Mkutano mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, umefunguliwa tarehe 31 Mei 2023 na utahitimishwa tarehe 6 Juni 2023. Mkutano mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, umefunguliwa tarehe 31 Mei 2023 na utahitimishwa tarehe 6 Juni 2023.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Mashirika ya Kimisionari Ya Kipapa, PMS Kwa Mwaka 2023

Utume wa kimisionari, Karama ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, na Matarajio na ndoto za upyaisho wa huduma ya uinjilishaji kwa Kanisa zima. Baba Mtakatifu ameishukuru mihimili yote ya utume wa uinjilishaji ndani ya Kanisa mintarafu mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kutambua kwamba, kila Mkristo amepokea karama za Roho Mtakatifu hivyo anatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, wema, huruma na upendo wa Yesu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, umefunguliwa tarehe 31 Mei 2023 na utahitimishwa tarehe 6 Juni 2023. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 3 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano huu mkuu kwa kukazia: Utume wa kimisionari, Karama ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, na Matarajio na ndoto za upyaisho wa huduma ya uinjilishaji kwa Kanisa zima. Baba Mtakatifu ameishukuru mihimili yote ya utume wa uinjilishaji ndani ya Kanisa mintarafu mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kutambua kwamba, kila Mkristo amepokea karama za Roho Mtakatifu hivyo anatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa wale wote wanaoguswa na mafungamano na upendo wa Kristo Yesu, wanawiwa kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa huruma na upendo wa Kristo Yesu, unaobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu. Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa uinjilishaji anayeleta amani na utulivu kwenye ghasia na mchanganyiko wa mambo. Tarehe 16 Mei 2023, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hii pia ni Siku ya Kuwaombea Mapadre: toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Mwenyezi Mungu amependa kukutana na binadamu wote kwa njia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini wote kuendelea kujiaminisha kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa kusema “Ee Yesu mwenye moyo mpole na mnyenyekevu, ifanye mioyo yetu ifanane na Moyo wako.”

Wajumbe wa mkutano mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimisionari
Wajumbe wa mkutano mkuu wa Mwaka wa Mashirika ya Kimisionari

Baba Mtakatifu anasema, Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kielelezo cha mpango wa Mungu katika ukombozi wa mwanadamu kwani kwa kumtoa Mwanaye wa pekee, ili kila mtu amwaminiye, asipotee, bali awe na uzima wa milele. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya upendo usiokuwa na kifani wa Baba wa milele, mwaliko kwa kushiriki furaha yake isiyokuwa na mwisho; anawasimamisha wale walioteleza na kuanguka, anawafufua kutoka kwa wafu. Na mapenzi ya Baba yake wa mbinguni ni haya ili kwamba wote aliopewa Yesu na Baba yake wasipotee, bali wafufuliwe siku ya mwisho. Kristo Yesu alionesha masikitiko makubwa kwa dhambi zilizotendwa na binadamu, lakini akaonesha huruma, upendo na msamaha kama kielelezo cha Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu, mwaliko kwa mihimili yote ya uinjilishaji kufuata mfano wa Baba mwenye huruma, kama kielelezo na kiini cha utume wa uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa, ili upendo wa Mungu uweze kuwafikia watu wote, bila mtu awaye yote kuachwa nyuma! Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa, kama ambavyo umeshuhudiwa na Mwenyeheri Pauline Marie Jaricot, Muasisi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, na ambaye alikuwa na Ibada ya pekee kabisa kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Utume, Karama na Upyaisho mambo msingi kwa Mashirika haya.
Utume, Karama na Upyaisho mambo msingi kwa Mashirika haya.

Baba Mtakatifu Francisko amekugusia pia Karama ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, kwa nyakati hizi na kwamba, yanapaswa kuwa ni nyenzo muhimu ya uinjilishaji na uwajibikaji wa kimisionari unaotekelezwa na kila mbatizwa pamoja na kuyaenzi Makanisa mapya mahalia, kwa kukuza na kuhamasisha roho ya kimisionari miongoni mwa watu wa Mungu. Kumbe, ni wajibu wao, kumwomba Roho Mtakatifu ili awawezeshe kuhamasisha, kuunda na kujenga ari na mwamko wa kimisionari, ili kila mbatizwa aweze kuwajibika barabara katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kutokana na watu kutopea kwa imani kuna haja tena ya uinjilishaji mpya na wongofu wa kichungaji. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, yasigeuzwe kuwa ni chombo cha kugawa fedha kwani matokeo yake ni mihimili ya uinjilishaji kugeuka na kuanza kumezwa na malimwengu pamoja na rushwa na ufisadi wa mali ya Kanisa.

Ushuhuda wa imani nyenzo muhimu ya Uinjilishaji
Ushuhuda wa imani nyenzo muhimu ya Uinjilishaji

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha matarajio na ndoto za upyaisho wa huduma ya uinjilishaji kwa Kanisa zima. Upyaisho huu unajikita katika mchakato wa umoja na ushirikiano, ili kuwa ni chachu inayosaidia kunogesha ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa kwa kuunga mkono juhudi za matendo ya uinjilishaji: Ili kufanikisha azma hii, kuna haja ya kujenga ushirika na udugu wa kimisionari unaotekelezwa kwa njia ya miundo ya Mabaraza ya Maaskofu na Majimbo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Itakumbukwa kwamba, waasisi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa alikuwa ni Askofu, Padre na Waamini wawili walei, mwaliko wa ushiriki mkamilifu wa watu wote wa Mungu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kimisionari. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wote wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kwa huduma makini kwa watu wa Mungu, licha ya matatizo na magumu wanayokabiliana nayo katika maisha na utume wao, lakini wakisukumwa na moyo pamoja na ari ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, huku wakisindikizwa kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Papa PMS 2023

 

03 June 2023, 15:18