Rais Luiz Lula da Silva wa Brazil Azungumza na Baba Mtakatifu Francisko Kwa Simu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, Jumatano tarehe 31 Mei 2023 amezungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya simu. Kati ya mambo waliyozungumza viongozi hawa wawili ni pamoja na Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, mwezi Oktoba, 2019 yaliyonogeshwa na kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ikolojia fungamani”; Mapambano dhidi ya umaskini unaosigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu; Vita kati ya Ukraine na Urusi pamoja na madhara yake kwa Jumuiya ya Kimataifa na mwishoni, Rais Luiz Inacio Lula da Silva amemwalika Baba Mtakatifu Francisko kutembelea tena Brazil, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo thabiti. Tarehe 24 Februari 2023, Urusi iliivamia Ukraine na huo ukawa ni mwanzo wa vita ya kipuuzi kabisa, ambayo imesababisha mateso makubwa kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Ukraine. Baba Mtakatifu anasema, jambo la kujiuliza ni ikiwa kama kumekuwepo na juhudi za kutosha ili kukomesha vita hii? Si rahisi kuweza kujibu kwamba, diplomasia ya Kimataifa ilitia nia ya dhati kabisa ili kuhakikisha kwamba, vita inakoma, amani inatawala. Hakuna ushindi wa kweli unaojengwa na kusimikwa juu ya vifusi na damu ya watu wasiokuwa na hatia. Takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya wakimbizi milioni 5 wanaokimbia vita na baridi kutoka nchini Ukraine.
Takwimu zinaonesha kwamba, watu zaidi milioni 18 wanahitaji msaada wa dharura na kwamba, watu waliofariki dunia kutokana na vita hiyo kwa sasa wamefikia raia zaidi ya 8, 000 na huku wengine 13, 300 walibaki kuwa ni majeruhi. Katika vita hii isiyokuwa na “macho wala miguu” kuna miji sita imeharibiwa vibaya sana kiasi kwamba, haifai kwa maisha ya binadamu. Kuna majimbo manne ambayo yamejitenga na kuwa ni sehemu ya Urusi. Inakadiriwa kwamba, vita hii imezalisha deni kiasi cha dola bilioni 108, deni la nje, litakalolipwa na Ukraine kwa kipindi cha miaka mingi ijayo. Vita hii imepelekea kupanda zaidi kwa bei ya nishati ya mafuta na hivyo kuibua mnyororo wa kupanda kwa bei za uzalishaji, usafirishaji na ugavi wa bidhaa na huduma. Tatizo kubwa zaidi kiuchumi ni kwamba sasa nchi nyingi zimelazimika kutumia fedha nyingi zaidi za kigeni kuagiza nishati ya mafuta kuliko kawaida na hili limeathiri akiba ya fedha za kigeni ya nchi husika na kupunguza matumizi ya fedha ambazo zingetumika kwenye mambo mengine muhimu. Urusi na Ukraine ni wazalishaji na wasambazaji wakuu wa ngano na mazao mengine ya nafaka duniani. Vita hii imeongeza gharama ya mazao ya nafaka na hivyo kupelekea baadhi ya nchi kukosa uhakika na usalama wa chakula. Nchi zile zilizokuwa zinafanya biashara ya moja kwa moja na Urusi pamoja na Ukraine zinajikuta zikiwa na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na vita kupamba moto. Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, anashauri kuundwa kwa nchi zitakazosaidia kupatikana kwa suluhu ya amani na ametoa shukrani zake za dhati kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa jitihada zake za kutaka kuona kwamba, haki, amani na maridhiano vinatawala nchini Ukraine.
Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, mwezi Oktoba, 2019 yakinogeshwa na kauli mbiu ni: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ikolojia fungamani”; Mapambano dhidi ya umaskini unaosigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa linataka kuwa ni sauti ya kinabii inayojikita katika wongofu wa kichungaji, wongofu wa kiekolojia na wongofu wa kimisionari, ili kuweza kutoka kifua mbele kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa, kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ndiye nguzo kuu ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Maendeleo fungamani ya binadamu yanagusa kimsingi: masuala ya kisiasa, kijamii, kitamaduni na kimazingira. Ni mwaliko wa kujizatiti katika misingi ya haki sanjari na kujenga tasaufi ya utunzaji bora wa mazingira. Kimsingi, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapaswa kuwa ni dira na mwongozo katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Ukanda wa Amazonia. Lengo liwe ni kukabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi katika umoja na mshikamano wa watu wa Mungu, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Ukanda wa Amazonia unaonekana kwa sasa kukabiliwa na mvutano wa Kikanda na Kiulimwengu, kutokana na mvutano huu, Kanisa halina budi kutumia msingi wa Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili hatimaye, liweze kutoa majibu muafaka kwa changamoto changamani zinazoendelea kwenye Ukanda wa Amazonia. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, mwezi Oktoba, 2019 anasema Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil ni kielelezo cha mshikamano na watu wa Mungu nchini Brazil. Ametumia fursa hii kumkaribisha tena Baba Mtakatifu Francisko nchini Brazil, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo thabiti. Mazungumzo haya yanapania kujenga ulimwengu unaosimikwa katika misingi ya haki na udugu wa kibinadamu.