Maadhimisho ya Sinodi XVI ya Maaskofu: Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum Laboris
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yananogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Ni kusikiliza Neno la Mungu, ili kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya waamini. Kusikiliza ni kujenga utamaduni wa kusali pamoja na Neno la Mungu, “Lectio Divina.” Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yamegawanywa sasa katika awamu kuu mbili. Awamu ya kwanza ni kuanzia tarehe 4 hadi 29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili itaadhimishwa Mwezi Oktoba 2024. Lengo ni kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa watu wa Mungu katika ujumla wao kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili. Maadhimisho ya Sinodi ni wakati muafaka wa toba na wongofu wa ndani, kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza, ili hatimaye, kuhamasisha umoja na ushiriki wa watu wa Mungu kutoka katika ngazi mbalimbali za maisha, kama ilivyokuwa kwa Wafuasi wa Emau. Wafuasi hawa baada ya kukutana, kuzungumza na kutembea na Yesu Kristo Mfufuka, walirejea wakiwa wamesheheni furaha, imani na matumaini kedekede, tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Mfufuka aliyewafufua kutoka katika makaburi yao ya kutoamini na kujikatia tamaa. Kwa kukutana na Kristo Mfufuka wakapata nafasi ya kufafanuliwa utimilifu wa Maandiko Matakatifu, Sheria na Unabii na hatimaye, kufahamu kwa kina maana ya Kashfa ya Fumbo la Msalaba.
Ni katika muktadha huu, Jumanne tarehe 20 Juni 2023 Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imechapisha Hati ya Kutendea Kazi “Instrumentum laboris” kwa Maadhimisho ya Awamu ya Kwanza ya Sinodi kuanzia tarehe 4 hadi 29 Oktoba 2023. Hati hii inagusia kuhusu: Kanisa la Kisinodi Uzoefu Muhimu: Sifa za Kanisa la Kisinodi; Mwelekeo wa Maadhimisho ya Kanisa la Kisinodi: Majadiliano na Roho Mtakatifu. Sehemu ya Pili ni: Umoja, Ushiriki na Utume: Vipaumbele vitatu vya Kanisa la Kisinodi. Huu ni umoja unaong’ara, alama na chombo cha ushirika na Mwenyezi Mungu na alama ya umoja kati ya binadamu. Uwajibikaji katika utume na jinsi ya kushirikishana karama katika huduma ya Injili. Ushiriki, utawala na madaraja: Je ni mchakato, miundombinu na taasisi gani zinapaswa kushiriki katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi? Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum laboris ni matunda ya ushiriki mkamilifu wa watu wa Mungu kutoka katika: Majimbo, Mabaraza ya Maaskofu na katika maadhimisho ngazi ya Kimabara, sanjari na maadhimisho yaliyokuwa yakiendeshwa kwa njia ya mitandao ya kijamii na hivyo kubainisha vipaumbele vya Makanisa mahalia vinavyopaswa kufanyiwa kazi kuanzia tarehe 4 – 29 Oktoba 2023. Lengo kuu ni kutekeleza utume wa Mama Kanisa wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ni muda wa kusikiliza kwa makini jinsi ambavyo limeishi na kutekeleza dhamana na utume wake; matatizo na changamoto zinazojitokeza. Changamoto kubwa katika maadhimisho ya Sinodi ni uwezo wa kuratibu kinzani ili ziweze kuwa ni chemchemi ya nguvu mpya ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Huu ni wakati ambapo utambulisho na wito wa Kanisa unajikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi pamoja na kuhakikisha kwamba, matunda yaliyojitokeza yanamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya Jumuiya za waamini sehemu mbalimbali za dunia.
Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum laboris Kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2024. Hapa nyaraka za rejea ni zile zilizozalishwa kwenye maadhimisho ya Sinodi katika ngazi ya Mabara na Taarifa ya Maadhimisho ya Sinodi katika mfumo wa kidigitali. Nyaraka hizi ni muhimu katika kufanya mang’amuzi. Makanisa mahalia yanahimizwa kuendelea kusali, kutafakari na kutenda kama sehemu ya mchango wao katika maadhimisho ya Sinodi kwa Kanisa la Kiulimwengu. Maadhimisho ya Sinodi Awamu ya Kwanza yameliwezesha Kanisa kufahamu umuhimu wa Kanisa mahalia kama sehemu muhimu sana ya rejea ya kitaalimungu, mahali ambapo wabatizwa wanahamasishwa kutembea kwa pamoja na kwamba, Baba Mtakatifu ni kielelezo cha ushirika wa Kanisa katika maadhimisho haya yatakayofanyika katika awamu kuu mbili yaani Oktoba 2023 na Oktoba 2024. Hati ya Kutendea Kazi: Instrumentum Laboris imegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ni kwa ajili ya Kanisa la Kisinodi. Hapa hati hii inabainisha sifa msingi zinazolibainisha Kanisa la Kisinodi pamoja na mchakato wake unaoliwezesha kufanya majadiliano na Roho Mtakatifu. Sehemu ya Pili inajikita katika: Umoja, Ushiriki na Utume; muhimu sana katika majadiliano ya vikundi vidogo vidogo “Circuli minores” na kwamba, nyaraka nyingi za Kanisa kama zile zinazohusu: familia na vijana pamoja na nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican zitahusishwa kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.
