Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 5 Mei 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 5 Mei 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM   (Vatican Media)

Papa Francisko: Tasaufi za Malipizi Dhidi ya Nyanyaso za Kijinsia

Papa amekutana na kuzungumza na wajumbe Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo na kutoa aina tatu za tasaufi za malipizi: katika maisha kwa kukumbuka kazi ya uumbaji ili kurejesha matumaini dhidi ya hali ya kukata tamaa na kifo. Pili, Kashfa ya nyanyaso za kijinsia imepelekea madonda makubwa kwa Kanisa na jamii katika ujumla wak. Tatu ni kutengeneza heshima na upole wa Mungu, kwa kusaidiana kubeba machungu ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM, ambayo kwa sasa iko chini ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa ni utekelezaji wa maamuzi yaliyotolewa na Baraza la Makardinali takribani miaka kumi iliyopita na Kanisa limejifunza mengi katika kipindi hiki. Tukio la kwanza la kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa liliibuliwa huko Jimbo kuu la Boston, nchini Marekani. Vita, baa la njaa na umaskini na tabia ya kutokuguswa na mahangaiko ya wengine ni ukweli unaosikika sehemu mbalimbali za dunia. Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa ni hatari kwani linakwamisha mchakato wa uwepo endelevu wa Mungu anayeokoa na kwamba, jitihada za kupambana na kashfa hii ni kielelzo cha upendo kwa Mungu. Mama Kanisa anaomba msamaha kwa makosa yaliyotendeka na yale mema na mazuri ambayo viongozi wa Kanisa walipaswa kutenda lakini hawakutenda, na hali hii ikageuka kuwa ni kashfa kwa watu wengi na Jumuiya ya waamini katika ujumla wake. Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia.  Katika barua hii, Baba Mtakatifu anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanapaswa kuwajibika barabara. Sheria hizi zinawalazimisha wakleri na watawa kutoa taarifa pale kunapokuwepo na shutuma kama hizi. Kila Jimbo linapaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kutoa taarifa za shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Tasaufi za malipizi dhidi ya nyanyaso za kijinsia
Tasaufi za malipizi dhidi ya nyanyaso za kijinsia

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 5 Mei 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM na kutoa aina tatu za tasaufi za malipizi: katika maisha kwa kukumbuka kazi ya uumbaji ili kurejesha matumaini dhidi ya hali ya kukata tamaa na kifo. Pili, Kashfa ya nyanyaso za kijinsia imepelekea madonda makubwa kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Tatu ni kutengeneza heshima na upole wa Mungu, kwa kusaidiana kubeba machungu ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Tasaufi ya malipizi katika maisha kwa kukumbuka kazi ya uumbaji ili kurejesha matumaini dhidi ya hali ya kukata tamaa na kifo, kwani kwa baadhi ya watu kashfa hii ni jambo lisiloweza kuvumilika. Hali kama hii imewakumba hata viongozi wa Kanisa walioshindwa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao, kiasi hata cha kuathiri mchakato wa kutangaza na hatimaye kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe, kuendelea kuwapatia imani wale wote wanaokutana na kushirikishana machungu kama haya katika maisha, hata kama ni hatua ndogo tu imekwisha kupigwa, kamwe wasikate tamaa, bali wapige moyo konde na kusonga mbele. Pili, Kashfa ya nyanyaso za kijinsia imepelekea madonda makubwa kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Hii ni kashfa pengine ambayo imetendeka ndani ya familia, jumuiya na hata katika jamii, kiasi kwamba, inakuwa ni chanzo cha kinzani na mipasuko ya kijamii katika nyoyo zao.

Ninyi ni nuru ya ulimwengu
Ninyi ni nuru ya ulimwengu

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, pale ambapo maisha yametikiswa, kupondeka na hata kugawanyika, wajitahidi kurejesha imani na matumaini; amani na utulivu kati yao na Kanisa. Malipizi ya kashfa hizi ni Njia ya Msalaba wa Kristo Yesu, ili kuwarejeshea tena watu matumaini waliyopoteza. Kumbe, waathirika wanapaswa kupokelewa, kusikilizwa na kufarijiwa. Tatu ni kutengeneza heshima na upole wa Mungu, kwa kusaidiana kubeba machungu ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, kielelezo cha historia ya kazi ya ukombozi. Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu ni alama na chemchemi ya huruma ya Mungu, toba na wongofu wa ndani, mwaliko kwa Mama Kanisa kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa. Wajumbe, waendelee kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuyasaidia Makanisa mahalia katika uhalisia wa maisha ya kila siku katika maparokia, seminarini; katika mchakato wa majiundo na malezi ya Makatekista, walimu wa dini shuleni pamoja na wafanyakazi katika shughuli za kichungaji. Kumbe, kuna haja ya kurithishana uzoefu na mang’amuzi; kwa kuheshimu na kuthamini utu wa kila mtu. Viongozi wa Kanisa wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma. Ulinzi na usalama vitaweza kufanikiwa tu, ikiwa kama kutakuwa na wongofu wa kichungaji kati ya viongozi wa Kanisa. Baba Mtakatifu ameridhishwa na juhudi zinazofanywa na Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM, katika malezi na huduma kwa waathirika Barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini. Ni jambo lisilokubalika na kwamba, baadhi ya maeneo yamepewa programu bora, wamegharimiwa, waathirika pamoja na familia zao wanaheshimiwa, wakati sehemu nyingine za ulimwengu watu wanaendelea kuteseka kutokana na kimya kikuu au kukatishwa tamaa wanapoonesha dalili za kutaka kuzungumzia nyanyaso zilizowasibu maishani. Katika hali na mazingira kama haya, Kanisa halina budi kuwa ni mfano bora wa ukarimu kwa kuwapokea waathirika pamoja na kutenda kwa hekima na busara!

Tasaufi ya Malipizi

 

05 May 2023, 15:32