Katika Ibada hii, Baba Mtakatifu Francisko atabariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu wapya 32 walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2022-2023. Katika Ibada hii, Baba Mtakatifu Francisko atabariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu wapya 32 walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2022-2023.   (Vatican Media)

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume na Miamba wa Imani

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na miamba ya imani, Alhamisi tarehe 29 Juni 2023 anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, atabariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu wapya 32 walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2022-2023. Kutoka Barani Afrika ni: Askofu mkuu João Carlos Hatoa Nunes na Askofu mkuu Jean de Dieu Raoeli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na miamba ya imani, Alhamisi tarehe 29 Juni 2023 anatarajia kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 3:30 asubuhi kwa Saa za Ulaya. Katika Ibada hii, atabariki Pallio Takatifu watakazovishwa Maaskofu wakuu wapya 32 walioteuliwa katika Kipindi cha Mwaka 2022-2023. Kutoka Barani Afrika Maaskofu wakuu hao ni: Askofu mkuu João Carlos Hatoa Nunes wa Jimbo kuu Maputo Msumbiji pamoja na Askofu mkuu Jean de Dieu Raoelison wa Jimbo kuu la Antananarivo, Madagascar. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu João Carlos Hatoa Nunes alizaliwa tarehe 8 Machi 1968 Jimbo kuu la Beira, Msumbiji. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 17 Julai 1995 akapewa Daraja takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo kuu la Maputo, Msumbiji. Tarehe 25 Mei 2011, Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Maputo na kuwekwa wakfu ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu tarehe 10 Julai 2011. Tarehe 12 Januari hadi tarehe 29 Juni 2012 akateuliwa na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo kuu la Beira. Ilikuwa ni tarehe 2 Januari 2017 alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Chimoio, nchini Msumbiji. Tarehe 15 Novemba 2022, Baba Mtakatifu Francisko akamteua Askofu mkuu João Carlos Hatoa Nunes kuwa Askofu mkuu Mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Maputo, Msumbiji. Na tarehe 5 Mei 2023 Askofu mkuu João Carlos Hatoa Nunes akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Maputo, Msumbiji.

Papa atabariki Palio takatifu wanazovikwa maaskofu wa majimbo makuu
Papa atabariki Palio takatifu wanazovikwa maaskofu wa majimbo makuu

Askofu mkuu Jean de Dieu Raoelison wa Jimbo kuu la Antananarivo, Madagascar alizaliwa tarehe 31 Julai 1963 huko Arivonimamo. Akapewa daraja Takatifu ya Upadre 7 Septemba 1996. Tarehe 25 Machi 2010 Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Antananarivo nchini Madagascar na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 13 Juni 2010. Tarehe 11 Aprili 2015 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Ambatondrazaka, nchini Madagascar. Ilipogota tarehe 5 Juni 2023 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Antananarivo. Pallio takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa kwa manyoya ya kondoo wachanga; na kinavaliwa na Baba Mtakatifu pamoja na Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki pamoja na Mapatriaki wa Makanisa ya Mashariki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, hata Maaskofu wakuu wanahamasishwa kuwabeba kondoo wao kama kielelezo cha wachungaji wema; wakumbuke kwamba, wameteuliwa si kwa ajili ya mafao yao binafsi, bali kwa ajili ya kondoo wa Kristo Yesu. Maaskofu wakuu wapya wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Maaskofu wakuu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume kwa mwaka 2019 alikazia mambo makuu matatu: Mitume hawa walikuwa ni mashuhuda wa maisha, msamaha na mashahidi wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Kristo Yesu ni Mchungaji mwema walio wake wanaisikia sauti yake.
Kristo Yesu ni Mchungaji mwema walio wake wanaisikia sauti yake.

