Ujenzi wa Familia Inayosimikwa Katika Udugu Wa Kibinadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Umuhimu na ukitovu cha familia kuhusiana na mtu na jamii umeelezwa kwa mkazo na kurudiarudia katika Maandiko Matakatifu. Ni katika familia ndipo mtu hujifunza upendo na uaminifu wa Mungu na sababu ya kuupokea upendo na uaminifu huo. Kristo Yesu alizaliwa na kuishi katika familia, akakubali hali na tabia ya familia yake na akaipatia ndoa heshima ya juu kabisa, akaifanya iwe Sakramenti. Kwa kuangaziwa na ujumbe wa Biblia, Kanisa linaichukulia familia kuwa ni jumuiya ya kwanza katika jamii ya asili, ikiwa na haki ambazo ni sahihi kwake na kuiweka familia katika kitovu cha maisha ya jamii. Familia ina umuhimu wa pekee kuhusiana na mtu. Jumuiya ya asili, familia, ambamo mahusiano na mafungamano ya jamii kiutu yanastawi, inatoa mchango wa aina yake, usio na mbadala katika uzuri wa jamii. Ni katika familia tunu za kimaadili zinafundishwa kuanzia mwanzo wa uhai. Ni katika familia mtu hujifunza uwajibikaji katika jamii na ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu. Rej. Mafundisho Jamii ya Kanisa, 209-214.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu mwaka 2022 alifanya hija ya kichungaji Jimboni Asti, huko kwenye asili yake, akapata nafasi ya kukutana na ndugu, jamaa na marafiki; akakutana na Kanisa mahalia kama familia ya Mungu na baadaye na akakutana na raia wengine wote, kielelezo cha familia inayotembea kufuata tunu msingi za Kiinjili, katika ubora, utajiri, fursa na changamoto mbalimbali zinazoiandama familia. Ijumaa tarehe 5 Mei 2023, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na familia ya Mungu kutoka Jimbo Katoliki la Asti, Kaskazini mwa Italia. Katika mazungumzo yake amekazia kuhusu umuhimu wa familia, mabadiliko ya familia yaliyoletwa na Kristo Yesu katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu ndiye aliyeleta mageuzi makubwa mintarafu familia kama yanayovyosimuliwa na Wainjili Mathayo, Marko na Luka: “Alipokuwa katika kusema na makutano, tazama, mama yake na ndugu zake walikuwa wakisimama nje, wataka kusema naye. Mtu mmoja akamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wamesimama nje, wanataka kusema nawe. Akajibu, akamwambia yule aliyempasha habari, Mama yangu ni nani? Na ndugu zangu ni akina nani? Akawanyooshea mkono wanafunzi wake, akasema, Tazama, Mama yangu na ndugu zangu! Kwa maana ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.” Mt 12:46-50: Rej. Mk 3:31-35; Lk 8:19-21.
Mabadiliko makubwa katika sehemu hii ya Maandiko Matakatifu si mahusiano na mafungamano ya damu, bali upendo kwa Kristo Yesu unaoleta mabadiliko katika mahusiano ya kifamilia yanayosimikwa katika majitoleo, shukrani na huduma makini. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni vyema na haki kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai, lakini shukrani kubwa zaidi zinamwendea Kristo Yesu ambaye kwa njia ya Ubatizo anawashirikisha waja wake katika familia kubwa ya wafuasi wa Kristo Yesu, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu. Msimamo huu wa familia unatoa mwelekeo na mafungamano ya maisha ya Kanisa kama familia ya Mungu na ile familia ya kawaida inayotoa fursa ya kukua na kukomaa katika sadaka na majitoleo, kwa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kujikita katika ukarimu pamoja na tunu msingi za kiutu. Ndugu wamoja ni neno ambalo lina maana kubwa katika mahusiano na mafungamano ya kijamii, kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa ndani ya familia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Ndugu wamoja ni msingi unaowawezesha waamini kutembea kwa pamoja katika upendo, huduma, msamaha na huku wakisaidiana kwa hali na mali.