Tafuta

Mwenyeheri Armida Barelli ni kati ya wanawake wa “shoka” ambaye kunako mwaka 1909 alijiweka wakfu mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwenyeheri Armida Barelli ni kati ya wanawake wa “shoka” ambaye kunako mwaka 1909 alijiweka wakfu mbele ya Mwenyezi Mungu.   (ANSA)

Mwenyeheri Armida Barelli: Uzazi na Malezi; Maisha na Utume wa Kuyatakatifuza Malimwengu

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa mahujaji amekazia dhamana ya mwanamke katika uzazi na malezi; mfano bora wa uongozi ndani ya Kanisa na katika jamii; mtume mwaminifu aliyejiweka wakfu kwa ajili ya Mungu, akabahatika kusoma alama za nyakati ili kukabiliana na changamoto za: malezi, elimu na makuzi ya vijana wa kizazi kipya. Leo hii kuna mambo ambayo yanakwenda kinyume chake na yana madhara makubwa katika maisha ya kifamilia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mahujaji kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Milano, Italia, Jumamosi tarehe 22 Aprili 2023 wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Mtumishi wa Mungu Armida Barelli kutangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 30 Aprili 2022 kwenye Kanisa kuu la “Santa Maria Nascente” lililoko Jimbo kuu la Milano, nchini Italia. Mwenyeheri Armida Barelli ni kati ya wanawake wa “shoka” ambaye kunako mwaka 1909 alijiweka wakfu mbele ya Mwenyezi Mungu. Mwaka 1918 akapewa dhamana ya kuanzisha Tawi la Wasichana Wakatoliki nchini Italia. Kunako mwaka 1919, watu watano mashuhuri akina Padre Agostino Gemelli, Ludovico Necchi, Francesco Olgiati, Armida Barelli pamoja na Ernesto Lombardo walianzisha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” “L'Università Cattolica del Sacro Cuore (UCSC) Jimbo kuu la Milano. Chuo hiki kilianza kufanya shughuli zake hapo tarehe 7 Desemba 1921 ili kujibu hitaji la mahali pa malezi na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya nchini Italia, changamoto iliyovaliwa njuga na matokeo yake Chuo hiki kimeendelea kukua na kupanuka na hatimaye, kuwa ni jukwaa la malezi na majiundo ya kielimu kitaifa na kimataifa. Mwenyeheri Armida Barelli anaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka tarehe 19 Novemba. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa mahujaji amekazia dhamana ya mwanamke katika uzazi na malezi; mfano bora wa uongozi ndani ya Kanisa na katika jamii; mtume mwaminifu aliyejiweka wakfu kwa ajili ya Mungu, akabahatika kusoma alama za nyakati ili kukabiliana na changamoto za: malezi, elimu na makuzi ya vijana wa kizazi kipya.

Mwenyeheri Armida Barelli alitatangazwa kuwa mwenyekeri 30 Aprili 2022
Mwenyeheri Armida Barelli alitatangazwa kuwa mwenyekeri 30 Aprili 2022

Baba Mtakatifu anasema, mwanamke ni mzazi na mlezi, utume alioutekeleza Mwenyeheri Armida Barelli katika maisha na utume wake kama inavyoshuhudiwa katika nyaraka mbalimbali. Kwa bahati mbaya, leo hii, mambo yanayonekana kwenda kinyume chake, kwani kuna madhara makubwa katika maisha ya familia na katika jamii kutokana na ubaguzi na itikadi kali ambazo hazitoi nafasi ya majadiliano na matokeo yake ni kudhalilishana. Mwenyeheri Armida Barelli ni mfano bora wa kuigwa katika kujenga mahusiano na mafungamano na wanawaume; kwa kukazia utamaduni wa kusikilizana na hivyo kujenga mtandao katika maisha ya kijaamii na maeneo ya kazi. Maadhimisho Siku ya 99 ya Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” Dominika tarehe 23 Aprili 2023 yananogeshwa na kauli mbiu: “Kwa ajili ya upendo kwa ujuzi. Changamoto za ubinadamu mpya.” Huu ni mwaliko wa kuunda dhamiri nyofu, kukuza na kudumisha demokrasia; elimu na majiundo ya kitaaluma yanayosimikwa katika tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Mwenyeheri Armida Barelli alikuwa ni mtume mwaminifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Alikuwa ni mnyenyekevu, mwenye kipaji cha ugunduzi na aliyejitahidi katika maisha yake, akitaka kubaki daima akiwa ameaandamana na Kikristo Yesu, ili hatimaye, mang’amuzi haya ya maisha aweze kuwashirikisha watu wengine upendo wenye kuokoa, Neno lake na nguvu yake na kwamba, mapungufu yake haikupaswa kuwa ni kisingizio, kinyume chake, kimekuwa ni kichocheo cha kukua na kukomaa zaidi na zaidi. Rej. Evangelii gaudium, 121.

