Tafuta

Kongamano la 6 la Kimataifa la Tenisi na Padel kwa Mwaka 2023, linafanyika kuanzia Jumamosi tarehe 6 na Jumapili tarehe 7 Mei 2023. Kongamano la 6 la Kimataifa la Tenisi na Padel kwa Mwaka 2023, linafanyika kuanzia Jumamosi tarehe 6 na Jumapili tarehe 7 Mei 2023.  (Vatican Media)

Kongamano la Sita la Tenisi na Padel: Michezo na Nguvu ya Kuelimisha Vijana

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Tenisi na Padel ni michezo na nguvu yake ya kuelimisha inabaki katika masuala ya michezo. Kumbe, watu waendelee kucheza kama sehemu ya burudani na kwamba, michezo ikigeuzwa kuwa ni sehemu ya mashindano itamezwa na ubinafsi na uchoyo na matokeo yake ni kuharibu michezo na hivyo kwenda kinyume cha maana ya michezo. Kuna haja ya kujifunza umuhimu wa kushambua na kujilinda; hekima na hatari zake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wachezaji wa Kimataifa wa Italia wamekwisha kuwasili kwenye viwanja vya “Foro Italico.” Lakini pia kuna matukio mengi yanayoendeshwa kando ambayo yatafanyika kwa muda wa siku kumi na nne zijazo. Kongamano la 6 la Kimataifa la Tenisi na Padel kwa Mwaka 2023, limeandaliwa na Taasisi ya 'Roberto Lombardi' Istituto Superiore di Formazione” linafanyika kuanzia Jumamosi tarehe 6 na Jumapili tarehe 7 Mei 2023. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 6 Mei 2023 amekutana na washiriki wa Kongamano la 6 la Kimataifa la Tenisi na Padel kwa Mwaka 2023 linalowashirikisha wakufunzi, watoto na vijana mintarafu mwelekeo wa elimu na mafunzo ya michezo, changamoto na mwaliko wa kujikita zaidi katika elimu na mafunzo ya michezo, katika kushambulia na kulinda; hatari na busara: Kuna mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika kujilinda na kushambulia; kielelezo muhimu katika masuala ya elimu na utu wa mtu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mkufunzi makini lazima atambue hatari za kumruhusu kijana kufanya mang’amuzi mapya ambayo yanaweza kumsaidia kukua na kukomaa; lakini pia awe na busara ya kusindikiza na kutenda kwa hekima na busara.

Michezo na nguvu yake ya kuelimisha
Michezo na nguvu yake ya kuelimisha

Kijana wakati wa michezo anapaswa kujisikia kuwa huru, lakini akilindwa na kamwe asijisikie kuwa ametelekezwa. Kwa wakufunzi, wazazi au walezi wanaowatafutia watoto wao majibu ya changamoto zote wanazokutana nazo hawamsaidii kukua na kukomaa na kwa hakika huu ni ukosefu wa busara na matokeo yake ni mchanganyiko wa woga na wasiwasi, uchoyo, ubinafsi na tabia ya kutaka kummiliki mtoto. Hii ni hatari kwa makuzi na malezi ya watoto. Mwelekeo chanya wa hekima unajielekeza katika kushambulia kwa kupima vyema hali halisi, kwa kuzingatia nguvu za kijana. Mkufunzi hana budi kuwanoa wachezaji wake kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu pasi na kukata tamaa.Tenisi na Padel ni michezo na nguvu yake ya kuelimisha inabaki katika masuala ya michezo. Kumbe, watu waendelee kucheza kama sehemu ya burudani na kwamba, michezo ikigeuzwa kuwa ni sehemu ya mashindano itamezwa na ubinafsi na uchoyo na matokeo yake ni kuharibu michezo na hivyo kwenda kinyume cha maana ya michezo. Kumbe, hii ni changamoto ya kuendelea kujifunza umuhimu wa kushambulia na kujilinda, hatari na hekima. Mwishoni mwa hotuba yake amewabariki wote waliohudhuria pamoja na familia zao.

Kongamano la Tenisi
06 May 2023, 14:20