Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Mei 2023 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Mei 2023 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mazungumzo Kati ya Papa Francisko na Maaskofu Katoliki Tanzania!

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania liliweka mbele ya Baba Mtakatifu: Fursa, matatizo, changamoto na matarajio ya Kanisa la Tanzania kwa siku za usoni, kama sehemu ya Kanisa la Kiulimwengu. Jambo kuu ni ukuaji wa miito ya kipadre licha ya changamoto nyingi zilizopo. Kuna matumaini makubwa na changamoto la hitaji la wachungaji wema, watakatifu na wachapakazi katika shamba la Bwana pamoja na ongezeko kubwa la waamini wa Kanisa Katoliki Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC kuanzia tarehe 14 hadi 21 Mei 2023 limekuwa likifanya Hija ya Kitume “Ad Limina Apostolorum Visitatio,” kwa kifupi, “Ad Limina” inayofanyika kila baada ya miaka mitano hapa mjini Vatican. Hija ya Kitume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Lengo kuu lilikuwa pamoja na mambo mengine: Kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na kutoa taarifa ya Maandishi kwa Baraza la Kipapa la Maaskofu kuhusu mwenendo mzima wa maisha na utume wa Kanisa katika Jimbo husika. Imekuwa pia ni fursa ya kujadiliana na wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Kwa hakika umekuwa ni wakati muafaka wa sala na tafakari ya kina kuhusu maisha na utume wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Mei 2023 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Flavian Matindi Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania anasema, kwamba, Baba Mtakatifu aliwapokea na kuwaonesha upendo mkubwa wa kibaba, mwonekano wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Baba Mtakatifu anakazia ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza, kukutana na kufanya mang’amuzi ya pamoja. Neno la Mungu ni ufunguo wa mang’amuzi na mwanga wa maisha ya kiroho, ili kweli maadhimisho na hatimaye ujenzi wa Kanisa la Kisinodi uweze kuwa ni sehemu ya mchakato wa toba na wongofu wa ndani. Hili ni tukio la neema na mchakato wa uponyaji unaotekelezwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Katika kipindi hiki cha maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu, Kristo Yesu anawataka waamini kutomezwa na malimwengu; kuwa wazi kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kuondokana na tabia ya kutekeleza shughuli za kichungaji kwa mazoea, ili hatimaye, kutambua kile ambacho Mwenyezi Mungu anataka kwa ajili ya Kanisa lake katika nyakati hizi na wapi anataka kulipeleka.

Ukuaji wa miito na wingi wa waamini wa Kanisa katoliki ni ishala njema.
Ukuaji wa miito na wingi wa waamini wa Kanisa katoliki ni ishala njema.

Askofu Flavian Matindi Kassala, anasema, Maaskofu walikaa pamoja na Baba Mtakatifu kama familia, Jumuiya ya wachungaji wakuu wa Kanisa au kama inavyozoeleka na wengi, Jumuiya ya Mitume, kama walivyokaa kwenye Mtaguso Mkuu wa kwanza wa Yerusalemu kama ilivyoandikwa kwenye Kitabu ya Matendo ya Mitume, Sura ya 15:7-21. Lakini baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walioamini wakasimama wakisema, Ni lazima kuwatahiri na kuwaagiza kuishika torati ya Musa. Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno hilo. Na baada ya hoja nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini. Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia, akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi; wala hakufanya tofauti kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani. Basi sasa mbona mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua. Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao. Basi mkutano wote wakanyamaza, wakawasikiliza Barnaba na Paulo wakiwapasha habari za ishara na maajabu, ambayo Mungu aliyafanya kwa ujumbe wao katika Mataifa. Na hao walipokwisha kunyamaza Yakobo akajibu, akisema, Ndugu zangu, nisikilizeni. Simeoni ametueleza jinsi Mungu hapo kwanza alivyowaangalia Mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya jina lake. Na maneno ya manabii yapatana na hayo, kama ilivyoandikwa, Baada ya mambo haya nitarejea, Nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena maanguko yake, Nami nitaisimamisha; Ili wanadamu waliosalia wamtafute Bwana, Na mataifa yote ambao jina langu limetajwa kwao; Asema Bwana, ajulishaye hayo tangu milele. Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; Tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika Mataifa; bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu. Kwa maana tangu zamani za kale Musa anao watu wahubirio mambo yake; katika kila mji husomwa kila sabato katika masinagogi."