Mwenyeri Armida  Barelli mtambuzi mkuu wa elimu kwa vijana
Mwenyeri Armida Barelli mtambuzi mkuu wa elimu kwa vijana

Hii ni changamoto ya kulinda na kudumisha Injili ya uhai, kwa kujikita katika udugu wa kibinadamu; kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza na kuzungumza na wote, ili hatimaye, kushikamana na kutembea na watu wote katika medani mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa. Mwenyeheri Armida Barelli alijiweka wakfu kuwa mmisionari wa Ufalme wa Kristo Yesu. Huu ni wito wenye masharti magumu. Ilikuwa ni Papa Pio XII kwa Waraka wake wa Kitume wa “Provida Mater Ecclesia” aliyepitisha Mashirika ya kitawa yenye mwelekeo wa Kisekulari na hivyo kuleta magauzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa, alama wazi ya kinabii na ujasiri wa kumtumikia na kumshuhudia Kristo Yesu kwa walimwengu, namna mpya ya waamini walei kuishi ndani ya Ulimwengu. Ni katika muktadha huu, mashuhuda wengi wa Injili wameibuka. Ni mtu aliyebahatika kusoma alama za nyakati, kwa kuwahusisha waamini wengi zaidi katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa linalosimikwa katika umoja, ushiriki na utume. Ni vyema Wakristo katika ulimwengu mamboleo wakatambulikana kwa uzazi na malezi yao na kwamba wao ni mitume na wamewekwa wakfu kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu. Hii ni amana na utajiri wa Kanisa zima.

Mwenyeheri Armida Barelli anaadhimishwa 19 Novemba
Mwenyeheri Armida Barelli anaadhimishwa 19 Novemba

Kwa upande wake, Askofu mkuu Mario Delpini wa Jimbo kuu la Milano ameongoza Ibada ya Misa Takatifu na mahubiri yake kujikita kwa Roho Mtakatifu, ili kuvunjilia mbali minyororo ya utumwa wa Shetani, Ibilisi kama vile manung’uniko kama yalivyojitokeza kati ya Wayahudi na Wayunani, kiasi cha Mitume kuamua kuwachagua Mashemasi saba miongoni mwao. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Mwenyeheri Armida Barelli aliyejitahidi kusoma alama za nyakati na kufanya mang’amuzi kuhusu nyakati, wito na utume wake, kiasi cha kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili utume miongoni mwa wasichana sanjari na elimu makini kwa vijana hawa. Matunda ya Roho Mtakatifu yanaendelea kujionesha miongoni mwa vijana wanaosoma Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore.” Huu ni mwaliko pia wa kuvunjilia mbali woga na wasiwasi, kwani Kristo Yesu daima anatembea bega kwa bega na waja wake. Kumbe, waamini wajitahidi kufiri na kutenda pamoja na Kristo Yesu pamoja na kujiaminisha kwake kama kielelezo ushuhuda na tafiti za maisha kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Askofu mkuu Mario Delpini anawaombea ili Mwenyezi Mungu awajalie karama, ari na mwamko mpya wa kufiri na kutenda pamoja na Kanisa, katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mihimili ya Uinjilishaji wa kina ihamasishwe na kauli mbiu ya Maadhimisho Siku ya 99 ya Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” Dominika tarehe 23 Aprili 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Kwa ajili ya upendo kwa ujuzi. Changamoto za ubinadamu mpya.” Ni busara kukusanya ushuhuda wa Armida Barelli na waanzilishi wa Umoja wa Wasichana Italia kumkaribisha Yesu na kumruhusu Roho wa Mungu kushinda njama za Ibilisi, Shetani na hali ya kutoridhika, hofu na mashaka, bali utume uweze kusonga mbele.

Mwenyeri Armida Barelli mfano bora wa kuigwa
Mwenyeri Armida Barelli mfano bora wa kuigwa

Kwa upande wake Emmanuela Gitto katika salam zake kwa Baba Mtakatifu Francisko, kwa niaba ya watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia, kama kielelezo cha shukrani kwa Mama Kanisa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Armida Barelli kuwa Mwenyeheri, anasema, kwao ni ushuhuda wa utakatifu wa “mwanamke wa shoka” aliyejisadaka kwa ajili ya malezi, makuzi na majiundo ya wasichana wengi nchini Italia. Huu ni utakatifu unaopata chimbuko lake katika: Maisha ya sala na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu sanjari na mfano wa maisha ya Mtakatifu Francisko wa Assisi yaliyokuwa yanamwilishwa hatua kwa hatua katika maisha ya kila siku. Mwenyeheri Armida Barelli, ni mwanamke aliyelipenda Kanisa, akajiweka wakfu kwa ajili ya Mungu na jirani; akawa ni chombo na msaada mkubwa kwa viongozi wa Kanisa, changamoto kubwa iliyofanyiwa kazi na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, yaani umuhimu wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Hata leo hii, waamini wanaweza kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, kwa kuimba, kumpenda na kusali. Yote haya yafanyike kwa furaha ndani ya Kanisa pamoja na Kristo Yesu!

Mwenyeheri Barelli

 

22 April 2023, 14:54