Papa Francisko: Majadiliano ya Kidini Yanasimikwa Katika Ukweli na Uhalisia wa Maisha
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Damu ya Wakristo, itaendelea kuwa ni mbegu ya Ukristo na mchakato wa umoja wa Wakristo. Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbalimbali za dunia ni mambo yanayowaunganisha wote bila ubaguzi hata kidogo. Wakristo wote wanateseka na kudhulumiwa kwa sababu ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kumbe, uekumene wa damu una nguvu sana kama kielelezo cha ushuhuda wa imani yenye mvuto na mashiko! Takwimu zinaonesha kwamba, hata katika ulimwengu mamboleo, bado kuna Wakristo wanaoendelea kuteseka kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza.
Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu Injili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Mei 2023 amekutana na kuzungumza na Taasisi ya Majadiliano ya Kidini kutoka nchini Argentina, amekazia umuhimu wa dini na madhehebu mbalimbali ya Kikristo kujikita katika majadiliano ili kuondokana na tabia ya kudhaniana vibaya, dhuluma na nyanyaso; tayari kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wazazi na walezi wanayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanawarithisha watoto wao amana, utajiri na tunu njema za maisha ya kiroho kutoka kwa waamini wa dini na madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Baba Mtakatifu anasema, amebahatika kukutana, kusoma na kuishi na Wayahudi, ambao bado anayo kumbukumbu njema ya ushuhuda wa maisha na imani yao. Ufahamu na uelewa wake wa majadiliano ya kiekumene ni matunda ya urithi kutoka kwa Bibi yake.
Kumbe, majadiliano ya kweli yanakita mizizi yake katika wongofu wa ndani, uzoefu na mang’amuzi ya maisha yanayopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, anayejifunua taratibu na tofauti katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anakazia njia ya majadiliano katika ukweli na uhalisia wa maisha ya mwanadamu na waamini wa dini na madhehebu mbalimbali ya Kikristo, ili kuweza kushirikiana na kushikamana katika maisha. Huu ni mwaliko kwa waamini wa dini na madhehebu mbalimbali ya Kikristo kushirikishana historia na mang’amuzi ya maisha, ili kujenga Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume. Kuheshimiana na kuthaminiana ni mambo msingi katika majadiliano ya kidini na kiekumene. Mwishoni, aliwaomba wajumbe, kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amewashukuru kwa yale mambo mema na mazuri wanayotenda kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Argentina.