Tafuta

Maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 10 tangu Papa Francisko alipotembelea Kisiwa cha Lampedusa, tarehe 8 Julai 2013 Maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 10 tangu Papa Francisko alipotembelea Kisiwa cha Lampedusa, tarehe 8 Julai 2013  

Kumbukizi ya Miaka 10 Tangu Papa Atembelee Kisiwa cha Lampedusa

Papa Francisko katika kumbukizi ya miaka 10 tangu alipotembelea Kisiwa cha Lampedusa, tarehe 8 Julai 2013 katika ujumbe aliomwandikia Askofu mkuu Alessandro Damiano anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa sala pamoja na kuendelea kuwatia shime, hasa wakati huu, ambapo bado Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kushuhudia watu wakifa maji kwenye Bahari ya Mediterrania, hasa watoto wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kutoka kwenye vita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 8 Julai 2013 kwa mara ya kwanza kabisa, Baba Mtakatifu Francisko, baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, alipofanya ziara yake ya kwanza kutoka mjini Vatican ili kwenda kwenye Kisiwa cha Lampedusa, kilichoko Kusini mwa Italia, kuonesha mshikamano wake wa dhati kwa wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanahifadhiwa Kisiwani hapo. Lakini pia, Baba Mtakatifu alipenda kusali na kuwaombea wale wote waliofariki dunia na kumezwa kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania na makaburi yao hayana alama wala kumbukumbu tena! Hili ni tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kiasi hata cha kuanzisha Idara ya Wakimbizi na Wahamiaji kwenye Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, inayowajibika moja kwa moja kwake binafsi! Mama Kanisa anapenda kuwa ni sauti ya wanyonge na maskini; wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Maskini kama ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo, wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwani hawa ni walengwa wa Habari Njema ya Wokovu. Juhudi hizi hazina budi kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Mchakato wa ujenzi wa mshikamano wa udugu wa binadamu ni msingi wa huduma makini kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Udugu wa kibinadamu uwe ni kikolezo kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete, kushirikiana na kushikamana katika mapambano dhidi ya baa la njaa, umaskini na magonjwa yanayoendelea kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Makaburi ya wakimbizi na wahamiaji yasiyo na alama baharini
Makaburi ya wakimbizi na wahamiaji yasiyo na alama baharini

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, leo hii kuna aina mbalimbali za umaskini zinazomwandama mwanadamu. Hawa ni wale wanaonyanyaswa na kupuuzwa; watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; watoto wadogo, wazee na wagonjwa bila kuwasahau wale ambao jamii haiwathamini tena kutokana na hali yao ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 10 tangu alipotembelea Kisiwa cha Lampedusa, tarehe 8 Julai 2013 katika ujumbe aliomwandikia Askofu mkuu Alessandro Damiano wa Jimbo kuu la Agrigento, Italia, anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa sala pamoja na kuendelea kuwatia shime, hasa wakati huu, ambapo bado Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kushuhudia watu wakifa maji kwenye Bahari ya Mediterrania, hasa watoto wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kutoka kwenye maeneo ya vita! Hiki ni kilio ambacho hakisikilizwi, aibu kwa jamii ambayo haiwezi tena kuwalilia watoto wake. Vifo vya wakimbizi na wahamiaji lazima visute dhamiri za Jumuiya ya Kimataifa na Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuwauliza watu wa Mataifa, “Je, mko wapi, Ndugu yako yuko wapi?” Umefika wakati wa kubadili tabia na mwenendo wa maisha, tayari kuwafungulia malango ya huruma na mapendo wakimbizi na wahamiaji, ili kuwapokea na kuwapatia hifadhi pamoja na kugawana mazao ya nchi.

Kuna watoto wengi wanaofariki dunia wakiwa njiani kuitafuta Ulaya
Kuna watoto wengi wanaofariki dunia wakiwa njiani kuitafuta Ulaya

Huu ni mwaliko wa kupyaisha kutoka katika undani wa maisha ya watu dhamana na wajibu na hivyo kuanza kujikita katika ujenzi wa mshikamano wa udugu na ushirikiano. Ili Kanisa liweze kuwa ni la kinabii, halina budi kujitosa kikamilifu katika kuwahudumia na kuwasaidia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa mafuta ya udugu wa kibinadamu, mshikamano na upendo wa dhati, kwani kufanya hivi wanayahudumia Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu Jimbo kuu la Agrigento, lililoko Kusini mwa Italia kuondokana na woga usiokuwa na mvuto wala mashiko, bali wajikite katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na ya Kiinjili, ili utukufu wa Mungu uweze kung’aa tena Kisiwani hapo. Kwa upande wake, Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii anasema, wakimbizi na wahamiaji ni kati ya vipaumbele vya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kujenga ndani mwao ile hali na tabia ya Msamaria mwema. Ni mwaliko kwa kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji. Mtakatifu Paulo VI kunako mwaka 1966 alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari kuhusu vita alisema, amani inawezekana kutawala katika akili na nyoyo za watu, lakini uvumilivu na subira ni mambo yanayohitajika. Baba Mtakatifu Francisko anasema, amani ni kikolezo cha maendeleo endelevu ya binadamu, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Lampedusa 2023
08 July 2023, 15:28