Siku ya Wazazi Ulimwenguni, Tarehe 1 Juni 2023: Dhamana na Wajibu wa Wazazi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jumuiya ya Kimataifa tarehe Mosi Juni ya kila mwaka inaadhimisha Siku ya Wazazi Ulimwenguni, iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2012, ikiwa na lengo la kuwasaidia wazazi kutafakari kwa kina na mapana juu ya dhamana na wajibu wao wa elimu, malezi na makuzi ya watoto wao. Mkazo zaidi umewekwa katika utunzaji bora wa watoto, ulinzi na usalama pamoja na elimu bora na makini kwa watoto, ili kuwawezesha watoto kupata malezi na makuzi bora. Ni katika muktadha wa maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anawataka wazazi kamwe wasichoke kuzungumzia kuhusu imani yao kwa watoto wao, wawe na nguvu ya kuwa wapatanishi wa imani waliyorithi kutoka kwa wazazi wao. Tunakumbushwa kwamba, familia ni tabernakulo ya uhai wa mwanadamu ni mahali ambapo watoto wanarithishwa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kitamaduni. Ni shule ya malezi na makuzi bora; mahali pa kujifunza kusamehe na kusamehewa, kupenda na kupendwa. Familia ni kitalu cha haki, amani na upatanisho wa kweli; mahali ambapo watu wanajifunza kutaabikiana na kusumbukiana kwa hali na mali. Ni mahali muafaka pa kujifunza maisha ya Kisakramenti, Tafakari ya Neno la Mungu na kuhakikisha kwamba, kweli imani inamwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Katika familia za Kikristo, baba na mama wanapaswa kuonesha upendo wa dhati, kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia inayoambata Injili ya uhai, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayokwenda sanjari na malezi pamoja na makuzi ya watoto. Ni wajibu wa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanawafunda watoto wao katika maisha ya sala, kwa njia ya mifano na ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, ili waweze kuvuta neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika maisha yao.
Dhamana na utume wa familia ya Kikristo unajikita katika malezi, ambayo kimsingi ni shule ya kumfuasa Kristo Yesu. Familia ni kikolezo cha Uinjilishaji wa kina kwani kwa kujiinjilisha yenyewe inashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji. Wazazi ni mashuhuda wa kwanza wa Injili ya Kristo. Watoto wanapaswa kusaidiwa kukua na kuimarika katika fadhila mbalimbali za Kikristo kwa njia ya mshikamano wa umoja, upendo, udugu wa kibinadamu na msamaha unaojikita katika maisha ya wazazi wenyewe. Watoto wajengewe utamaduni wa kushiriki katika sala, tafakari na maisha ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ili kuwasaidia kumwilisha imani katika matendo tangu wakiwa wadogo. Changamoto kubwa inayowakabili wazazi na walezi katika ulimwengu mamboleo ni kutokana na pilika pilika za malimwengu kiasi kwamba, wakati mwingine wazazi hawana nafasi hata kidogo ya kukaa na watoto wao. Watoto nao kutokana na majukumu mbalimbali wanajikuta kwamba, wanapata muda kidogo sana wa kukutana na kuzungumza na wazazi wao. Kumbe, hapa kuna haja ya kuweka uhusiano mwema kati ya maisha ya kiroho na maisha ya kijamii, ili watoto waweze kuwa na malezi pamoja na makuzi bora: kiroho, kiutu, kijamii na kimataduni. Mambo yote haya ni muhimu katika ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili.
Wataalamu wa masuala ya malezi wanabainisha kwamba, kuna aina nne za malezi na makuzi ya watoto na zote hizi zina athari zake kwa watoto. Kuna malezi ya kimabavu, hapa wazazi hutumia adhabu kali kuliko kuonya na matokeo yake ni watoto kutojiamini. Malezi ya mamlaka, au demokrasia ni malezi yanayotoa nafasi kwa watoto kukabiliana na matatizo na changamoto za maisha ili kuwajenga na kuwakomaza watoto hawa katika makuzi yao. Watoto kama hawa mara nyngi hujawa na furaha na kuwa na mafanikio katika maisha. Malezi Huru: Wazazi wenye malezi huru ni wavumilivu, na hawawafuatilii watoto wao sana. Huingilia na kuonekana pale tu panapojitokeza tatizo kubwa dhidi ya watoto wao. Wazazi hawa hawawajibishi watoto wao kwa wakati na ikitokea kuwawajibisha hufanya hivyo mara chache zaidi. Hutoa msamaha zaidi na huamini “mtoto ni mtoto tu” wanapowawajibisha watoto mara nyingi hutoa msamaha pale mtoto anapoomba msamaha na kuahidi kubadili tabia. Wazazi hawa huchukua nafasi na jukumu la rafiki zaidi kuliko nafasi na jukumu la mzazi. Huwashawishi watoto wazungumze matatizo yao, lakini hawafanyi juhudi kubwa kukemea tabia na maamzi yasiyo sahihi ya watoto wao. Hawakemei tabia nyingi mbovu za watoto wao. Malezi huria: Wazazi hawatumii nguvu nyingi kutafta mahitaji ya watoto wao. Wakati mwingine wazazi hawa, hawafahamu juu ya maendeleo ya watoto wao. Mara nyingi wazazi hujikita kutatua shida nyingine tu na mahitaji ya nyumbani. Wazazi hawana ufahamu wa kutosha juu ya wanachofanya watoto wao. Wazazi huweka sheria na miongozo michache tu. Hakuna msisitizo wa kutosha katika kuwaelekeza watoto wao, kuwaongoza na kuwajali. Watoto waliokulia katika malezi huria, huwa hawana ufaulu mzuri darasani, wala hawajiamini. Watoto hawa hukumbwa na matatizo mengi ya kinidhamu na huwa hawana furaha.