Papa Francisko:Je tunajua kuacha milango wazi,msamaha wa Mungu&furaha ya kiinjili?
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Katika Dominika ya tarehe 4 Mei 2023, Mama Kanisa anaadhimisha Siku Kuu ya Utatu Mtakatifu, ambapo kabla ya sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu ametoa tafakari yake kwa waamini na mahujaji waliounganika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu akianza amesema: “Leo ni siku kuu ya Utatu Mtakatifu, Injili inaleta mazungumzo ya Yesu na Nikodemu (Yh 3,16-18). Nikodemu alikuwa ni mjumbe wa Baraza, aliyekuwa anapenda fumbo la Mungu na hivyo alimjua katika Yesu, Mwalimu wa kimungu na kwa kujificha alikwenda kuzungumza naye. Yesu alimsikiliza, na kutambua kuwa ni mtu anayetafuta na hivyo kwa mara ya kwanza alimshangaza huku akimjibu kwamba ili kuweza kuingia Ufalme wa Mungu lazima kuzaliwa tena; na baadaye aliumfungulia moyo wa fumbo akisema kuwa Mungu aliupenda ubinadamu sana hadi kumtuma Mwanaye katika Ulimwengu. Kwa hiyo Yesu, Mtoto anazungumza nasi kuhusu Baba na upendo wake mkuu.
Baba Mtakatifu akitafakari zaidi kuhusu Baba na Mwana amesema, ni picha ya kifamilia ambayo, ikiwa tunafikiria inaleta sura ya kufikiria ya Mungu. Neno sawa Mungu kiukweli linatushauri uhalisia wa kipekee, aliye mkuu na wa mbali, wakati kwa kusikia Baba na Mwana inatupeleka nyumbani. Ndivyo tunaweza kumfikiria Mungu hivyo, kwa njia ya picha ya familia iliyoungana pamoja mezani, mahali ambapo wanaposhirikishana maisha. Mengineyo ni ile ya chakula, ambayo kwa wakati huo huo ni altare ni alama ambayo baadhi ya picha zinaonesha Utatu. Ni picha ambayo inazungumza nasi kuhusu umoja wa Mungu. Lakini sio tu picha bali ni uhalisia! Ni uhalisia kwa sababu Roho Mtakatifu, Roho ambaye Baba kwa njia ya Yesu alituvuvia katika mioyo yetu (Gal 4,6), anatufanya tuonje, na tuhisi ladha ya uwepo wa Mungu: uwepo karibu, wa huruma na mwororo. Roho Mtakatifu anatufanya sisi kama Yesu na Nikodemu na anatupeleka katika fumbo jipya la kuzaliwa, anatuonesha wazi moyo wa Baba na kutufanya kushiriki maisha yake na Mungu.
Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu amesisitiza kwamba mwaliko ambao tunapewa na ambao tunaweza kusema ni ule wa kukaa mezani na Mungu ili kushirikishana upendo wake. Hicho ndicho kinatokea kila wakati wa Misa, katika Altare ya Ekaristi, mahali ambapo Yesu anajitoa kwa Baba na anajitoa kwa ajili yetu. Ndiyo kwa sababu Mungu wetu ni muungano wa upendo; na ndivyo anavyotuonesha Yesu. Papa ameuliza ni jinsi gani ya kuweza kukaa na kumbu kumbu hiyo? Kwa kujibu ameongeza “Ni kwa ishara rahisi zaidi ambayo tulijifunza tukiwa watoto: Ishara ya Msalaba. Akiendelea amesema kwa kufanya ishara ya msalaba juu ya mwili wetu tunakumbuka ni kwa jinsi gani Mungu alitupenda hadi kutoa maisha yake kwa ajili yetu; na kufikiria sisi wenyewe ambao kwa upendo wake anatuelekeza Kanisa kutoka juu hadi chini, kutoka kushoto hadi kulia, kama mkumbatiao ambao hautuachi kamwe. Na wakati huo huo, anatusindikiza kushuhudia Mungu upendo, kwa kuunda umoja katika jina lake. Papa Francisko katika tafakari hiyo amesema tunaweza kujiuliza leo hii: je sisi tunamshuhudia Mungu upendo? Au Mungu upendo amegeuka kwa mara nyingine kuwa mantiki, kitu ambacho kilishasikika na ambacho hakina mguso na hakichochei tena maisha? Ikiwa Mungu ni upendo, Jumuiya zetu zinamshuhudia? Je Jumuiya zetu zinajua kupenda? Na familia yetu… Je ndani ya Familia zetu tunajua kupenda?
Je tunajua kuacha daima milango wazi na kuwakaribishwa wote, yaani wote kama kaka na dada? Je tunatoa kwa wote chakula cha msamaha wa Mungu na furaha ya kiinjili? Je tunapumua hewa ya nyumbani au tunafanana zaidi na ofisi au mahali ambapo pamehifadhiwa kwa kuingia walioteuliwa? Mungu ni upendo, Mungu ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu na alitoa maisha kwa ajili yetu kwa njia ya msalaba huo, amekazia kusema Papa. Kwa kuhitimisha, amesema na Maria atusaidie kuishi Kanisa kama ile nyumba ambayo inapenda kwa namna ya kifamilia kwa utukufu wa Mungu Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.”