Tafuta

Mpango Mkakati wa Dakika Moja kwa ajili ya kuombea amani, ulizinduliwa kwa mara ya kwanza kunako mwaka tarehe 6 Juni 2014 Majira ya Saa 7:00 Mchana. Mpango Mkakati wa Dakika Moja kwa ajili ya kuombea amani, ulizinduliwa kwa mara ya kwanza kunako mwaka tarehe 6 Juni 2014 Majira ya Saa 7:00 Mchana.  (AFP or licensors)

Mpango Mkakati wa 8 Juni 2023 Dakika Moja ya Kuombea Amani

Jukwaa la Kimataifa la Vijana Wakatoliki “Forum Internazionale di Azione Cattolica, FIAC” kupitia mpango mkakati wa tarehe 8 Juni: Dakika Moja ya Amani” linatoa mwaliko kwa watu wote wa Mungu ifikapo saa 7:00 za Mchana, kusimama na kuinamisha vichwa, ili kuombea amani duniani kila mtu kadiri ya Mapokeo ya dini na dhehebu lake. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuunga mkono juhudi za kuombea amani duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili mambo msingi yanayofafanuliwa katika Waraka wa Kitume wa Mtakatifu Yohane XIII “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” ambao kwa Mwaka 2023, Kanisa linafanya kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuchapishwa kwake. Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo fungamani ya binadamu. Ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.  Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha duniani; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani! Tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa limeendelea kuandika na kushuhudia Injili ya amani inayofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika tunu msingi za Kiinjili yaani: haki, upendo, utu na heshima ya binadamu. Hii ni misingi inayopambana na vitendo vyote vya kigaidi, vita na machafuko ya aina mbalimbali ambayo kimsingi ni kashfa kubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Dakika Moja ya Kusimama na Kuombea Amani Duniani
Dakika Moja ya Kusimama na Kuombea Amani Duniani

Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wa Pasaka kwa ajili ya mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake maarufu kama “Urbi et Orbi” kwa Mwaka 2023 alitoa mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inaharakisha kushinda migogoro, kinzani na mipasuko ya kijamii, tayari kufungua nyoyo kwa wale wanaohitaji zaidi. Huu ni mwaliko wa kuharakisha kutembea katika njia ya amani na udugu wa kibinadamu. Haya ni maneno ambayo yanaendelea kujirudia katika nyoyo za wale walio na dhamiri ya kutaka kulinda, kutunza na kudumisha amani duniani. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 7 Juni 2023 amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kwa dakika moja kwa ajili ya kuombea amani duniani, lakini kuombea zaidi mwisho wa vita nchini Ukraine. Jukwaa la Kimataifa la Vijana Wakatoliki “Forum Internazionale di Azione Cattolica, FIAC” kupitia mpango mkakati wa tarehe 8 Juni: Dakika Moja ya Amani” linatoa mwaliko kwa watu wote wa Mungu ifikapo saa 7:00 za Mchana, kusimama na kuinamisha vichwa, ili kuombea amani duniani kila mtu kadiri ya Mapokeo ya dini na dhehebu lake. Ili kufanikisha tendo hili la imani, FIAC inawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kueneza ujumbe huu, ili watu wengi waweze kushiriki kikamilifu kwa ajili ya kuombea amani duniani.

Mpango Mkakati wa Dakika Moja Kwa Ajili ya Kuombea Amani Duniani
Mpango Mkakati wa Dakika Moja Kwa Ajili ya Kuombea Amani Duniani

Mpango Mkakati wa Dakika Moja kwa ajili ya kuombea amani, ulizinduliwa kwa mara ya kwanza kunako tarehe 6 Juni 2014 Majira ya Saa 7:00 Mchana, ili kuunga mkono wito na jitihada za Baba Mtakatifu Francisko za kutafuta na kudumisha amani duniani. Itakumbukwa kwamba, tarehe 8 Juni 2014, Baba Mtakatifu Francisko aliungana na Hayati Simon Peres, Rais wa Israeli na Bwana Mahmoud Abbas -Abu Mazen, Rais wa Mamlaka ya Palestina pamoja na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli kupanda miti ya kumbukumbu ya kuombea amani duniani. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja naye kwa ajili ya kusali na kuombea amani katika Nchi Takatifu. Bado anakumbuka lile tukio la tarehe 8 Juni 2014 alipokutana na kusali pamoja na Patriaki Bartolomeo wa kwanza, Hayati Rais Shimon Peres wa Israeli pamoja na Rais Mahmoud Abbas -Abu Mazen wa Palestina ili kuombea amani huko Mashariki ya Kati! Baba Mtakatifu anasema baadhi ya watu wanaweza kufikiri kwamba, mkutano ule wa sala haukuwa na mafanikio yoyote, lakini hii si kweli, kwani Sala inawasaidia waamini kutokatishwa tamaa na hivyo kushindwa na ubaya, wala matumizi ya nguvu kushika hatamu; badala ya majadiliano na upatanisho. Baba Mtakatifu anawaalika wadau mbalimbali kuongeza juhudi zao katika kukomesha uadui na chuki kati ya watu, ili amani, ustawi na mafao ya wengi yaweze kushika mkondo wake.

Dakika Moja ya Amani
07 June 2023, 14:46