Kusikilizana ni sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Kusikilizana ni sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania liliweka mbele ya Baba Mtakatifu: Fursa, matatizo, changamoto na matarajio ya Kanisa la Tanzania kwa siku za usoni, kama sehemu ya Kanisa la Kiulimwengu. Jambo kuu ni ukuaji wa miito ya kipadre licha ya changamoto nyingi zilizopo. Kuna matumaini makubwa na changamoto la hitaji la wachungaji wema, watakatifu na wachapakazi katika shamba la Bwana. Askofu Kassala anasema, bila shaka ongezeko hili ni matunda ya sala ya kuombea miito ndani ya Kanisa, ili Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika shamba lake. Pili, kuna ongezeko kubwa la idadi ya waamini walei nchini Tanzania, kumbe kuna hitaji la wachungaji ili kusaidia mchakato wa malezi na makuzi ya waamini walei. Ni katika muktadha huu, Maaskofu Katoliki Tanzania, walimshirikisha Baba Mtakatifu kuhusu malezi na makuzi ya miito ya kipadre na kitawa yanayotekelezwa nchini Tanzania hasa kutokana na kuongeza kwa mashirika ya kitawa na kazi za kitume nchini Tanzania. Maaskofu wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kutoa kibali kwa mashirika yaliyokuwa na hadhi ya Kijimbo kuwa na hadhi ya Mashirika ya Kipapa. Maaskofu Katoliki Tanzania wamemshirikisha Baba Mtakatifu kuhusu ushiriki wa Kanisa la Tanzania katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika utamaduni wa kusikilizana, kuamua na kutenda kwa pamoja. Kuna mambo mengi yaliyoibuliwa katika mchakato wa maadhimisho ya Siku ya Maaskofu nchini Tanzania. Huu ni uvuvio wa Roho Mtakatifu kwa Kanisa kwani maoni na ushauri vilikuwa vinatoka kwa waamini wenyewe ambao kimsingi wanaunda sehemu kubwa ya watu wa Mungu, Maaskofu na Mapadre ni wahudumu wa mafumbo matakatifu ya Mama Kanisa. Mchakato wa maadhimisho ya Sinodi umetoa fursa ya kusikiliza shida, matatizo, changamoto na matamanio halali ya watu wa Mungu nchini Tanzania. Waamini wamebainisha fursa zilizopo kwenye maisha na utume wa Kanisa na kuanza sasa kujikita katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa mwezi Oktoba 2023.

Tayari utekelezaji wa baadhi ya maamuzi umeanza kufanyiwa kazi
Tayari utekelezaji wa baadhi ya maamuzi umeanza kufanyiwa kazi

Tayari Baraza la Maaskofu Katoliki limekwisha anza kutekeleza yale mambo ambayo yako kwenye uwezo wao, yaani kwenye ngazi ya Kanisa mahalia la Tanzania, kwani Sinodi imekwisha kuanza sasa huu ni mwendelezo wake. Maaskofu walimpongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuanzisha mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Mafanikio, matatizo, changamoto pamoja na fursa mbalimbali ziliweza kujibiwa kwa ufasaha na Baba Mtakatifu Francisko mintarafu hali na mazingira ya Kanisa la Tanzania. Maaskofu wanaongoza maeneo makubwa yenye idadi kubwa ya waamini inapojitokeza hali kama hii, basi wanaweza kuomba kupatiwa Maaskofu wasaidizi, ili waendelee kujikita katika kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu nchini Tanzania. Baba Mtakatifu ameonesha ufahamu mkubwa wa Kanisa la Tanzania, changamoto na matumaini yake halali mintarafu Kanisa la Kiulimwengu. Askofu Flavian Matindi Kassala, anasema kubwa zaidi ni uhuru aliowaachia Maaskofu Katoliki Tanzania wa kuzungumza yale yote waliokuwa wamebeba nyoyoni mwao, kiasi cha Maaskofu “kunyoosha mikono” na akajibu maswali yote kwa ufasaha kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa ajili ya Kanisa la Tanzania ambalo ni sehemu ya Kanisa la Kiulimwengu. Baba Mtakatifu Francisko alikazia umuhimu wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ambalo kimsingi ni tukio endelevu na fungamani, linalowapatia waamini fursa ya kutafakari Kanisa kwa nyakati za sasa na zile zijazo ili kuwekeza kwa Kanisa lijalo, kama ilivyokuwa kwenye Mtaguso wa kwanza wa Yerusalemu kama unavyosimuliwa na Mwinjili Luka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Mitume wakapitisha sera na maazimio yanayoliongoza Kanisa hadi leo hii. Kumbe, matatizo, fursa na changamoto mbalimbali zinazolikumba Kanisa zisaidie mchakato wa ujenzi wa Kanisa linalojibu mahitaji ya wale wanaoitwa na Kristo Yesu, ili kujadiliana na kusikilizana, ili hatimaye, kuweza kujifunza kusaidiana kwa hali na moyo mkuu.

