Tafuta

Tuzo ya Kimataifa ya Biagio Agnes 2023 inatolewa kwa ushirikiano wa RAI na “Confindustria” chemchemi ya matumaini. Tuzo ya Kimataifa ya Biagio Agnes 2023 inatolewa kwa ushirikiano wa RAI na “Confindustria” chemchemi ya matumaini.   (Vatican Media)

Tuzo ya Uandishi wa Habari Kimataifa ya Biagio Agnes Kwa Mwaka 2023: Kanuni Maadili

Baba Mtakatifu Francisko ameonesha "vipengele" vitatu vya kazi ya uandishi wa habari, ambayo labda hutumiwa kidogo sana lakini ambavyo bado vina mengi ya kuwafunda: daftari, kalamu na kutazama. Papa anakazia umuhimu wa waandishi wa habari kuchakarika kutafuta habari, kwa kusikiliza na kukutana na watu ili kutoa simulizi linaojikita katika ukweli, linalohitaji mwandishi wa habari kupiga moyo konde, ili kwenda mahali ambapo hakuna mtu anayetaka kwenda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tuzo ya Uandishi wa Habari Kimataifa ya Biagio Agnes kwa mwaka 2023, hutolewa kwa waandishi bora wa habari waliojipambanua kwenye tasnia ya mawasiliano ya jamii. Sherehe ya ufunguzi wa tuzo hii ilikuwa ni tarehe 23 Juni 2023 huko Campidoglio na tarehe 4 Julai kwenye Makao makuu ya Kituo cha Televisheni cha Taifa, Rai. Tuzo za taasisi za Ulaya zitakusanywa na Bwana Roberta Metsola, Rais wa Bunge la Umoja wa Ulaya, EU. Biagio Agnes ni mwandishi wa habari mahiri kutoka nchini Italia aliyetekeleza dhamana na utume wake kwenye Kituo cha Televisheni cha Taifa, RAI, akajipambanua kuwa ni mtetezi wa huduma hii msingi kwa jamii, akatumia hekima na busara katika kufanya maamuzi yake, ili kuhakikisha kwamba, jamii inapata habari ya kweli na sahihi. Tuzo ya Kimataifa ya Biagio Agnes 2023 inatolewa kwa ushirikiano wa RAI na “Confindustria” chemchemi ya matumaini. Itakumbukwa kwamba, “Confindustria” ni Chama kikuu kinachowakilisha makampuni ya uzalishaji na huduma nchini Italia, chenye wanachama wa hiari wa zaidi ya makampuni 150,000 yanayoajiri wafanyakazi 5,383,286. “Confindustria” ni kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiraia nchini Italia. Kwa kuwakilisha makampuni na maadili yao katika taasisi za ngazi zote, “Confindustria” inachangia katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini Italia pamoja na kuhakikisha kwamba, uzalishaji na huduma zinatolewa kwa ufanisi mkubwa. Ni katika muktadha huu wa Tuzo ya Kimataifa ya Biagio Agnes kwa mwaka 2023, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 24 juni 2023 alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Tuzo ya Uandishi wa Habari Kimataifa ya Biagio Agnes 2023 ambayo kwa mwaka 2023 imefikia awamu ya kumi na tano.

Tuzo ya uandishi wa habari kimataifa ya Biagio Agnes
Tuzo ya uandishi wa habari kimataifa ya Biagio Agnes

Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko alikazia mambo yafuatayo: Kwa kuonesha "vipengele" vitatu vya kazi ya uandishi wa habari, ambayo labda hutumiwa kidogo sana lakini ambavyo bado vina mengi ya kuifunda jamii: daftari, kalamu na kutazama. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa waandishi wa habari kuchakarika kutafuta habari, kwa kuwasikiliza watu wanaokutana nao ili kutoa simulizi linaojikita katika ukweli, jambo ambalo linahitaji mwandishi wa habari kupiga moyo konde, ili kwenda mahali ambapo hakuna mtu anayetaka kwenda huko kama sehemu ya harakati ya kuona; kwa njia ya udadisi, uwazi na shauku. Daftari: Kuandika ukweli daima kunahusisha kazi kubwa ya ndani, huu ni ushuhuda wa moja kwa moja au kwa kutoka katika chanzo kinacho aminika na kutegemewa, kisha kuna kufungua uthibitisho unaofuata. Daftari linawakumbusha waandishi wa habari umuhimu wa kusikiliza na kufadhaika na kile kinachotendeka, ili kupata athari zake kwa kushiriki kwa njia ya huruma. Bado kalamu inasaidia kufafanua mawazo, kuunganisha kichwa na mikono kwa kuunganisha kumbukumbu zilizoko. Kalamu huchochea ufundi ambao mwandishi wa habari anaalikwa kuwa nao, ili kuangalia, kuchunguza mawazo ili hatimaye kujenga upya kwa kuthibitisha hatua iliyofikiwa. Katika muundo huu, akili na dhamiri hutenda pamoja na hivyo kugusa masharti yao ya uwepo. Kwa hivyo kalamu inakumbusha "tendo la ubunifu" la waandishi wa habari na waendeshaji wa vyombo vya mawasiliano ya jamii, kitendo ambacho kinahitaji kuchanganya utafutaji wa ukweli, uadilifu na heshima kwa watu, hasa kwa heshima ya maadili ya kitaaluma, kama vile Biagio Agnes alivyofanya katika huduma yake kama mwandishi wa habari.

Waandishi wa habari: madaraja ya kuwakutanisha watu
Waandishi wa habari: madaraja ya kuwakutanisha watu

Baba Mtakatifu anakaza kusema: Kutazama: Daftari na kalamu ni vifaa rahisi ikiwa hakuna macho juu ya ukweli. Mwonekano wa kweli, sio tu wa kawaida. Leo, zaidi ya hapo awali, jamii inaweza kukengeushwa kwa maneno, picha na jumbe zinazochafua maisha ya watu kama vile habari za uongo, maneno ya kivita au maneno yanayo jaribu kupindisha ukweli. Hapa kuna umuhimu wa kuwapokonya watu silaha za lugha ili kukuza na kudumisha majadiliano, jambo linalohitaji hisia za uwajibikaji unaotekelezwa na wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, ili waweze kutekeleza dhamana na taaluma yao kama sehemu muhimu sana ya utume wao. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewataka wajumbe wa Tuzo ya Uandishi wa Habari Kimataifa ya Biagio Agnes kwa mwaka 2023, kukupaza sera na mipango ya kitamaduni, ili kusaidia mchakato wa usambazaji wa taarifa sahihi, kuelimisha umma pamoja na kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya. Amewapongeza tena washindi wa Tuzo ya Uandishi wa Habari Kimataifa ya Biagio.

Tuzo Biagio Agnes

 

 

25 June 2023, 14:52