Kikosi cha Walinzi wa Papa: Askari Wapya 23 Wala Kiapo cha Utii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswisi, kilichoundwa kunako mwaka 1506 na Papa Giulio II, maarufu kama “Swiss Guards” kina dhamana na utume unaojikita katika wito, uaminifu, umakini na sadaka inayotekelezwa kwa moyo wa unyenyekevu pasi na makuu. Jumamosi tarehe 6 Mei 2023 Wanajeshi wa Kikosi cha Ulinzi wa Papa kutoka Uswisi, wamefanya kumbukizi ya askari 147 kutoka Uswisi walioyamimina maisha yao mjini Roma kwa ajili ya kumlinda na kumtetea Papa Clement VII kunako mwaka 1527. Katika tukio hili, askari wapya 23 kutoka sehemu mbalimbali za Uswisi wamekula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwashukuru kwa uwepo, dhamana na wajibu wao unaoshuhudia uaminifu wao kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, umuhimu wa kufanya kazi mjini Vatican kama ushuhuda wa imani tayari kupyaisha uzuri wa Mungu katika maisha yao sanjari na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kikosi cha Walinzi wa Papa kutoka Uswisi, ni familia kubwa, iliyo hai na inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, wakati wa kutekeleza dhamana na wajibu wake na hata wakati wa mapumziko binafsi. Hapa ni mahali pa kukua na kukomaa; mahali pa kujifunza maisha ya kiutu na Kikristo; huku wakishirikishana uzoefu na mang’amuzi ya maisha! Ni jambo la muhimu kwa wanajeshi wapya kuwa na ujasiri, ari na moyo mkuu wa kugundua mambo mapya!
Hii ni njia pia ya kujisadaka kwa ajili ya utume kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Vatican katika ujumla wake. Hii ni njia ya kuweza kuishi vyema Ubatizo wao, tayari kushuhudia ile furaha ya imani yao kwa Kristo Yesu. Hii ni imani inayopata chimbuko lake kutoka katika familia, ikarutubishwa Parokiani na hatimaye, kushuhudiwa kama kielelezo cha mafungamano ya Kanisa la Uswisi na Kanisa la Roma. Ushuhuda huu wa imani unapaswa kutolewa wakati wa huduma yao kwa Sekretarieti kuu ya Vatican, kwa mahujaji na wageni mbalimbali wanaofika mjini Vatican. Huu ni wakati muafaka wa kumwilisha Injili ya Kristo kwa kujifunza kutoka kwake, ili hatimaye, kuweza kuishi upendo wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anawataka wanajeshi wapya kutumia fursa hii kujifunza tunu msingi za Kiinjili, ili waweze kushirikisha furaha ya Kristo Mfufuka kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu, Maandishi ya maisha ya kiroho, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na ushiriki mkamilifu wa Sakramenti mbalimbali za Kanisa. Uzuri wa historia, majengo na sanaa mbalimbali ziwawezeshe kupyaisha uzuri wao kwa Mwenyezi Mungu na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Watambue kwamba, Kristo Yesu anatembea pamoja nao na yuko kati yao, wakati wa utulivu na amani na hata wakati wa shida na mahangaiko ya ndani, daima wajitahidi kuonja uwepo angavu wa Mungu, mwingi wa huruma na mapendo.
Baba Mtakatifu anawataka wanajeshi wapya kuwa jasiri, huku wakiendelea kuimarishwa na imani kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Wawe ni mashuhuda na mitume wa upyaisho wa maisha binafsi na yale ya kijumuiya, kama kielelezo cha utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka katika huduma na maisha ya kijumuiya. Watu wanataka kuona utakatifu wa maisha kutoka kwa wafanyakazi wa Vatican! Kambi ya Jeshi iwe ni mahali pa kujifunza kanuni maadili na tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kukuza na kudumisha majadiliano, ukweli wa maisha, mahusiano mema pamoja na kuelewana. Katika hali na mazingira kama haya, kutakuwepo na nyakati za furaha pamoja na nyakati za majonzi. Kipindi hiki, kiwe ni fursa ya kujenga urafiki mwema, kwa kuheshimu na kuthamini mawazo yanayotolewa na wengine; kwa kuendelea kujifunza kuona kwa mwingine yule ndugu na jirani ambaye ni mwadani wa safari ya pamoja. Tabia hii itawawezesha kuishi katika Jamii wakiwa na mwelekeo sahihi wa maisha, kwa kutambua tofauti za kitamaduni, kidini na kijamii kama amana na utajiri na wala si tishio la maisha.
Hii ni changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo kutokana na uwepo wa makundi makubwa ya watu wanaotafuta usalama na maisha bora zaidi. Mwishoni, mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewashukuru wanajeshi hawa wapya kwa sadaka na majitoleo yao na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Katika majiundo yao, wanajeshi wapya wanapata katekesi ya kina na endelevu kuhusu: uaminifu, maana ya sadaka na zawadi ya maisha; ulinzi na usalama; dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika Kanisa la Kristo. Hiki pia ni kipindi kinachowawezesha askari hawa kupata utajiri wa kitamaduni kwa kufanya hija katika maeneo muhimu ya kihistoria. Wanajeshi hawa wanajifunza kwa kina na mapana matendo ya huruma kiroho na kimwili, kwani ni sehemu ya vinasaba vya utume wao. Mara nyingi hawa ndio wanaomsindikiza mtunza sadaka mkuu wa Papa katika kuwasaidia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii katika mitaa ya Roma nyakati za usiku, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.