Papa kwa washairi na waandishi Kanisa linahitaji kipaji chao!
Na Angella Rwezaula,- Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 27 Mei 2023 amekutana na washiriki wa Warsha ya “Civilta’ Cattolica na Chuo Kikuu cha Georgetown kuhusu mada ya “maarifa ya kupambanua mazuri ya kimataifa ya mawazo ya Kikatoliki”. Ameanza salamu kwa Mkurugenzi wa Gazeti la Civilta Cattolica, Padre Antonio Spadari (Js) baada ya ufupi wa hotuba yake, Profesa John DeGioia Mkuu wa Chuo Kikuu cha Georgetown. Vile vile furaha yake kukutana nao wakati wanashikiri wataka ambao inawaleta pamoja washairi, waandishi wa vitabu, watayarishaji wa filamu na wakurugenzi kutoka sehemu mbali mbali za ulimwengu kwa kuzungukia mada ya mawazo ya ushairi na msukumo wa Kikatoliki. Baba Mtakatifu hata hivyo amemgeukia na kumsalimia Martin Charles Scorsese mzaliwa wa New York Marekani mnamo 17 Novemba 1942 ambaye ni mkurugenzi na mtayarishaji wa filamu, mwandishi wa skrini na mwigizaji mwenye uraia wa Italia. Mshiriki wa Hollywood Mpya, na ambaye anachukuliwa kuwa mmoja wa wakurugenzi wakuu na muhimu zaidi katika historia ya filamu. Dhamira kuu za filamu zake ni vurugu za silika za mwanadamu na uhusiano wake na hatia, dhambi na dini. Kwa hiyo Papa Franciso amesema: Nina furaha kukutana nawe: wewe ni jasiri, wewe… Asante kwa kuja na mke wako”. Kwa hiyo amesema jinsi ambavyo anajua katika siku hizi wamekuwa wakitafakari juu ya mitindo ambayo imani inahoji maisha ya kisasa, na hivyo kujaribu kujibu njaa ya maana.”
Njaa ya maana: lakini haina maana ya kupunguza kwa dhana, hapana. Ni maana ya jumla ambayo inachukua mashairi, ishara, hisia. Maana ya kweli si ile ya kamusi: hiyo ndiyo maana ya neno na neno ni chombo cha kila kilichomo ndani yetu”. Papa ameeleza jinsi ambavyo amekuwa akipenda washairi na waandishi wengi maishani mwake, ambao anamkumbuka sana ni Dante, Dostoevsky na wengine. Pia amependa kuwashukuru wanafunzi wangu katika Chuo cha Maria Safi wa Mtakatifu Fe, ambao alishiriki nao wakati wa mafunzo yake alipokuwa mdogo na kufundisha fasihi. “Maneno ya waandishi yalinisaidia kujielewa mwenyewe, ulimwengu, watu wangu; lakini pia kuimarisha moyo wa mwanadamu, kuimarisha maisha yangu binafsi ya imani, na hata kazi yangu ya uchungaji, hata sasa katika huduma hii. Kwa hiyo, neno la fasihi ni kama mwiba katika moyo unaotusukuma kutafakari na kutuweka njiani. Shairi liko wazi, linakutupa mahali pengine. Kuanzia kwenye uzoefu huu wa kibinafsi, ambapo Papa amependa kushirikisha na wao baadhi ya mambo ya kuzingatia kuhusu umuhimu wa huduma yao.
Kwanza kabisa amependa kueleza kwamba “ninyi ni macho ambayo yanayotazama na ambayo yanaota”, Sio kutazama tu, lakini pia kuota. Sisi wanadamu tunatamani ulimwengu mpya ambao pengine hatutauona kikamilifu kwa macho yetu wenyewe, hata hivyo tunautamani, tunautafuta, tunauota. Mwandishi wa Amerika ya Kusini alisema kwamba tuna macho mawili: moja la mwili na lingine la kioo. Kwa lile la mwili tunaangalia kile tunachokiona, na lile cha kioo tunaangalia kile tunachoota”, Papa ameongeza :“ sisi ni maskini ikiwa tutaacha kuota, sisi ni masikini”. Baba Mtakatifu akiendelea amekazia kusema kwamba “Msanii ni mtu ambaye kwa macho yake anatazama na kuota kwa wakati mmoja, huona zaidi, anatabiri, anatangaza njia tofauti ya kuona na kuelewa mambo yaliyo mbele ya macho yetu. Kwa hakika, ushairi hauzungumzii ukweli kuanzia kanuni dhahania, bali kwa kusikiliza ukweli wenyewe: kazi, upendo, kifo na mambo yote madogo madogo yanayojaza maisha. Na, kwa maana hiyo, inatusaidia “kuielewa sauti ya Mungu pia kutokana na sauti ya wakati”. Wao kwa kumnukuu Paul Claudel alisema ni “jicho la kusikiliza”.
