Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 23 Julai 2023 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee kwa mwaka 2023. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 23 Julai 2023 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee kwa mwaka 2023.   (Vatican Media)

Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani: Mahubiri: Ngano na Magugu Vikue Pamoja

Papa Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee kwa mwaka 2023. Katika mahubiri yake amekazia kuhusu magugu “Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; wito wa kupokea fumbo la maisha kwa amani na uvumilivu bila kujutia yale yaliyopita katika maisha; Ufalme wa Mungu umefanana na chachu, kazi ya Mwenyezi Mungu katika hali ya ukimya kwa kujikita katika historia kama mbegu ya haradali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani, Dominika tarehe 23 Julai 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi” Lk. 1:50. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa mwaka 2023 anagusia kuhusu: Bikira Maria akiwa amejazwa na nguvu ya Roho Mtakatifu akaondoka kwa haraka, Mkutano kati ya Bikira Maria na Elizabeti, Kati ya vijana na wazee; Iwe ni siku ya kukutana kwa furaha na kwa upya kati ya vijana wa kizazi kipya na vijana wa zamani, yaani wazee. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee kwa mwaka 2023 inaonesha ile furaha aliyokuwa nayo Bikira Maria aliyekuwa amejazwa nguvu ya Roho Mtakatifu alipokutana na binadamu yake Elizabeti na kumwakia akisema, “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Lk 1:42. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 23 Julai 2023 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee kwa mwaka 2023. Katika mahubiri yake amekazia kuhusu magugu “Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; wito wa kupokea fumbo la maisha kwa amani na uvumilivu bila kujutia yale yaliyopita katika maisha; Ufalme wa Mungu umefanana na chachu, kazi ya Mwenyezi Mungu katika hali ya ukimya kwa kujikita katika historia kama mbegu ya haradali. Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu iliyotiwa katika unga ukachachwa wote. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu alitumia mifano mbalimbali iliyokuwa inawafikia na kugusa undani wa maisha ya wasikilizaji wake, ni mifano kama hii, mababu, mabibi na wazee sehemu mbalimbali za dunia wametumia kuwasimulia wajukuu wao.

Ibada ya Misa Takatifu kwa Babu, Bibi na Wazee Duniani 2023
Ibada ya Misa Takatifu kwa Babu, Bibi na Wazee Duniani 2023

Kristo Yesu katika Injili anakaza kusema, “Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno.” Hii ni picha inayoonesha hali halisi ya maisha ya mwanadamu; mwanga na vivuli vya giza; upendo na ubinafsi pamoja na uwepo wa dhambi na ubaya wa moyo. Mwamini Mkristo akiwa anahamasishwa na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayeweza kuyatazama kutoka moyo mwake: mabaya kwa mazuri kwani ulimwenguni kumesheheni “magugu na ngano”; na kwamba, mwanadamu anao ubaya unaokita mizizi yake katika undani wa maisha, changamoto na mwaliko kwa waamini kupambana ili hatimaye, kuboresha undani wa maisha yao. Pale magugu na ngano vinapoishi kwa pamoja, kwani si rahisi sana kuweza kupata jamii au Kanisa lililosafi kabisa, kwani ili kuweza kufikia usafi na ubora huu, kuna hatari ya kukosa uvumilivu kwa wale walioteleza na kuanguka katika ubaya wa moyo, kiasi hata cha kukwamisha juhudi za kutembea, kukua na kukomaa. Ndiyo maana Kristo Yesu anasema kwa msisitizo: “Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno.” Rej. Mt 13:30. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa wavumilivu kwa waamini wenzao, tayari kuwakaribisha na kuwapokea kwenye familia, katika Kanisa na jamii katika ujumla wake, walio wanyonge na wadhaifu na kamwe wasiridhike na kujihesabia haki, bali wawe tayari kujifunza kwa uvumilivu utunzaji wa ngano bora. Toba, wongofu wa ndani na utakaso wa roho ni ushindi dhidi ya dhambi na ubaya wa moyo ni kazi ya Mwenyezi Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kushinda kile kishawishi cha kutenganisha magugu na ngano, daima wawe macho kusoma alama za nyakati, ili hatimaye, kufiri na kutenda kwa wakati.

Wazee wana dhamana ya kurithisha imani kwa vijana na watoto wao
Wazee wana dhamana ya kurithisha imani kwa vijana na watoto wao

