Tafuta

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Juni inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kusaidia Waathirika wa Utesaji. Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Juni inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kusaidia Waathirika wa Utesaji.  (ANSA)

Tarehe 26 Juni ni Siku ya Kimataifa ya Kusaidia Waathirika Wa Utesaji

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Juni inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kusaidia Waathirika wa Utesaji, iliyoanzishwa tarehe 12 Desemba 1997 na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa ili kusaidia juhudi za Umoja wa Mataifa za kujizatiti katika kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, kwa watu wote na mahali popote pale walipo. Papa anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kukomesha vitendo na hofu ya mateso. Muhimu: Utu, Heshima na Haki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Juni inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kusaidia Waathirika wa Utesaji, iliyoanzishwa tarehe 12 Desemba 1997 na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa ili kusaidia juhudi za Umoja wa Mataifa za kujizatiti katika kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, kwa watu wote na mahali popote pale walipo. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Jumatatu tarehe 26 Juni 2023 anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kupambana hadi kukomesha hofu ya mateso; kwa kutanguliza kwanza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa kujitolea bila kuchelewa kukomesha mateso na kutoa msaada kwa waathirika. Utesaji ni uhalifu chini ya sheria za Kimataifa na kwamba Umoja wa Mataifa unasisitiza kwamba utesaji ni uhalifu chini ya sheria za kimataifa. “Kwa mujibu wa vyombo vyote muhimu, ni marufuku kabisa na hauwezi kuhesabiwa kuwa ni haki kwa hali yoyote.” Marufuku hii ni sehemu ya sheria ya kimila ya kimataifa, ambayo ina maana kwamba inambana kila mwanachama wa jumuiya ya kimataifa, bila kujali kama taifa limeidhinisha mikataba ya kimataifa ambayo mateso yamepigwa marufuku waziwazi. Matendo ya utaratibu au yaliyoenea ya mateso yanajumuisha uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Utesaji ni uhalifu kadiri ya sheria za Umoja wa Mataifa
Utesaji ni uhalifu kadiri ya sheria za Umoja wa Mataifa

Tarehe 12 Desemba 1997, kwa azimio namba 52/149, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilitangaza tarehe 26 Juni kuwa Siku ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa ya Kuwaunga mkono waathirika wa mateso, kwa nia ya kutokomeza kabisa mateso na utekelezaji mzuri wa mkataba dhidi ya mateso na adhabu zingine za ukatili wa mateso, kinyama au wa kudhalilisha. Umoja wa Mataifa unasema tarehe 26 Juni ni fursa ya kutoa wito kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kiraia na watu binafsi kila mahali kuungana na kuunga mkono mamia ya maelfu ya watu duniani kote ambao wamekuwa wahanga wa mateso na wale ambao bado wanateswa hadi leo hii katika ulimwengu mamboleo. Mkataba dhidi ya Mateso na Unyanyasaji au Adhabu Nyingine za Kikatili, Kinyama au Udhalilishaji ulipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 10 Desemba 1984. Ulikamilisha mchakato wa kuweka kanuni za kupambana na utesaji. Kama sehemu ya chombo hiki, bodi ya ufuatiliaji, Kamati dhidi ya Mateso, iliundwa.

26 Juni Ni Siku ya KImataifa kupinga ukatili
26 Juni Ni Siku ya KImataifa kupinga ukatili

Katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kusaidia Waathirika wa Utesaji, Umoja wa Mataifa unataka hatua madhubuti zichukuliwe ili kuhakikisha watesaji wanahukumiwa kutokana na uhalifu huo. Akinukuliwa katika ujumbe wake wa siku hii ambayo huadhimishwa kila mwaka Juni 26, kwa mwaka 2022 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema “Watesaji wasiruhusiwe kamwe kutowajibika kwa uhalifu wao na mifumo ambayo inawawezesha watesaji ni lazima isambaratishwe au kubadilishwa.” Utesaji ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Umoja wa Mataifa unasema mateso yanatafuta kuangamiza utu wa muathiriwa na kukataa utu wa asili wa mwanadamu. Licha ya kupingwa kabisa kwa mateso chini ya sheria za kimataifa, mateso yanaendelea katika maeneo yote ya dunia. “Wasiwasi kuhusu kulinda usalama wa taifa na mipaka unazidi kutumiwa kuruhusu mateso na aina nyingine za ukatili, udhalilishaji na unyanyasaji wa kinyama.” Umeonya Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa matokeo yake ya utesaji huo huenda mbali zaidi ya tendo la pekee kwa mtu binafsi na unaweza kuambukizwa kupitia vizazi na kusababisha mzunguko wa vurugu usiokwisha. Umoja wa Mataifa unalaani mateso tangu awali kuwa ni miongoni mwa vitendo viovu vinavyofanywa na binadamu kwa binadamu wenzao.

Bado kuna watu wanateswa, dhulumiwa na nyanyaswa
Bado kuna watu wanateswa, dhulumiwa na nyanyaswa

Nia za Jumla za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Juni 2023 ni kusali ili kwamba, Jumuiya ya Kimataifa iweze kujizatiti zaidi ili kuhakikisha kuwa, mateso yanakomeshwa na dhamana ya msaada kwa waathirika na familia zao unatolewa. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake unaosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anasema, utesaji ni kati ya madonda yanayoendelea kuuandama ulimwengu mamboleo na wala si matukio ya kihistoria. Baba Mtakatifu anashangaa kuona ukatili umekubuhu kiasi hata cha kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kristo Yesu aliteswa hata akafa Msalabani. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kukomesha vitendo vya utesaji na hivyo kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapewa kipaumbele cha kwanza. Ikumbukwe kwamba, waathirika wa vitendo vya utesaji na ukatili ni binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu. Utesaji na ukatili ni mambo yanayo weza kusababisha vifo au yanaacha madhara makubwa katika maisha ya watu. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha nia zake za jumla kwa Mwezi Juni 2023 kwa kuiombea Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti kikamilifu ili hatimaye, kuweza kukomesha vitendo vya utesaji na ukatili pamoja na kuhakikisha kwamba, waathirika pamoja na familia zao wanapata msaada wa hali na mali.

Waathirika wa utesaji

 

26 June 2023, 15:47