“Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya imani na baadae kwa kunizawadia neema ya kumtumikia na kuwatumikia watu kama mchungaji sasa hilo aliloliweka ndani mwaka likue kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. “Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya imani na baadae kwa kunizawadia neema ya kumtumikia na kuwatumikia watu kama mchungaji sasa hilo aliloliweka ndani mwaka likue kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.  (Vatican Media)

Kardinali Mteule Protase Rugambwa: Imani, Huduma na Ujenzi wa Ufalme wa Mungu

Kardinali Protase R. “Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya imani na baadae kwa kunizawadia neema ya kumtumikia na kuwatumikia watu kama mchungaji na ninaomba sasa hilo aliloliweka ndani mwangu liendelee kukua na daima kwa ajili ya kuujenga ufalme wake. Pamoja na wote waaminio na wenye mapenzi mema naamini kabisa kuwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu tutaweza kuyafanya mapenzi yake Mungu, ahimidiwe, tumtukuze na tumsifu milele."

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 9 Julai 2023 amewateuwa Makardinali wapya 21 kati yao Makardinali watatu ni wale ambao wamejipambanua katika huduma kwa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao. Makardinali wapya watasimikwa rasmi katika mkutano wa kawaida wa Makardinali utakaoadhimishwa tarehe 30 Septemba 2023 mjini Vatican. Idadi yao inapaswa kuwa ni Makardinali 137, Idadi ya Makardinali wenye sifa za kuchagua au kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ikiwa kama kutafanyika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.Takwimu zinaonesha kwamba hadi mwezi Septemba 2023 Bara la Ulaya litakuwa na Makardinali 53 kati yao Makardinali kutoka Italia 15; Amerika ya Kaskazini wapiga kura ni 15, Marekani ikiwa na wapiga 11 na 4 ni kutoka Canada. Makardinali kutoka Amerika ya Kusini wapiga kura ni 19 na Bara la Afrika wapiga kura ni 23, Barani Asia, Makardinali wapiga kura ni 23 wakati ambapo Oceania wapiga kura ni 3.   Hawa ni Makardinali wanaoonesha ukatoliki wa Kanisa, wanaotumwa kutangaza na kushuhudia upendo wa huruma ya Mungu kwa watu wote wa Mataifa. Makardinali hawa wataingizwa kwenye Jimbo kuu la Roma ili kuonesha mahusiano na mafungamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia yaliyoenea sehemu mbalimbali za dunia. Makardinali kimsingi ndio washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kukoleza juhudi za toba, haki, amani na maridhiano; kwa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, ili watu waweze kuishi katika mazingira bora zaidi.

Kardinali Protase Rugambwa, akiagwa Jimboni Kigoma, tayari kwenda Tabora
Kardinali Protase Rugambwa, akiagwa Jimboni Kigoma, tayari kwenda Tabora

Makardinali wateule kutoka Afrika ni: Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania anasema: “Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya imani na baadae kwa kunizawadia neema ya kumtumikia na kuwatumikia watu kama mchungaji na ninaomba sasa hilo aliloliweka ndani mwangu liendelee kukua na daima kwa ajili ya kuujenga ufalme wake. Pamoja na wote waaminio na wenye mapenzi mema naamini kabisa kuwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu tutaweza kuyafanya mapenzi yake Mungu, ahimidiwe, tumtukuze na tumsifu milele." Wakati huo huo, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amemwandikia Kardinali mteule Protase Rugambwa, ujumbe wa matashi mema, huku akiungana na watanzania wote kumtakia heri na kumsindikiza katika sala anapoendelea na utume wake katika hatua hii mpya kama Kardinali. Mwenyezi Mungu ambaye amemwinua kwa baraka na jukumu hili kwenye wito wake mtakatifu, aendelee kumwongoza kulitumikia Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Kardinali Stephen Ameyu Martin Mulla, Jimbo kuu la Juba
Kardinali Stephen Ameyu Martin Mulla, Jimbo kuu la Juba

Kardinali Stephen Ameyu Martin Mulla wa Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini alizaliwa huko Alodu Jimbo Katoliki la Torit, Sudan Kusini kunako tarehe 10 Januari 1964. Alijiunga na Seminari ndogo ya Torit, kati ya mwaka 1978 - 1981 na baadaye akaendelea na seminari ya Wau, tangu 1981- 1983. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 21 Aprili 1991, akapewa daraja takatifu ya Upadre katika Jimbo Katoliki la Torit Sudan ya Kusini. Tarehe 3 Januari 2019 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa jimbo Katoliki la Torit, Sudan Kusini. Katika maisha na utume wake amewahi kuwa: Jaalim na Profesa na Dekano wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Paulo, Jimbo kuu la Juba, Sudan ya Kusini.

Kardinali Stephen Brislin, Askofu mkuu Jimbo kuu la Cape Town
Kardinali Stephen Brislin, Askofu mkuu Jimbo kuu la Cape Town

Kardinali Stephen Brislin Askofu mkuu wa Jimbo kuu la “Cape Town”, Afrika ya Kusini alizaliwa tarehe 24 Septemba 1956 huko Welcome. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre tarehe 19 Novemba 1983 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Kroonstad, Afrika ya Kusini. Baba Mtakatifu Benedikto XVI, tarehe 17 Oktoba 2006 akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Kroonstad na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 28 Januari 2007. Na ilipogota tarehe 18 Desemba 2009 Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Cape Town, Kaapstad, Afrika ya Kusini na tarehe 30 Septemba 2023 anasimikwa kuwa Kardinali. Jimbo kuu la Tabora, Jimbo kuu la Juba pamoja na Jimbo kuu la Cape Town, Kaapstad, Afrika ya Kusini, kwa mara ya kwanza katika historia majimbo haya makuu yamepata Kardinali tayari kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza wa Mungu.

Kardinali Luis Pascual Dri, Umri miaka 96 huma ya Upatanisho
Kardinali Luis Pascual Dri, Umri miaka 96 huma ya Upatanisho

Padre Luis Pascual Dri, Mtawa Mfranciskani Mkapuchini alizaliwa tarehe 17 Aprili 1927, Entre Rios, Argentina. Baada ya malezi na majiundo yake ya kitawa tarehe 21 Februari 1945 akaweka nadhiri za kwanza na mwaka 1949 akaweka nadhiri za daima. Tarehe 29 Machi 1952 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Alibahatika katika maisha na utume wake kuwa Gambera wa Seminari ya Serafico di Villa Gdor; Mlezi wa Wanovisi, Paroko na kuanzia mwaka 2007 akajichimbia kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei “Santuario di Nuestra Señora de Pompeya.” Nchini Argentina. Leo hii ana umri wa miaka 96 na anaendelea kuwahudumia watu wa Mungu kwa kutoa Sakramenti ya Upatanisho! Chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, wanaokimbilia kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, tayari kuomba huruma, msamaha na upendo wa Mungu.

Makardinali Afrika
10 July 2023, 17:16