Tafuta

Kwa muda wa siku kumi na tano mfululizo, mvua kubwa imeendelea kunyeesha katika Mkoa wa Emilia Romagna, nchini Italia na hivyo kusababisha mafuriko makubwa pamoja na maporomoko ya udongo. Kwa muda wa siku kumi na tano mfululizo, mvua kubwa imeendelea kunyeesha katika Mkoa wa Emilia Romagna, nchini Italia na hivyo kusababisha mafuriko makubwa pamoja na maporomoko ya udongo.   (AFP or licensors)

Papa Francisko Asikitishwa na Maafa Makubwa Nchini Italia

Mvua kubwa imeendelea kunyeesha katika Mkoa wa Emilia Romagna, nchini Italia na hivyo kusababisha mafuriko makubwa pamoja na maporomoko ya udongo. Tayari watu kumi na nne wamekwisha fariki dunia, watu 320 wameokolewa na Kikosi cha Zimamoto, watu 27, 000 hawana nishati ya umeme na kwamba, jumla ya watu 10, 000 wameathirika kutokana na mafuriko haya. Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za rambirambi kutokana na maafa haya makubwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa muda wa siku kumi na tano mfululizo, mvua kubwa imeendelea kunyeesha katika Mkoa wa Emilia Romagna, nchini Italia na hivyo kusababisha mafuriko makubwa pamoja na maporomoko ya udongo. Tayari watu kumi na nne wamekwisha fariki dunia, watu 320 wameokolewa na Kikosi cha Zimamoto, watu 27, 000 hawana nishati ya umeme na kwamba, jumla ya watu 10, 000 wameathirika kutokana na mafuriko haya. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Edgar Peña Parra, Katibu mkuu Msaidizi wa Vatican, kwenda kwa Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, anasema, amesikitishwa sana na maafa makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa pamoja na maporomoko ya udongo mkoani Emilia Romagna.

Mvua kubwa imesababisha maafa nchini Italia
Mvua kubwa imesababisha maafa nchini Italia

Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wale wote walioguswa na kutikiswa na maafa haya. Anapenda kuwahakikishia sala kwa wale wote waliofariki dunia, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma aweze kuwarehemu na hatimaye, kuwakirimia maisha na uzima wa milele. Anapenda kuchukua fursa hii, kutoa rambirambi zake kwa ndugu, jamaa na marafiki wa wale wote waliofariki dunia. Anawaombea majeruhi, ili waweze kupona haraka na hatimaye, kurejea tena katika shughuli zao za kila siku. Baba Mtakatifu anapenda kuwafariji wale wote wanaoteseka kutokana na maafa haya, anawatia shime, ari na moyo mkuu, wale wote wanaoendelea kujisadaka usiku na mchana ili kuokoa maisha ya wananchi wa Mkoa wa Emilia Romagna. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha umoja na ushirika wake wa kidugu kwa watu wote wa Mungu walioathirika kwa mafuriko pamoja na maporomoko haya. Kardinali Pietro Parolin anapenda pia kuungana na Baba Mtakatifu kutuma salam zake za rambirambi kwa wote waliofariki dunia, anapenda kuwahakikishia sala zake. Maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na Cesena, Forli na Faenza, ambamo mafuriko makubwa yamesababisha nyumba nyingi kuzama. Tayari Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Italia, Caritas Italiana, limeanza kutoa huduma kwa waathirika wa mafuriko haya.

Maafa Italia
19 May 2023, 13:51