Kanisa la Kisinodi Uzoefu Muhimu: Mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ni fursa kwa waamini kukutana katika imani na hivyo kujenga mahusiano na Kristo Yesu, ili kudumisha utamaduni wa udugu wa kibinadamu na upendo kwa Mama Kanisa. Kanisa la Kisinodi linajipambanua kwa kutambua utu, heshima na dhamana inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, inayowafanya wabatizwa kuwa ni watoto wapendwa wa Mungu, wanaounda familia ya Mungu na kwamba, wamempokea Roho Mtakatifu tayari kutekeza utume wa Kanisa unaofumbatwa katika ushirika na utume. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaendelea kujielekeza katika ujenzi wa mifumo, taasisi pamoja na michakato ya uundaji wake. Kanisa la Kisinodi linatamani kujikita katika unyenyekevu na hivyo kuendelea kujifunza kuwa ni chombo cha msamaha. Huu ni ujenzi wa Kanisa linalosikiliza; Kanisa ambalo linajihusisha na ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu na kujadiliana; Kanisa la Kisinodi linalojielekeza katika ujenzi wa umoja wa Kanisa na wala si katika ubinafsi. Hili ni Kanisa linalojipambanua kwa kujikita katika uaminifu pasi na woga; Kanisa linalojitahidi kufahamu kati ya upendo na ukweli. Kanisa la Kisinodi linapaswa kuratibu kinzani na mipasuko mbalimbali bila kunyong’onyeshwa na kinzani hizi na hivyo kujitahidi kuwa ni chombo cha upatanisho. Kanisa la Kisinodi linajikita katika mang’amuzi. Ni kwa njia ya mang’amuzi, Kanisa limekuwa “likipata mang’amuzi mapya katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalopania kukutana na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wale wafuasi wawili wa Emau. Majadiliano na Roho Mtakatifu yanaweza kueleweka kuwa ni sala kwa washiriki wote wa mkutano mkuu, mchakato wa kusikilizana wao kwa wao, ili hatimaye, kuweza kumsikiliza Roho Mtakatifu, ili kuchukua matunda ya kazi ya pamoja, ili hatimaye, kutambua upya wa kazi ya Mungu.
Sehemu ya Pili ni: Umoja, Ushiriki na Utume: Vipaumbele vitatu vya Kanisa la Kisinodi. Ushirika na utume ni chanda na pete kwani vinakamilishana. Kanisa la Kisinodi ni Jumuiya inayong’ara na ni chombo makini cha Mungu na ujenzi wa umoja wa Kanisa. Hii ni changamoto kwa Kanisa kuendelea kujizatiti katika majadiliano ya kiekumene, ili siku moja Kanisa liweze kuwa na umoja kama kielelezo cha utume kwa Injili. Kipaumbele cha kwanza ni Kanisa kutambua kwamba, ni la kisinodi na kimisionari linaloundwa na watu wenye karama na mapaji mbalimbali katika maisha. Kumbe, huu ni umoja unaofumbatwa katika utofauti wao na kwamba, Kanisa linathamini sana mchango wa kila mwamini mbatizwa katika maisha na utume wa Kanisa. Sehemu ya Pili inajikita katika: Umoja, Ushiriki na Utume: Madaraka au uongozi ndani ya Kanisa la Kisinodi ni huduma makini kwa watu wa Mungu. Taasisi na miundombinu peke yake haiwezi kujenga na kudumisha Kanisa la Kisinodi. Kumbe, kuna haja ya kujenga utamaduni na tasaufi ya kisinodi inayofumbwa katika toba na wongofu wa ndani, kwa kuenziwa na majiundo makini yanayojikita katika mwelekeo wa utume, uwezo wa kujenga mahusiano na mafungamano kati ya watu wa Mungu; ujenzi wa jumuiya ya waamini pamoja na utayari wa kusikiliza kwa makini sanjari na kufanya mang’amuzi ya mtu mmoja mmoja na yale ya kijumuiya.
Hili ni Kanisa linalojikita katika mchakato wa udumifu, kwa kujiamini na uhuru wa kuzungumza ukweli “parrhesia.” Hati ya Kutendea Kazi, Instrumentum laboris inakazia umuhimu wa watu wote wa Mungu kupata majiundo ya awali na endelevu ili kutambua maisha na utume wa Kanisa la Kisinodi, ili kupata mang’amuzi mapya ya uongozi ndani ya Kanisa, mchakato wa kufanya maamuzi pamoja na kuisindikiza jumuiya ya waamini katika kufanya mang’amuzi na majadiliano katika Roho Mtakatifu. Majandokasisi hawana budi kuwa na uelewa mpana maisha na mantiki ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Kumbe, uragibishaji wa utamaduni wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unakwenda sanjari na upyaishaji wa mfumo wa elimu na majiundo seminarini, kwa kujielekeza zaidi katika ujenzi wa maisha ya umoja, ushiriki na utume. Malezi na majiundo makini ni kiini cha tasaufi ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaolenga kulipyaisha Kanisa. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na upyaishaji wa lugha inayotumika Kanisani mintarafu: Liturujia ya Kanisa, Mahubiri, Katekesi, Sanaa Takatifu pamoja na mifumo yote ya mawasiliano ya jamii inayowalenga waamini na hadhira kubwa zaidi. Lengo ni kuhakikisha kwamba, amana na utajiri wa Kanisa unawafikia watu wengi zaidi badala ya kuwa ni vikwazo vinavyowaweka mbali. Lugha mpya ya Kanisa haina budi kujikita katika mchakato wa utamadunisho ili kuziinjilisha tamaduni na kuitamadunisha Injili hata katika mfumo wa kidigitali, ili hatimaye, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ufanisi mkubwa, lengo kuu la ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.