Shirikisho hili ni kati ya Mashirikisho makubwa yanayounda Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Kimataifa. Shirikisho hili ni kati ya Mashirikisho makubwa yanayounda Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Kimataifa.  (Vatican Media)

Kumbukizi ya Miaka 70 ya Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Amerika ya Kusini, ODUCAL

Lengo kuu la ODUCAL ni kuchangia katika utengenezaji wa sera na mikakati mintarafu elimu Kitaifa na Kimataifa. Kwa Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean, umaskini na ukosefu wa usawa ni janga kubwa linaloendelea kupanuka siku kwa siku, likichagizwa na masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kiitikadi kiasi hata cha kutishia maendeleo na uhuru wa kweli. Shirikisho linaadhimisha kumbukizi ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake na Askofu mkuu Alfredo Santiago.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki vya Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean, ODUCAL, lilianzishwa na Askofu mkuu Alfredo Silva Santiago, miaka 70 iliyopita. Hili ni Shirikisho la Vyuo vikuu vya Kikatoliki vipatavyo 115, vikiwa na wanafunzi 1, 500, 000 wanaofundishwa na Majaalimu 110, 000 na vinatoa kozi zaidi ya 5000 katika ngazi mbalimbali. Shirikisho hili ni kati ya Mashirikisho makubwa yanayounda Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki Kimataifa, “The International Federation of Catholic Universities, FIUC.” Ni katika muktadha wa kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, tarehe 4 Mei 2023 wamekutana katika moyo wa ushirikiano na udugu, ili kujenga na kuimarisha mtandao wa kazi ya ushirikiano. Lengo kuu la ODUCAL ni kuchangia katika utengenezaji wa sera na mikakati mintarafu elimu Kitaifa na Kimataifa. Kwa Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean, umaskini na ukosefu wa usawa ni janga kubwa linaloendelea kupanuka siku kwa siku, likichagizwa na masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kiitikadi kiasi hata cha kutishia maendeleo na uhuru. Changamoto mamboleo ni muda muafaka wa kufanya tafakari ya kina kuhusu mifumo wa uchumi, ili kuvuka kampeni za kiitikadi, kihisia na kisiasa na ubaguzi wa kitamaduni, ili kung’amua kazi bora na zenye ubunifu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Dhamana ya Shirikisho hili ni kuchangia majiundo makini ya wanafunzi wakatoliki, ili waweze kuwa na mwelekeo mpana wa kuyaangalia mambo; Fumbo la Kristo Yesu na Ulimwengu katika ujumla wake na katika Fumbo la maisha ya binadamu kama wanavyokaza kusema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwamba, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Rej. LG 1.

Kumbukumbu ya miaka 70 ya ODUCAL
Kumbukumbu ya miaka 70 ya ODUCAL

Katika maisha yote haya ya mwanadamu utukufu wa Mungu unajidhihirisha, mwaliko wa kuweza kuwekeza zaidi katika maisha ya mwanadamu, kwa kuwa ni vyombo vya faraja katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 4 Mei 2023 kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Kikatoliki vya Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean, ODUCAL. Shirikisho hili linaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato wa uponyaji huko Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean, ambako matajiri wanazidi kuneemeka na maskini wanazidi kutopea katika umaskini. Huu ndio mwelekeo wa Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ambao kimsingi ni mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kujenga mfumo wa elimu unaojikita katika msingi wa elimu fungamanishi. Lengo ni kuwasaidia vijana kujizatiti zaidi katika elimu fungamanishi inayowataka vijana wa kizazi kipya kuwa wasikivu, wajenzi wa haki, amani, umoja na udugu wa kibinadamu katika usawa! Baba Mtakatifu anakazia mfumo wa elimu itakayosaidia pia kuleta Mfumo Mpya wa Uchumi Duniani unaojikita katika wongofu wa kiikolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anakazia pia Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa kuchangia katika sera na mikakati ya kitamaduni na kwamba, Chuo Kikuu cha Kikatoliki hakina budi pia kuwa na mwelekeo wa kimisionari, dhamana na wajibu wa Kanisa zima. Vyuo vikuu vya Kikatoliki vishiriki kikamilifu katika majiundo ya waamini, ili waweze kujikita zaidi na zaidi katika tafiti za wamisionari ili kuweza kuzama katika ufahamu wa furaha ya Injili, tayari kuwashirikisha watu wengine: Wawe tayari kujifunza na kufundisha na kwamba, mtandao wa vyuo vikuu vya Kikatoliki uwe ni mahali pa kufanyia tafiti mbalimbali, tayari kwa majiundo ya wamisionari mbalimbali.

Papa ODUCAL

 

05 May 2023, 15:15