Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko Kwa Watoto Wagonjwa Kutoka Poland
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kristo Yesu anawaalika wafuasi wake kuwa ni Wasamaria wema kwa kuwekeza katika huduma ya tiba, ili kuokoa maisha ya watu, kielelezo cha upendo wa Mungu, ambaye kimsingi ni chanzo, maana na hatima ya maisha ya binadamu. Wajibu wa kimaadili, ukiongozwa na imani, uwasaidie watu kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, chanzo cha uhai. Kifo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na wanasayansi wanapaswa kutambua ukweli huu. Daima mgonjwa apewe tiba hata wale wenye magonjwa sugu na ya muda mrefu. Hii ni huduma ya tiba: kimwili, kisaikoljia, kijamii, kifamilia na katika maisha ya kiroho, kwa kuzingatia taalimungu ya maisha ya mwanadamu. Wadau mbalimbali wamsaidie mgonjwa kujiandaa kufa kifo chema, akiwa anasindikizwa na neema ya utakaso na upendo wa Mungu. Pale ambapo imani na matumaini vinakosekana wakati mgonjwa anapokaribia kifo kuna hatari ya kutumbukia katika kifolaini au msaada wa kutaka kujinyonga. Kuna umuhimu wa kuheshimu, kulinda, kupenda na kuhudumia zawadi ya maisha ya kila mwanadamu sanjari na kuhakikisha kwamba, wagonjwa wanasindikizwa katika hatua mbalimbali za ugonjwa wao. Ni muda wa kumwilisha huruma na mapendo katika matendo halisi. Ikumbukwe kwamba, matendo ya huruma ndicho kipimo cha hukumu ya mwisho!
Ni katika muktadha wa huduma na faraja kwa wagonjwa, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 29 Mei 2023 amekutana na kuzungumza na watoto wagonjwa kutoka Poland na kuhakikishia kwamba, Kristo Yesu daima yuko pamoja nao hata katika mateso na mahangaiko ya ugonjwa wao. Kumbe, huu ni mwaliko wa kuwa ni Mitume wa upendo wa Mungu katika maisha kwa kutambua kwamba, wanakabiliana na changamoto nyingi katika maisha, kwani wanapaswa kupewa tiba, kuishi na ugonjwa na wakati mwingine, hata mgonjwa mwenyewe anakosa nguvu, ari na ujasiri wa kusonga mbele, lakini Kristo Yesu amewahakikishia uwepo wake wa daima miongoni mwao ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo. Uwepo na ukaribu huu, unaoneshwa pia na: wazazi, ndugu, jamaa na madaktari, ili kuwasaidia kusonga mbele kwa kutambua kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Mungu, kumbe, wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa upendo wa Mungu na Kanisa ulimwenguni. Kristo Yesu anawahitaji watoto hawa kama mashuhuda wa upendo wa Mungu, huku wakitangaza na kushuhudia huruma, upendo na furaha, kwani pembeni mwao yupo pia Bikira Maria, Faraja ya wagonjwa, hasa pale wanapoelemewa na uzito wa ugonjwa, Bikira Maria yupo kwa upendo wake wa kimama!