Kumbukizi ya miaka 60 ya Waraka wa Kitume wa Amani Duniani, Miaka 60 tangu alipofariki dunia Papa Yohane XXIII na Miaka 60 tangu achaguliwe Papa Paulo VI kuliongoza Kanisa la Kristo Yesu. Kumbukizi ya miaka 60 ya Waraka wa Kitume wa Amani Duniani, Miaka 60 tangu alipofariki dunia Papa Yohane XXIII na Miaka 60 tangu achaguliwe Papa Paulo VI kuliongoza Kanisa la Kristo Yesu.  (Vatican Media)

Kumbukizi ya Miaka 60 ya Amani Duniani; Utume Papa Paulo VI na ya Kifo Cha Yohane XXIII

Papa Francisko Jumamosi tarehe 3 Juni 2023 amekutana na kuzungumza na mahujaji kutoka Jumuiya ya Sotto il Monte na Jumuiya ya Concesio, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 60 tangu Papa Yohane XXIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume wa “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani”, Miaka 60 tangu Papa Yohane XXIIIalipofariki dunia na Miaka 60 tangu Mtakatifu Paulo VI alipochaguliwa kuliongoza Kanisa. Hii ni kazi ya Roho Mtakatifu: ushuhuda, amana na utajiri.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili mambo msingi yanayofafanuliwa katika Waraka wa Kitume wa “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” ambao kwa mwaka 2023, Kanisa linaadhimisha kumbukizi ya miaka 60 tangu Mtakatifu Yohane XXIII alipouchapisha. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanawahimiza Wakristo kwa busara na mapendo, kwa njia ya majadiliano ya kidini, umoja na ushirikiano na waamini wa dini nyingine, kutoa ushuhuda wa imani na wa maisha yao. Mtakatifu Yohane wa XXIII ambaye hapo mwanzoni alijulikana kama Angelo Giuseppe Roncalli alizaliwa tarehe 25 Novemba 1881 na kufariki dunia kunako tarehe 3 Juni 1963. Alibahatika kuliongoza Kanisa Katoliki kuanzia tarehe 28 Oktoba 1958 hadi kifo chake. Mtakatifu Yohane XXIII alikuwa ni mtu mwema na mwenye mvuto na faraja kwa watu wengi Alitangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Mwenyeheri tarehe 3 Septemba 2000 wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo. Ni kiongozi aliyethubutu kuitisha Mtaguo Mkuu wa Pili wa Vatican kuanzia mwaka 1962 hadi mwaka 1965, ili kulipyaisha Kanisa la Kristo na kuendelea kusoma alama za nyakati. Mama Kanisa anamkumbuka kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba, siku ambapo Kanisa lilizindua rasmi Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mtakatifu Yohane XXIII katika maisha na utume wake, alikuwa ni mwanadiplomasia aliyejipambanua kwa kulinda na kutetea misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Alikuwa ni chombo cha majadiliano ya kidini na kiekumene nchini Bulgaria na Uturuki ambako alitekeleza utume wake kama Balozi wa Vatican.

Watakatifu Yohane XXIII na Paulo VI Mashuhuda wa imani tendaji
Watakatifu Yohane XXIII na Paulo VI Mashuhuda wa imani tendaji

Mtakatifu Paulo VI (26 Septemba 1897 hadi 6 Agosti 1978) alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro tarehe 21 Juni 1963. Tarehe 19 Oktoba 2014, Baba Mtakatifu Francisko akamtangaza kuwa ni Mwenyeheri. Na tarehe 14 Oktoba 2018 akatangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Mtakatifu. Ni kiongozi aliyetekeleza utume wake katika mazingira magumu ya Vita Baridi, akajitahidi kuwaganga na kuwafunga watu wa Mungu waliokuwa wamejeruhiwa, kwa haki na huruma. Mama Kanisa anamshukuru Mungu kwa kulipatia Kanisa Mtakatifu Yohane XXIII pamoja na Mtakatifu Paulo VI, walioacha chapa ya utakatifu katika maisha na utume wao kama viongozi wakuu wa Kanisa, mfano bora wa imani. Wameweza kuwa ni watakatifu kwa sababu walikutana na kusindikizana na wachamungu na watu watakatifu, mashuhuda amini wa Habari Njema ya Wokovu; msaada angavu kwa waamini kukua na kukomaa katika imani. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 3 Juni 2023 alipokutana na kuzungumza na mahujaji kutoka Jumuiya ya Sotto il Monte na Jumuiya ya Concesio, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 60 tangu Papa Yohane XXIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume wa “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani”, Miaka 60 tangu Papa Yohane XXIIIalipofariki dunia na Miaka 60 tangu Mtakatifu Paulo VI alipochaguliwa kuliongoza Kanisa.

Mtakatifu Yohane XXIII na Mtakatifu Paulo VI Mfano bora wa kuigwa.
Mtakatifu Yohane XXIII na Mtakatifu Paulo VI Mfano bora wa kuigwa.

Baba Mtakatifu anasema, ni kazi ya Roho Mtakatifu kuzalisha watakatifu, huku wakijenga na kusimika maisha yao katika Kristo Yesu, jiwe kuu la msingi, kiasi cha kuwawezesha waamini wakujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Kumbe, hiki ni kipindi cha kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Huu ni mwaliko kwa waamini kuiga mifano bora ya watakatifu hawa katika safari ya maisha yao, kwa kupenda asili na tunu msingi za Kiinjili; kwa kumpenda Kristo na Kanisa lake. Haya ndiyo mafundisho ya historia na ya Kanisa, amana na utajiri wanaopaswa kuurithisha kwa watoto na vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu amekumbusha kwamba, Mji wa Bergamo na Brescia imeteuliwa kuwa ni miji mikuu ya Utamaduni kwa mwaka 2023 nchini Italia. Utamaduni wa kweli unafumbatwa katika majadiliano, ili kujenga na kudumisha maisha ya udugu wa kibinadamu. Utamaduni unasimikwa katika ukweli, ustawi na maendeleo ya wengi, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni utume unaopaswa kuendelezwa na kudumishwa na wote anasema Baba Mtakatifu Francisko. Amehitimisha hotuba yake kwa kuwaweka mahujaji hawa wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria ili awasaidie kuimarisha: imani, matumaini na mapendo thabiti!

Kumbukizi ya Miaka 60

 

03 June 2023, 15:00