Kwa kufafanua Baba Mtakatifu alisema: “Jicho linalosikiliza”, kwamba Sanaa ni dawa ya mawazo ya hesabu na usawa; ni changamoto kwa mawazo yetu, kwa njia yetu ya kuona na kuelewa mambo. Na kwa maana hiyo Injili yenyewe ni changamoto ya kisanii, yenye gharama ya kimapinduzi ambayo wanaitwa kutoa shukrani kwa fikra yao kwa neno linalopinga, kupiga simu, kupiga kelele. Leo Kanisa linahitaji fikra zao, kwa sababu linahitaji kupinga, kuita na kupiga kelele! Hata hivyo, kwa kuoongeza Papa amependa kusema jambo la pili kuwa wao pia “ni sauti ya wasiwasi wa kibinadamu. Mara nyingi wasiwasi huzikwa ndani ya vilindi vya moyo”. Wanajua vizuri kwamba msukumo wa kisanii haufariji tu, bali pia unasumbua, kwa sababu unaonesha ukweli mzuri na wa kutisha wa maisha. Sanaa ni uwanja wenye rutuba ambapo upinzani wa juu wa ukweli huoneshwa, ambao daima unahitaji lugha ya ubunifu na isiyo ngumu, yenye uwezo wa kuwasilisha ujumbe na maono yenye nguvu.
Kwa mfano, Papa ameomba kufikiria wakati Dostoevsky katika kitabu “Ndugu wa Karamazov” alielezea juu ya mtoto mdogo, mtoto wa mtumishi, ambaye alitupa jiwe na kugonga mguu wa mmoja wa mbwa wa bwana wake. Kisha bwana huyo aliamlisha mbwa wote dhidi ya mtoto. Yeye alikimbia na kujaribu kujiokoa na ghadhabu ya kundi, lakini anaishia kuraruliwa vipande vipande chini ya macho ya jenerali yaliyoridhika na macho ya mama yake ya kukata tamaa. Sehemu hii ina nguvu kubwa ya kisanii na kisiasa kwani inazungumza juu ya ukweli wa jana na leo, juu ya vita, migogoro ya kijamii, ubinafsi wetu wa kibinafsi. Kwa kutaja kifungu kimoja tu cha kishairi kinachotufanya tuendelee mbele. Baba Mtakatifu kwa kuongezea amesema kwamba hazungumzii tu juu ya ukosoaji wa kijamii ulio katika kifungu hicho. Amezungumzia juu ya mvutano wa kiroho, na ugumu wa maamuzi, wa hali inayopingana ya uwepo. “Kuna mambo katika maisha ambayo, wakati mwingine, hatuwezi hata kuelewa au ambayo hatuwezi kupata maneno sahihi. Na hiyo ndiyo ardhi yao yenye rutuba, uwanja wao wa hatua. Na hapo pia ni mahali ambapo Mungu mara nyingi anafanya uzoefu. Uzoefu ambao daima unafurika: ambapo huwezi kuuchukua, unauhisi na unakwenda mbali zaidi; uzoefu wa Mungu daima hufurika, kama beseni ambalo maji humwagika mfululizo na baada ya kujaa maji hufurika.
Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu ndio amependa kuwaomba kwa siku hiyo ili waweze kwenda mbele zaidi ya mipaka iliyofungwa na iliyoainishwa, kuwa wabunifu, bila kudhibiti wasiwasi wao na wa wanadamu. Kwa kuongezea amesema “Ninaogopa mchakato huu wa ufugaji, kwa sababu unaondoa ubunifu, unaondoa ushairi.” Kwa neno la mashairi, kukusanya shauku zisizo na utulivu ambazo hukaa ndani ya moyo wa mwanadamu, ili wasipate baridi na wasiondoke. Kazi hii inamruhusu Roho kutenda, kuunda maelewano ndani ya mivutano na migongano ya maisha ya mwanadamu, kuweka moto wa shauku nzuri kuwaka na kuchangia ukuaji wa uzuri katika aina zake zote, uzuri huo ambao unaoneshwa kwa usahihi kupitia utajiri wa sanaa. Hii ni kazi yao kama washairi, waandishi wa hadithi, wakurugenzi, wasanii ili kutoa uhai, kutoa kiungo, kutoa neno kwa kila kitu ambacho wanadamu wanapata, kuhisi, ndoto, kuteseka, kuunda maelewano na uzuri. Ni kazi ya kiinjilisha inayotusaidia kumwelewa Mungu vizuri zaidi, kama mshairi mkuu wa wanadamu. Papa ameongeza “Je, watakukosoa? Sawa, kubeba mzigo mkubwa wa ukosoaji, huku pia ukijaribu kujifunza kutoka katika ukosoaji. Lakini bado usiache kuwa asili, ubunifu. Msikose mshangao wa kuwa hai.”
Kwa hiyo, macho ambayo huota, sauti ya kutotulia kwa mwanadamu; na kwa hivyo wao pia wana jukumu kubwa. Na lipi? Ni jambo la tatu ambalo Papa Francisko amependa kuwambia kwamba wao ni miongoni mwa wale wanaounda mawazo ya watu. Hii ni muhimu. Hakika, kazi yao ina matokeo juu ya mawazo ya kiroho ya watu wa wakati wetu, hasa kuhusu sura ya Kristo. Katika wakati wetu kama alivyotanguliza kusema: “Tunahitaji fikra ya lugha mpya, ya historia na picha zenye nguvu, za waandishi, washairi, wasanii wenye uwezo wa kutangaza ujumbe wa Injili kwa ulimwengu, wa kutufanya tumuone Yesu.” Kazi yao amesema inatusaidia kumwona Yesu, kuponya mawazo yetu kutoka kwa kila kitu kinachoficha uso wake au, mbaya zaidi, kutoka kwa kila kitu kinachotaka kumfuga. Kuficha uso wa Kristo, kana kwamba kujaribu kufafanua na kufunga katika mipango yetu, kunamaanisha kuharibu sura yake: Bwana daima hutushangaza, Kristo daima ni mkuu, yeye daima ni fumbo ambalo kwa namna fulani hutuepuka. Ni ngumu kuiweka sura katika ukuta. Yeye daima hutushangaza, na wakati hatuhisi kwamba Bwana anatushangaza, kitu hakifanyi kazi na mioyo yetu haikamilika na imefungwa.
Papa hapo ameonesha changamoto kwa fikira za Wakatoliki wa wakati wetu, changamoto ambayo wamekabidhiwa ya “kutoeleza” fumbo la Kristo, ambalo kwa hakika haliwezi kuisha; lakini kulifanya lituguse, tulisikie karibu mara moja, litufikishe kama uhalisi ulio hai, na tulishike uzuri wa ahadi yake. Kwa sababu ahadi yake inasaidia mawazo yetu: inatusaidia kuwazia maisha yetu, historia yetu, na wakati ujao wa wanadamu kwa njia mpya! Na hapo Papa Francisko amekazia kusema kuwa ndio ilikuwa kazi nyingine bora ya Dostoevsky, ndogo lakini ambayo ina vitu hivi vyote ndani mwake ya historia kutoka chini ya ardhi. Kwa hiyo kumbukumbu kutoka chini ya ardhi. Mle ndani kuna ukuu wote wa ubinadamu na maumivu yote ya wanadamu, taabu zote, pamoja. Hiyo ndiyo njia. Papa alishukuru kwa huduma yao na amewaeleza waendelee “kuota, kuwa na wasiwasi, kuwazia maneno na maono ambayo hutusaidia kuelewa fumbo la maisha ya mwanadamu na kuongoza jamii zetu kuelekea uzuri na udugu wa ulimwengu wote. Usaidie tena kufungua mawazo yetu ili iweze kushinda mipaka finyu ya nafsi na kufungua kwa siri takatifu ya Mungu. Kusonga mbele, bila kuchoka, kwa ubunifu na ujasiri.” Amewabariki na kuwaombea; na wao pia, wamwombee.