Vyama, mashirika na jumuiya mbalimbali za Kitume ndani ya Kanisa ni kama shule ya imani, matumaini na mapendo. Vyama, mashirika na jumuiya mbalimbali za Kitume ndani ya Kanisa ni kama shule ya imani, matumaini na mapendo.   (@Comunità Sant'Egidio)

Nia za Papa Francisko Kwa Mwezi Mei 2023: Vyama na Mashirika ya Kitume: Utume wa Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za jumla kwa Mwezi Mei 2023 anapenda kuvialika vyama, mashirika na jumuiya mbalimbali za kitume ndani ya Kanisa kutambua kwamba, wao ni zawadi na amana ya Kanisa, mwaliko kwa wanachama wake kujikita zaidi na zaidi katika majadiliano kwa ajili ya huduma ya uinjilishaji inayotekelezwa na Mama Kanisa. Waamini wawe tayari kujibu mwito wa Roho Mtakatifu ili kukabiliana na changamoto mamboleo kwa ari kuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vyama, mashirika na jumuiya mbalimbali za Kitume ndani ya Kanisa ni kama shule ya imani, matumaini na mapendo. Hapa ni mahali ambapo waamini wanaweza kusaidiana katika kukuza, kulinda na kudumisha: imani, maisha ya kisakramenti, maadili na sala. Karama ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa waamini ndani ya Kanisa, tukio ambalo ni endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Vyama na mashirika ya kitume yaliyoibuka baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ni zawadi kubwa kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Vinapaswa kupokelewa kwa imani na moyo wa shukrani, kama rasilimali kwa Kanisa, ili hatimaye, viweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za jumla kwa Mwezi Mei 2023 anapenda kuvialika vyama, mashirika na jumuiya mbalimbali za kitume ndani ya Kanisa kutambua kwamba, wao ni zawadi na amana ya Kanisa, mwaliko kwa wanachama wake kujikita zaidi na zaidi katika majadiliano kwa ajili ya huduma ya uinjilishaji inayotekelezwa na Mama Kanisa. Baba Mtakatifu anavitaka vyama na mashirika haya, daima yawe tayari kujibu mwito wa Roho Mtakatifu, ili kuweza kukabiliana na changamoto, ili kuleta mabadiliko katika ulimwengu mamboleo. Huu ni wito na mwaliko wa kuhakikisha kwamba, vyama, mashirika na jumuiya mbalimbali zinaweka karama zao kwa ajili ya huduma ya uinjilishaji, mahitaji ya walimwengu na hivyo kuondokana na kishawishi cha kutaka kujifungia katika ubinafsi wao.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio katika mchakato wa uinjilishaji wa kina.
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio katika mchakato wa uinjilishaji wa kina.

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha linavipongeza vyama, mashirika na jumuiya mbalimbali za Kitume ndani ya Kanisa kwa kutenda kadiri ya karama zao kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii. Vimekuwa msaada mkubwa kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; huduma kwa familia zinazokabiliana na changamoto za umaskini na hali ngumu ya maisha sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Shughuli zote hizi ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu. Hizi zote ni juhudi za makusudi kabisa zinazotekelezwa na waamini walei ndani ya Kanisa kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko baada ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao! Haya ni majadiliano na Injili ya Kristo. Kila chama, shirika na jumuiya za Wakristo zina karama zao, lakini zote hizi ni kwa ajili ya ujenzi wa ushirika wa waamini tayari kutekeleza utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba, vyama, mashirika na jumuiya hizi hazijifungii katika ubinafsi wao, bali vinashiriki kikamilifu katika wito na utume wa Mama Kanisa ulimwenguni. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe wa vyama hivi kuhakikisha kwamba vinashirikiana kikamilifu na Maaskofu mahalia, Parokia na Jumuiya zao ndogo ndogo za Kikristo ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika hali na mazingira yao. Vyama hivi viwe ni mahali muafaka pa wajumbe wake kukutana na Mwenyezi Mungu katika uhalisia wa maisha, ili hatimaye, kupata utimilifu wake katika huduma kwa watu wa Mungu.

Vyama na mashirika ya kitume yawe ni chachu ya uinjilishaji.
Vyama na mashirika ya kitume yawe ni chachu ya uinjilishaji.

Kwa upande wake, Padre Frédéric Fornos S.J, Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko anavihamasisha vyama, mashirika na jumuiya za Kikanisa kuwa safarini tayari kujibu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu changamoto katika ulimwengu mamboleo, mintarafu karama zao, tayari kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika medani mbalimbali za maisha. Anapenda kuchukua fursa hii, kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Mei 2023. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, waamini wasali ili kumwomba Roho Mtakatifu wa maisha na ukweli; ushirika na upendo aweze kuwashukia wote kama ilivyokuwa wakati wa Pentekoste. Kwa kweli Kanisa na Ulimwengu unahitaji uwepo angavu wa Roho Mtakatifu, ili aweze kushusha karama na mapaji yake.

Nia za Mwezi Mei 2023

 

02 May 2023, 16:00