Tafuta

Mtumishi wa Mungu Elisa Martinez, Mwanzilishi wa Shirika la Mabinti wa Bikira Maria wa Leuca “Congregazione delle Figlie di Santa Maria di Leuca” ametangazwa kuwa ni Mwenyeheri. Mtumishi wa Mungu Elisa Martinez, Mwanzilishi wa Shirika la Mabinti wa Bikira Maria wa Leuca “Congregazione delle Figlie di Santa Maria di Leuca” ametangazwa kuwa ni Mwenyeheri.   (Vatican Media)

Mwenyeheri Mama Elisa Martinez: Mfano Bora wa Unyenyekevu na Huduma kwa Maskini na Wagonjwa

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 28 Juni 2023 amesema ni vyema ikiwa kama waamini wataifanya nia ya Mwenyeheri Eliza Martinez kuwa yao, ili kuweza kukumbatia viumbe wote waliotawanyika sehemu mbalimbali za dunia, hasa wahitaji zaidi na wale waliotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Mwenyeheri Eliza Martinez alizaliwa tarehe 25 Machi 1905 na kufariki dunia kunako mwaka 1991 baada ya mafanikio!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwa, jumuiya ya waamini inazaliwa kwa sababu ya utume na umisionari, huku ikisukumwa na Roho Mtakatifu, waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 25 Juni 2023, kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Leuca, Jimbo Katoliki la Leuca, Kusini mwa Italia, amemtangaza Mtumishi wa Mungu Elisa Martinez, Mwanzilishi wa Shirika la Mabinti wa Bikira Maria wa Leuca “Congregazione delle Figlie di Santa Maria di Leuca” kuwa ni Mwenyeheri.

Mwenyeheri Eliza Martinez 1905-1991
Mwenyeheri Eliza Martinez 1905-1991

Mwenyeheri Elisa Martinez alizaliwa tarehe 25 Machi 1905. Kunako mwaka 1930 akajiunga na Shirika la Watawa wa Bibi Yetu wa Upendo wa Mchungaji Mwema “Congregazione delle Suore di Nostra Signora della Carità del Buon Pastore” lakini akalazimika kuachana na maisha ya kitawa kutokana na changamoto za kiafya. Baadaye aliamua kuanzisha Shirika la Mabinti wa Bikira Maria wa Leuca, kwa lengo la kujikita katika utume wa malezi na makuzi ya wasichana; kutoa elimu ya awali na msingi kwa watoto wadogo; huduma kwa wanawake pamoja na utume parokiani. Akafanikiwa kuona Shirika lake likisimika mizizi na kutoa huduma Barani Ulaya, Marekani, Canada, India na Ufilippini. Mwenyeheri Elisa Martinez akaitupa mkono dunia mwaka 1991. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 28 Juni 2023 amesema ni vyema ikiwa kama waamini wataifanya nia ya Mwenyeheri Eliza Martinez kuwa yao, ili kuweza kukumbatia viumbe wote waliotawanyika sehemu mbalimbali za dunia, hasa wahitaji zaidi na wale waliotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Mwenyeheri Eliza Martinez: Unyenyekevu, huduma kwa wagonjwa na maskini
Mwenyeheri Eliza Martinez: Unyenyekevu, huduma kwa wagonjwa na maskini

Kardinali Marcello Semeraro katika mahubiri yake amemtaja Mwenyeheri Elisa Martinez kuwa ni mtawa aliyeyasimika maisha yake katika fadhila ya unyenyekevu, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wagonjwa. Alipenda sana Injili ya Kristo na alikuwa na upendo wa dhati kabisa kwa Bikira Maria, akaendelea kukita maisha yake katika fadhila ya: Imani, matumaini na mapendo na hivyo kuboresha maisha yake kwa mashauri ya Kiinjili yaani: Ufukara, Usafi kamili na Utii. Mwenyeheri Eliza Martinez alifanikiwa kujenga maisha yake ya kiroho katika huduma iliyosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu, kichocheo kikuu cha utakatifu wa maisha. Ngazi kuu za kumwezesha mwamini kufikia utakatifu wa maisha ni: ufukara, unyenyekevu na upendo mkamilifu. Aliwapenda sana maskini kwa sababu wao walikuwa ni ufunuo wa Uso wa Kristo mwingi wa huruma na mapendo. Hata katika shida na mahangaiko yake ya ndani, Mwenyeheri Eliza Martinez alihisi ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu katika safari ya maisha yake. Alitambua kwamba, amani na utulivu wake wa ndani; matumaini na upendo wake kwa Mungu na jirani vilikuwa vinapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kumbe, utakatifu wa maisha ya mwamini unasimikwa katika imani kwa Mwenyezi Mungu, huduma na uaminifu kwa jirani, uvumilivu na udumifu wakati wa majaribu na magumu ya maisha. Hii ni changamoto hata kwa waamini katika ulimwengu mamboleo anasema, Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu.

Mwenyeheri Eliza
28 June 2023, 17:29