Ni Mitume waliojisadaka kutangaza, kushuhudia na kuishi utume wao, hija ambayo imewafikisha hadi Roma, na hapa wakayamimina maisha, kielelezo makini cha ushuhuda kwa Kristo Yesu, maisha na msamaha! Mitume Petro na Paulo walikuwa ni mashuhuda wa maisha ambayo yalisimikwa katika maisha ya kiroho kwani walikuwa ni wachamungu! Ni watu ambao walionesha udhaifu mkubwa wa kibinadamu, kiasi hata cha Mtakatifu Petro kumkana Kristo Yesu mara tatu wakati ambapo Mtume Paulo alilidhulumu Kanisa la Kristo. Lakini wote hawa wakaoneshwa na kuonjeshwa upendo wa Kristo hasa pale Yesu alipomuuliza Mtume Petro mara tatu, ikiwa kama alikuwa anampenda, Petro akasononeka sana. Mtume Paulo akaulizwa kwanini alikuwa analidhulumu Kanisa lake? Wote wawili waliitwa kwa majina yao, hali ambayo iliwaletea toba na wongofu wa ndani. Hawa ni wadhambi wawili waliotubu na kumwongokea Mungu; ni watu ambao walitambua kwamba ni wadhambi na Yesu akachukua fursa hii kuwafanyia miujiza, kielelezo cha upendo wake, kwa wale wote wanaothubutu kumfungulia hazina ya nyoyo zao, kwa kujiweka mbele ya Kristo, ili aweze kuwatumia kama vyombo na mashuhuda wake. Ni watu walioonesha moyo wa unyenyekevu hadi dakika ya mwisho wa maisha yao, kiasi hata cha Mtume Petro kusulubiwa miguu juu, kichwa chini! Baba Mtakatifu anafafanua kwa kusema, jina Paulo maana yake ni “mtu mdogo”, kielelezo cha unyenyekevu uliomfanya hata watu kusahau jina lake la asili, Saulo, aliyekuwa Mfalme wa kwanza wa Israeli.

Maaskofu wakuu 32 kupewa Pallio Takatifu
Maaskofu wakuu 32 kupewa Pallio Takatifu

Mitume hawa wakatambua kwamba, utakatifu wa maisha unafumbwa katika unyenyekevu, kwa kutambua na kukiri udhaifu na umaskini wao, kiasi cha kujiaminisha kwa Kristo Yesu, aliyewatendea miujiza kwa kuwanyanyua juu, kwa njia ya Msamaha unaoganga na kuponya! Mitume Petro na Paulo ni mashuhuda wa msamaha wa Kristo Yesu, uliowajalia toba na wongofu wa ndani, wakabahatika kuwa watu wapya, wenye furaha na amani ya ndani. Wakasahau ya kale na kuanza kuyaambata maisha mapya yaliokuwa yameboreshwa kwa upendo wa Kristo uliokuwa na nguvu kubwa kupita hata mapungufu na makosa yao ya kibinadamu. Huruma ya Mungu inawajalia waamini kuwa na maisha mapya, changamoto na mwaliko kwa waamini kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho katika maisha yao! Mitume Petro na Paulo walikuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka; mashuhuda wa msamaha unaoganga na kuponya na hatimaye, wakawa ni mashuhuda wa Masiha, Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Kristo Yesu ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, nyakati zote ni zake; chemchemi ya upendo wa kweli. Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni ushuhuda unaobubujika kutokana na Mtume Petro kukutana na Kristo Yesu katika maisha yake kama ilivyokuwa hata kwa Mtume Paulo anayelitaja jina la Kristo Yesu mara 400 katika nyaraka zake mbalimbali. Kwa Mtume Paulo, Kristo kwake ni nguzo ya maisha, kiasi kwamba, mambo yale yaliyokuwa faida kwake akayahesabu kuwa ni hasara kwa ajili ya Kristo!

Watakatifu Petro na Paulo miamba ya imani.
Watakatifu Petro na Paulo miamba ya imani.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, kuwaangalia Mashuhuda hawa wa imani, ili kupyaisha maisha yao, hatimaye, waweze kumfahamu Kristo Yesu kutoka katika undani wa maisha yao na wala wasikomee tu kwa yale yanayoandikwa kwenye mitandao ya kijamii au kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii, ili kweli Kristo Yesu aweze kuwa ni nguzo ya maisha yao, tayari kuwasamehe, ili kuanza kuandika ukurasa mpya wa maisha, kiasi hata cha kuwa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda hai wa Kristo Yesu katika ulimwengu mamboleo. Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani yanahudhuriwa pia na ujumbe kutoka kwa Patriaki Bartholomeo wa kwanza wa Kanisa la Costantinopol wamwendelezo wa mapokeo kwa Makanisa haya mawili. Hii ni changamoto ya kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene ili kuweza hatimaye, kufikia umoja kamili katika ngazi zote. Kwa sababu, wote wakiwa wamepatanishwa na Mwenyezi Mungu na kusamehewa dhambi zao; wanaitwa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao yenye mvuto na mashiko!

Pallio Takatifu
27 June 2023, 15:49