Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 5 Aprili 2023 ameyaelekeza mawazo yake kwa waathirika wa vita, wale wote wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 5 Aprili 2023 ameyaelekeza mawazo yake kwa waathirika wa vita, wale wote wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Kuna Wanawake Ambao Wako chini ya Msalaba kutokana na Vita

Katika maadhimisho ya Juma Kuu ni kiini cha Mwaka wa Liturujia ya Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko ameyaelekeza mawazo yake kwa waathirika wa vita, wale wote wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine, bila kusahau sehemu nyingine za dunia. Hawa ni wanawake wanaoshuhudia watoto wao wakipoteza maisha vitani, wakirejeshwa majumbani wakiwa vilema na wale wanaopotea katika mazingira ya kutatanisha! Amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 5 Aprili 2023 amedadavua kuhusu: Mitume walivyokaza macho yao juu ya Msalaba, Askari walivyomvua mavazi na walipokwisha kumsulubisha, waligawana mavazi yake, wakipiga kura, Kristo Yesu Msulubiwa, Mwili wake Mtukufu uliotundikwa Msalabani unaonesha Madonda yake Matakatifu, chemchemi ya toba na wongofu wa ndani, ubaya unageuzwa kuwa ni chemchemi ya msamaha, huruma na upendo. Siku tatu kuu za Pasaka, iwe ni fursa ya kumkaribia zaidi Kristo Yesu katika mateso yake ambayo ni chemchemi ya matumaini. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Msalaba kwa Mitume wa Yesu, ulionekana kuwa ni hatima ya mambo yote, yaani kielelezo cha hali ya juu kabisa cha mateso, lakini Msalaba ukageuka kuwa ni chemchemi ya matumaini, huruma, upendo na msamaha. Msalaba ambao ulikuwa ni mti wa kifo, ukageuka kuwa ni mti wa uhai, chemchemi ya matumaini yanayoganga na kuponya magonjwa ya mwanadamu ambayo yanaendelea kulichafua na kulinajisi Kanisa la Kristo Yesu na Ulimwengu katika ujumla wake. Katika Kipindi hiki cha Siku Tatu Kuu za Pasaka, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele.

Kuna wanawake ambao wamebaki chini ya Msalaba kutokana vita
Kuna wanawake ambao wamebaki chini ya Msalaba kutokana vita

Alhamisi kuu, Kanisa linaadhimisha Kumbukumbu ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Ijumaa kuu, Mama Kanisa anakumbuka mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Jumamosi kuu, Kanisa katika majonzi makubwa, linasubiria ushindi wa Kristo Yesu Mfufuka! Maadhimisho ya Juma Kuu ni kiini cha Mwaka wa Liturujia ya Kanisa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko ameyaelekeza mawazo yake kwa waathirika wa vita, wale wote wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine, bila kusahau sehemu nyingine za dunia. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali na kuwaombea wale wote wanaochochea vita kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuanza mchakato wa haki, amani na maridhiano. Baba Mtakatifu anapomtafakari na kumwona Bikira Maria chini ya Msalaba, anawakumbuka na kuwaombea wazazi wa askari kutoka Urusi na Ukraine, wanaoendelea kupoteza maisha kutokana na vita. Hawa ni wanawake na akina mama wazazi ambao watoto wao wamepata ulemavu wa kudumu au wamepoteza maisha vitani.

Wanawake chini ya Msalaba
06 April 2023, 15:22