Ni mwaka tangu kutumika rasmi Katiba ya Kitume:'Predicate evangelium'
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Katiba ya kitume Praedicate Evangelium ya Sekretarieti Kuu, 'Curia Romana' iliyochapishwa Jumamosi tarehe 19 Machi 2022 na kuanza kutumika rasmi tarehe 5 Juni 2022 imeimetimiza mwaka mmoja. Hati hii inapanga mchakato wa mageuzi yanayotokana na mjadala wa kabla ya mkutano mkuu wa 2013 na ambao tayari umetekelezwa kwa kiasi kikubwa katika miaka kumi sasa iliyopita ya Upapa wa Papa Francisko. Ni andiko linalokita kwa kina na kufanya miongozo ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Kiekuemene wa Vatican, ambao kama madhumuni yake ya awali ulikuwa na jibu la swali kuu kuhusu jinsi gani ya kutangaza Injili katika enzi ya mabadiliko ambayo baadaye yangejidhihirisha, kama Papa Fransisko mara nyingi alivyosisitiza kuwa na mabadiliko ya zama.
Marekebisho hayo yalikuja baada ya yale yaliyoasisiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II ya ‘Pastor Bonus’, 1988, ambayo kwayo ilirekebisha ile iliyotangazwa na Mtakatifu Paulo VI ya ‘Universi depositini Ecclesiae’ ya 1967). Kwa njia hiyo kipaumbele cha Uinjilishaji na nafasi ya waamini walei ni mawazo makuu yanayounganisha Katiba mpya ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.