Mahojiano maalum na Askofu Flavian Kassala Matindi
Mahojiano maalum na Askofu Flavian Kassala Matindi

Maisha ya makleri, watawa na waamini walei wote hawa ni kwa ajili ya wakati ujao wa Kanisa unaofumbatwa katika uhalisia wa maisha! Kumbe, dhamana na wajibu wa waamini ni kufahamu mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwani hili ni jambo la waamini wote ambalo limeasisiwa na Baba Mtakatifu Francisko. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi anasema Baba Mtakatifu unafumbatwa katika utamaduni wa majadiliano, kusikilizana na hatimaye, maridhiano yanayoanza ndani ya familia na katika ngazi mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa. Huu ni ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaowajibisha, kila mtu akitambua kwamba, anao wajibu na dhamana ya watu wote wa Mungu kila mtu kadiri ya wito, dhamana na nafasi yake katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia hii, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Mwanzo, litaweza kujibu kwa ufasaha mahangaiko ya watu wa Mungu. Kumbe, Kanisa la Kisinodi linasimikwa katika majadiliano, sala na maongozi ya Roho Mtakatifu. Kwa kusikilizana, waamini wanaweza kutambua busara ya kesho ya Mungu; kwa kusikiliza, wanaweza kugundua uvuvio wa Roho Mtakatifu na hatimaye, waweze kumwomba Roho Mtakatifu awaongoze, ili waweze kupata maamuzi kamili. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Roho Mtakatifu ni jirani mwema, maana anakaa kwao naye yu ndani yao. Roho Mtakatifu ni Mfariji wakati wa majaribu, mahangaiko na mateso, ndiye anayewaletea waamini msamaha na nguvu ya Mungu; anayewasahihisha kwa upole, huruma na upendo. Roho Mtakatifu Mfariji ni rafiki wa kweli na ni mwaminifu anayewafunza waamini yale mambo ya kubadili, ili hatimaye, waweze kukua. Ni Roho ambaye ni mnyenyekevu hata pale anapowasahihisha waja wake, anafanya hivyo kwa upole, bila kuondoa imani kwao, bali anawapatia uhakika kuhusu uwepo na ukaribu wa Mungu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Roho Mtakatifu Mfariji kama Wakili na mtetezi, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote waliyoambiwa na Kristo Yesu. Askofu Flavian Matindi Kassala, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania amehitimisha mahojiano haya maalum kuhusu mambo msingi yaliyojiri wakati Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kwamba, Roho Mtakatifu atawakumbusha yote. Na yale ambayo hayakueleweka kutokana na vikwazo mbalimbali vya: umri, uwezo wa uelewa kimaarifa na mambo yote ya kielimu, kwani Roho Mtakatifu yuko juu ya mambo yote haya: Kumbe mkazo katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni kusikilizana, kutoa muda wa kutafakari ili “kupumua” na hatimaye, kumpatia fursa Roho Mtakatifu ili aweze kutoa majibu!

Papa na Maaskofu Tanzania

 

23 May 2023, 14:31