Kumbukizi ya Miaka 145 ya Gazeti la "Il Messaggero": Kanuni Maadili na Jubilei ya Mwaka 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Gazeti la "Il Messaggero" lilianzishwa mjini Roma tarehe 8 Desemba 1878 na Luigi Cesana kutoka Milan, wakati huo akiwa na umri wa miaka ishirini na saba tu na Baldassarre Avanzini kutoka La Spezia, mwanzilishi wa zamani wa Il Fanfulla huko Florence. Matoleo manne ya majaribio yalichapishwa kati ya tarehe 16 na 19 Desemba 1878. Na kwa mwaka 2023 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 145 tangu kuanzishwa kwake. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Dr. Francesco Gaetano Caltagirone, Rais wa Gazeti la "Il Messaggero" pamoja na mambo mengine anakazia kanuni maadili ili kuepuka habari za kughushi, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, maana ya Jubilei pamoja na kuwa ni chemchemi ya matumaini mapya! Baba Mtakatifu Francisko anampongeza Dr. Francesco Gaetano Caltagirone, Rais wa Gazeti la "Il Messaggero" kwa maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 145 tangu kuanzishwa kwake na hivyo kusimulia sura mbalimbali za wananchi wa Italia, kwa kuendelea kutafakari fursa, matatizo na changamoto mbalimbali za Italia na kwamba, Gazeti hili limejipambanua kuwa na nguvu ya uandishi wa habari kwa ajili ya kuwahabarisha walimwengu. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime ili kujielekeza na kujikita zaidi katika kanuni maadili na utu wema, kama sehemu ya mapambano dhidi ya jamii inayoendelea kutopea katika habari za kughushi “fakenews” badala ya kutafuta na kuambata ukweli.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuzinduliwa kwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican imekuwa ni fursa ya maandalizi ya Mwaka wa kwanza wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025. Hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.” Hili ni tukio linalogusa maisha na utume wa Kanisa, mji wa Roma, Bara la Ulaya na Ulimwengu katika ujumla wake. Hii ni fursa ya pekee ya kutangaza na kushuhudi tunu msingi za maisha ya Kikristo, ili kuwasha tena upya moto wa matumaini katika uhalisia wa maisha ya watu wa Roma na kwa mahujaji watakaofika kufanya hija mjini Roma. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jubilei ni kipindi cha kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.
Ni wakati muafaka wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake hata bila mastahili yao. Huu ni muda muafaka wa kupyaisha kanuni maadili na utu wema mintarafu masuala ya kijamii na kitamaduni, tayari kuganga na kuponya madonda ya ukosefu wa haki, kinzani pamoja na mipasuko ya kijamii; tayari kurekebisha ukosefu wa uwiano wa usawa wa kiuchumi, kwa kuondokana na mifumo mbalimbali ya ubaguzi, ili hatimaye, kuwapatia watu wa Mungu imani na matumaini kama sehemu ya mchakato wa ukuaji na maendeleo fungamani ya binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ni fursa ya kujikita katika uhuru katika uelewa wake mpana yaani: uhuru wa kibinadamu na kijumuiya, tayari kutekeleza sera na mikakati itakayoleta ukombozi wa kweli kwa binadamu, miji na Mataifa. Huu ni ukombozi kutoka katika mifumo yote ya ubaguzi wa rangi na mimomonyoko ya maadili na utu wema. Ni vyema pia kufanya tafakari ya kina kuhusu madhara makubwa ya maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 uliowatumbukiza watu wengi katika dimbwi la kifo katika upweke hasi, mambo ambayo yameacha alama za kudumu katika maisha ya watu wengi. Baba Mtakatifu anatoa mwaliko kwa watu wa Mungu kuadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 kwa heshima na taadhima, daima waamini wakijikita katika fadhila ya imani na matumaini kama mwanzo mpya na alama ya upyaisho wa maisha.