baba Mtakatifu amewatia shime wajumbe hawa kuhakikisha kwamba, wanasaidia kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa la Kiulimwengu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa katika miaka ya hivi karibuni limeendelea kujizatiti kutoa huduma ya upendo kwa kukazia misingi ya ukweli na uwazi, kwa kutambua kwamba, fedha hii ni kielelezo cha ukarimu wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Kashfa ya wizi, ubadhilifu na matumzi mabaya ya mali ya Kanisa, kimsingi unachafua: jina, maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu amewapongeza wajumbe wa Mfuko huu kwa kuendelea kujikita katika misingi ya ukweli na uwazi katika kugharimia majiundo ya Mapadre pamoja na ujenzi wa miradi inayogharimiwa na Mfuko wa Papa, unaochangia kimsingi katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wajumbe hawa kwa kumsaidia kutekeleza utume wake wa upendo kwa ajili ya Kanisa zima.

Mfuko wa Papa 2023

 

22 April 2023, 14:30