Tafuta

Kardinali Pietro Parolin amesema, Vatican itaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake hadi haki ya amani ipatikane nchini Ukraine. Kardinali Pietro Parolin amesema, Vatican itaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake hadi haki ya amani ipatikane nchini Ukraine.  (ANSA)

Vatican Itaendelea Kusimama Kidete Ili Kuhakikisha Kwamba Haki ya Amani Inarejea Ukraine

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, alitumia fursa hii, kuwasilisha salam na matashi mema kwa wakuu wa nchi na Serikali waliohudhuria mkutano huu na kukazia umuhimu wa Umoja wa Ulaya kujikita katika mchakato wa ujenzi wa amani. Lakini, vita inayoendelea kati ya Urussi na Ukraine inatia mashaka, kiasi cha kufutilia mbali ndoto ya amani Ni muhimu kutekeleza ndoto ya amani mintarafu mtazamo wa waasisi wa Umoja wa Ulaya na Papa Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mnamo tarehe 7 Novemba 2022, Kamati ya Mawaziri wa Umoja wa Ulaya, EU ilikubali kwamba Mkutano wa 4 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Baraza la Ulaya ufanyike chini ya Urais wa Iceland wa Kamati ya Mawaziri huko Reykjavik, Iceland, tarehe 16 na 17 Mei 2023. Uamuzi wa kuitisha Mkutano huu ulifuatia taarifa iliyowasilishwa kunako mwaka Oktoba 2022. Taarifa ilibainisha changamoto zilizokabidhiwa kwa wakuu wa nchi na Serikali mbalimbali zinaonesha kwamba, Umoja wa Ulaya, EU unakabiliwa na changamoto pevu zinazohitaji uwekezaji zaidi katika masuala ya haki msingi za binadamu, demokrasia na utawala wa sheria. Kuna haja pia ya kuendelea kukazia umakini na ufanisi wa ulinzi wa haki msingi za binadamu katika mfumo ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Mkataba wa haki msingi za binadamu na utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama ya Umoja wa Ulaya ni mambo yanayopaswa kuvalia “njuga”. Taarifa iliweka bayana kuhusu suala la ushirikiano kati yake na Umoja wa Mataifa, Ukraine pamoja na mahusiano na serikali ya Urussi. Taarifa hivyo imebainisha umuhimu wa Umoja wa Ulaya kuzuia sanjari na kudhibiti vipigo vya wanawake majumbani.

Haki ya amani nchini Ukraine
Haki ya amani nchini Ukraine

Katrin Jakobsdóttir, Waziri Mkuu wa Iceland, anasema Mkutano huo unapaswa kuuongoza Umoja wa Ulaya katika kukabiliana na changamoto za dharura, kama vile athari za mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na mabadiliko ya haraka ya kiteknolojia, ambayo yana athari kubwa kwa haki msingi za binadamu. Iceland itaendeleza, haki za wanawake na wasichana, mazingira, watoto na vijana. Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, ametumia fursa hii, kuwasilisha salam na matashi mema kwa wakuu wa nchi na Serikali waliohudhuria mkutano huu na kukazia umuhimu wa Umoja wa Ulaya kujikita katika mchakato wa ujenzi wa amani. Lakini, vita inayoendelea kati ya Urussi na Ukraine inatia mashaka, kiasi cha kufutilia mbali ndoto ya amani. Jambo la msingi ni kufikiria umuhimu wa ujenzi wa amani ya kudumu mintarafu Waasisi wa Umoja wa Ulaya pamoja na Baba Mtakatifu Francisko. Ni jambo lisilokubalika kuona uvamizi wa Urussi nchini Ukraine ukiendelea na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Jumuiya ya Ulaya haina budi kutambua mateso na vifo vya watu wa Ukraine kutokana na vita hii. Umefika wakati wa kufanya maamuzi magumu ili kuhakikisha uwepo wa haki ya amani nchini Ukraine pamoja na maeneo mengine kwenye Umoja wa Ulaya. Vatican itaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake hadi haki ya amani ipatikane nchini Ukraine.

Amani Ukraine
18 May 2023, 17:12