Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.  

Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Misa, Kuabudu na Maandamano ya Ekaristi Takatifu

Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu yanaambatana na Ibada ya Kuabudu na Maandamano ya Ekaristi Takatifu, ushuhuda unaoonesha uwepo endelevu na anagavu wa Kristo Yesu kati ya watu wake. Ekaristi Takatifu ni Fumbo linalopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, kielelezo makini cha imani tendaji! Wuto kwa waamini ni kuwa na ushiriki mkamilifu, ili kupata nguvu, furaha na mwanga wa maisha; wongozo na dira ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia ya Roho Mtakatifu waamini wanafanywa kuwa jamaa moja wale wote wanaoshiriki Mwili na Damu ya Kristo! Ekaristi Takatifu ni chakula cha njiani katika maisha ya Kikristo. Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho ni Sakramenti pacha zinazomwezesha mwamini kuchuchumilia na kuambata upendo na huruma ya Mungu. Ekaristi Takatifu ina uhusiano wa dhati na Sakramenti nyingine za Kanisa. Kumbe, hili ni Fumbo linalopaswa kuadhimishwa kwa ushiriki mkamilifu na heshima kuu kwa kutambua kwamba, Kristo ndiye mhusika mkuu. Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu yanaambatana na Ibada ya Kuabudu na Maandamano ya Ekaristi Takatifu, ushuhuda unaoonesha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake. Ekaristi Takatifu ni Fumbo linalopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, kielelezo makini cha imani tendaji! Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 7 Juni 2023 amewakumbusha waamini kwamba, Sherehe ya Ekaristi Takatifu “Corpus Domini” ni kiini na chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa. Ametoa wito na mwaliko kwa waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu linalowakirimia nguvu, mwanga na furaha ya maisha na hatimaye, kuwa ni chemchemi, dira na mwongozo wa maamuzi makini na matendo katika maisha. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani, chemchemi ya neema, na utukufu wa Mungu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini cha utakatifu wa maisha na utume wa Kanisa.

Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Misa, Kuabudu na Maandamano
Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Misa, Kuabudu na Maandamano

Waamini wanapaswa kujenga utamaduni utakaowawezesha kufanya toba na wongofu wa ndani ili kutambua umuhimu wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu katika maisha yao ya kiroho na ushiriki mkamilifu kwa Fumbo la Ekaristi Takatifu. Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican unabainisha dhamana ya Fumbo la Ekaristi Takatifu katika maisha ya waamini, kwani hili ni Fumbo la Imani, chemchemi ya neema na mwaliko wa kuutakatifuza ubinadamu ndani ya Kristo, kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Utume wa Kanisa unapata chimbuko na hatima yake lake katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Haya yalisemwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI, tarehe 13 Machi, 2009, wakati alipokutana na Wajumbe wa Baraza la Kipapa la Ibada na Sakramenti za Kanisa, baada ya kuhitimisha mkutano wao wa mwaka, ulionogeshwa na kauli mbiu: Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kujichotea utajiri mkubwa wa Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa njia ya Ibada ya Misa Takatifu na ile ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Kristo Yesu katika maumbo ya mkate na divai anajitoa kikamilifu kuwa ni chakula na kinywaji kinachozima kiu ya maisha ya kiroho. Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu ni tendo la upendo kwa Kristo Yesu, linalomuunganisha mwamini na Kristo Yesu ambaye ni kichwa cha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, na hivyo kuonja uwepo wa Mungu kati ya waja wake. Muungano huu ulete mabadiliko ya toba na wongofu wa ndani kwa kuondokana na matumizi ya nguvu na badala yake kujenga misingi ya upendo; kifo na kuwa na matumaini ya maisha. Ni mabadiliko yanayogusa undani wa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Waamini wajenge utamaduni wa ushiriki mkamilifu katika Misa.
Waamini wajenge utamaduni wa ushiriki mkamilifu katika Misa.

Baba Mtakatifu Benedikto XVI anawaalika waamini kulifahamu kwa undani zaidi Fumbo la Ekaristi Takatifu, wakijitahidi kuwa waaminifu kwa Mapokeo hai ya Kanisa, hali inayohitaji majiundo endelevu miongoni mwa watu wa Mungu, ili kukoleza ari, mwamko na moyo wa Ibada kwa Ekaristi Takatifu. Kwa macho ya kibinadamu anasema Mtakatifu Toma wa Akwino, huwezi kuona kitu, lakini kwa jicho la imani, mwamini anamwona Mungu katika maumbo ya Mkate na Divai. Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu iwasaidie waamini kujiandaa vyema kwa maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, sala na matendo ya huruma kwa wahitaji zaidi, bila kusahau kufunga. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kurutubisha katika maisha yao upendo kwa Mungu na jirani. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni sehemu ya Utamaduni na Mapokeo ya Kanisa kama ushuhuda wa Injili ya furaha na imani kwa Kristo Yesu anayeendelea kubaki kati ya waja wake kwa njia ya Fumbo la Ekaristi takatifu. Waamini wanahamasishwa kujiandaa kikamilifu ili hatimaye, kuweza kuadhimisha Fumbo hili la imani linalopaswa kumwilishwa katika familia na Jumuiya za Kikristo kwa kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ushiriki mkamilifu katika Ibada ya Misa takatifu na tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika ushuhuda wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu ni fursa ya kukutana na Kristo katika Neno la Meza ya huruma, upendo na huduma.

Mchako wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Mchako wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Waamini wanaposhiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu wamwachie nafasi Kristo ili aweze kuwamegea huruma na upendo wake kwa njia ya Neno na hatimaye, wokovu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni ushuhuda wa uwepo angavu na endelevu wa Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu anayetembea na waja wake hadi utimilifu wa dahali. Uwepo wake unafichika katika maumbo ya Mkate na Divai; Sakramenti ya Upendo na chakula safi cha wasafiri kuelekea mbinguni kwa Baba. Ekaristi Takatifu ni chachu ya huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Uwepo wa Yesu katika Tabernakulo ni kielelezo cha mwanga angavu na uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo linaloendelea kuboreshwa kwa njia ya: unyenyekevu wa moyo, sala na upendo unaopyaishwa na kufumbatwa kwenye Jumuiya za Kikristo zilizotakaswa kwa Damu Azizi ya Kristo. Kanisa linalojikita katika Ekaristi, hili ni Kanisa la kimisionari na sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalotumwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya watu! Waamini wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upendo unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa kushuhudia kile walichoona na kusikia, kwa kuwatangazia wengine, ili wao pia waweze kushiriki na hatimaye, kufumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Corpus Domini 2023

 

11 June 2023, 10:18