Huu ni mwaliko kwa babu, bibi na wazee ambao wamekwisha kufanya safari ndefu na kupata mang’amuzi mbalimbali ya maisha. Wakiangalia nyuma, wataona mambo mazuri waliyotenda pamoja na yale ambayo pengine kutokana na sababu mbalimbali katika maisha hawakuweza kufaulu kutekeleza, leo hii, Kristo Yesu anatoa wito wa kupokea fumbo la maisha kwa amani na uvumilivu bila kujutia yale yaliyopita katika maisha, mfano wa ngano na magugu na kwamba, wema utashinda dhidi ya ubaya. Baba Mtakatifu anasema, uzee ni muda uliobarikiwa, ni muda wa kujipatanisha, kuyaangalia mambo kwa wema mintarafu umri wao, licha ya changamoto wanazokumbana nazo, wawe na imani na matumaini kwamba, ile mbegu bora ya ngano iliyopandwa na Mungu iko siku itashinda hata kama Shetani, Ibilisi amepandikiza magugu katika nyoyo za waamini. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ufalme wa Mungu ni kazi ya Mungu mwenyewe anayetenda katika hali ya ukimya mintarafu historia, kama vile punje ya haradali, nayo ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake. Rej. Mt 13:32. Hivi ndivyo yalivyo hata maisha ya binadamu, anazaliwa akiwa mdogo, analishwa kwa matumaini na kuanza kutekeleza miradi na ndoto na hatimaye kuwa mti mkubwa unatoa kivuli kwa wale wanaohitaji, na nafasi kwa wale wanaotaka kutengeneza kiota. Na hivi ndivyo kukua kwa pamoja na hatimaye, kuzeeka kama mtu na ndege waangani wanafanya makao yao! Hivi ndivyo mababu, mabibi na wazee wanavyobadilika na kuwa ni viota vya wajukuuu wao, wito wa kujenga mahusiano na mafungamano kati ya wazee, vijana na watoto, ili kuchanua matumaini, na hivyo kuendelea kujifunza uzuri wa maisha ili kujenga jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu na Kanisa linageuka na kuwa ni mahali pa kukutanikia watu katika majadiliano kati ya mapokeo na upya katika Roho Mtakatifu.

Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa Mwaka 2023
Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa Mwaka 2023

Kristo Yesu akawaambia akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia. Rej. Mt 13:32. Huu ni mwaliko kwa waamini kutoka nje ya nafsi zao wenyewe na kujiunga na wengine, ni tendo ambalo linaleta afya tele katika mahusiano na mafungamano ya kijamii, kiasi cha kushinda ubinafsi na uchoyo tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika utu na udugu wa kibinadamu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa macho ili ndani ya familia na jamii katika ujumla wake, yasijitokeze magugu, yanayowatenga wazee; badala yake, siasa na sera zisaidie kushughulikia mahitaji ya watu wanyonge ndani ya jamii, ili hatimaye, kuondokana na utandawazi usioguswa wala kujali mahangaiko ya wengine, bali kwa kusaidiana na kutangulizana. Huu ni mwaliko wa kujichanganya, ili hatimaye, kukua pamoja. Neno la Mungu linatoa mwaliko kwa waamini kushikamana ili kukua kwa pamoja, kwa kusikilizana, kujadiliana na kusaidiana. Baba Mtakatifu anasema, kamwe wazee wasisahaulike, bali waonjeshwe wema na ukarimu; ili wajisikie kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na hivyo kutakaswa kutoka katika undani wa utu wao. Kuna watu ambao wamejisadaka kwa ajili ya wazee, bibi na babu na kwamba, si haki kuwaibia vipaumbele vya maisha. Hiki ni kipindi cha kukua pamoja, kwa kusonga mbele kwa pamoja na kwamba, Mwenyezi Mungu atabariki safari hii njema.

Wazee wamewakabidhi vijana Msalaba wa Vijana kielelezo cha urithi wa imani
Wazee wamewakabidhi vijana Msalaba wa Vijana kielelezo cha urithi wa imani

Mara baada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wazee watano waliowawakilisha wazee wenzao kutoka katika mabara matano, wamewakabidhi vijana wa kizazi kipya Msalaba wa Siku ya Vijana Ulimwenguni, kama kielelezo cha kurithisha imani kutoka kizazi hata kizazi. Mwaka huu maadhimisho ya Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani yameadhimishwa karibu sana na Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yanayoanza kutimua vumbi huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Sherehe zote mbili zinagusia “haraka” ambayo Bikira Maria alipanga kumtembelea binamu yake Elizabeti, mwaliko kwa watu wa Mungu kutafakari dhamana na wajibu unaowaunganisha vijana na wazee. Mwenyezi Mungu kwa njia ya mahusiano na mafungamano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, wanatambua kwamba, wameitwa kukuza na kudumisha kumbukumbu na kutambua uzuri wa kuwa ni sehemu ya historia kubwa zaidi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, urafiki na wazee unaweza kuwasaidia vijana kuona maisha yao si tu kwamba, ni jambo la mpito na kwamba, si kila kitu kinawategemea wao na uwezo wao. Kwa wazee, uwepo wa kijana katika maisha yao unaweza kuwapa matumaini kwamba, uzoefu wao hautapotea na kwamba, ndoto zao zinaweza kupata utimilifu. Ibada hii ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican imehudhuriwa pia na Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson (Mb) Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyeongozana na ujumbe wa watu kumi na wawili!

Papa Wazee 2023

 

 

 

 

23 July 2023, 15:03