Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu: Siku ya Kuombea Toba, Wongofu wa Mapadre
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kama sehemu ya maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu sanjari na Siku ya Kuombea toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha ya Mapadre, tarehe 16 Juni 2023, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Kristo Yesu ili aifanye mioyo yao iweze kufanana na Moyo wake Mtakatifu, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya kutenda mema kwa watu wote. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 25 Machi 1995 alianzisha Siku ya Kuombea Toba, Wongofu na Utakatifu wa Maisha ya Mapadre. Siku hii ya sala inaakisi pia utakatifu wa watu wa Mungu, ambao kimsingi Mapadre wanawekwa wakfu kwa ajili ya kuwatumikia. Kwa njia ya Ubatizo wabatizwa hushiriki ukuhani wa Kristo Yesu; Utume wake wa kinabii na wa kifalme, kumbe Mapadre katika ukuhani wao wa huduma wanatekeleza kwa uhuru na furaha kubwa wito wa utakatifu wa watu wote wa Mungu. Kuna uhusiano mkubwa kati ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu na Siku ya Kuombea Toba, Wongofu na Utakatifu wa Maisha ya Kipadre, kwani huu ni mwaliko wa kurejea tena kufanya tafakari juu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kwa kuegemea kifuani pa Kristo Yesu, ili kuweza kujichotea neema, huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu uliotobolewa na ukabaki wazi, chemchemi ya Sakramenti za Kanisa. Hii inawasaidia Mapadre kugundua tena ule uzuri wa Sakramenti ya Daraja Takatifu, zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tayari kuipyaisha.
Utakatifu wa Mapadre una uhusiano wa karibu sana na utume wa kuwasindikiza watu wa Mungu waliokabidhiwa kwao, huku wakishirikishana: furaha na matumaini; mateso na machungu ya maisha. Kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, Padre anajifunza kuwapenda ndugu zake katika Kristo Yesu; anajifunza kutembea nao bega kwa bega huku wakikabiliana na changamoto za utakatifu wa maisha, daima wakijielekeza katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Katika Moyo Mtakatifu wa Yesu uliotobolewa kwa mkuki, Padre anatambua kwamba, kwa hakika anapendwa na Mwenyezi Mungu na ametakatifuzwa na Roho Mtakatifu na hivyo anajifunza daima kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Maadhimisho haya ya kila mwaka ni mwaliko kwa Makanisa mahalia kuadhimisha Sherehe hii kwa kujikita katika sala, ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kulipatia Kanisa lake wachungaji wema na watakatifu kadiri ya Moyo wake Mtakatifu. Katika mapambazuko ya kipindi kipya cha maisha na utume wa Kanisa, Mapadre wanahimizwa na kualikwa kutafakari jinsi ya kuuishi utume wao, kwa kuendelea kugundua zawadi ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwanza kabisa kwa kushirikishana Neno la Mungu; kwa kuwani vyombo na mashuhuda wa kweli wa furaha inayobubujika kutoka katika imani; tayari kumtangaza na kumshuhudia Mwenyezi Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao! Je, watu wanawasikiliza kwa makini na kuona ndani mwao uwepo wa Mungu anayetaka kukutana na waja wake.
Mwenyezi Mungu anaishi na kutenda katika Jumuiya mbalimbli za Kikristo na katika maisha ya ushirika. Mwenyezi Mungu anaonekana, anatangazwa na kushuhudiwa katika Sakramenti za Kanisa na katika ushuhuda wa maisha ya Mapadre na waamini walei. Huu ni mwaliko kwa wachungaji na watu wa Mungu katika ujumla wao, kugundua ndani mwao utambulisho na uwepo wao ndani ya Kanisa, tayari kuyapyaisha maisha yao yanayosimikwa katika imani, jambo muhimu sana kwa jumuiiya inayosali na kusikiliza kwa makini Neno la Mungu, huku wakimwendea Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anakazia msingi wa maisha na utume wa Kipadre katika ulimwengu mamboleo kwa kujikita katika mambo makuu manne yanayoonesha ukaribu wa Mungu kwa waja wake, kwa sababu Mwenyezi Mungu daima anataka kuonesha ukaribu wake, mwaliko kwa Mapadre kujenga na kudumisha ukaribu huu ili waweze kujichotea baraka, neema na rehama katika maisha na utume wao. Uwepo wa ukaribu wa Askofu, ili kutekeleza utii, Padre anahamasishwa kujenga utamaduni wa kusikiliza, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu kwa njia ya sanaa ya mang’amuzi. Ukaribu kati ya Mapadre unamwilishwa kwa njia ya udugu wa kibinadamu unaofukuzia mbali upweke hasi na tabia ya kutoguswa na mahangaiko ya wengine. Ukaribu wa watu wa Mungu hauna budi kuonekana kama neema na baraka. Waamini wanahimizwa kusali na kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Hii ni miito ya Kipadre na Maisha ya kuwekwa wakfu kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu uwe ni ushuhuda wa maisha ya utakatifu, vyombo na mashuhuda wa furaha ya upendo wa Baba wa milele na wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, unaosheheni upendo na huruma kwa kila kiumbe. Huu ni mwaliko wa kusali na kumwaombea mapadre ndani ya Kanisa.