Papa Francisko Ni Shuhuda wa Unabii wa Nguvu na Jasiri Kuhusu Amani Duniani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa hivi karibuni amezindua kitabu cha “Limes” kinachomzungumzia Baba Mtakatifu Francisko: Unabii wa nguvu na wenye ujasiri kuhusu amani duniani. Mwitikio wa watu wa Mungu kutoka Ukraine kwa matamko mbalimbali ya Baba Mtakatifu unaonesha tamaa kubwa ya kutaka kupata amani ya kudumu. Tamaa hii imeoneshwa na viongozi wa Serikali, dini na watu wa Mungu katika ujumla wao. Maneno na ishara za hadhara zinazofanywa na Baba Mtakatifu ni kweli na tafsiri yake inaweza kutolewa kwa uhuru kamili na busara na wala si matamanio ya kufikirika tu juu ya amani nchini Ukraine. Baba Mtakatifu anawaalika wapenda haki, amani na maridhiano kukusanya nguvu zao za pamoja, ili kukoleza majadiliano katika ukweli na uwazo, ili hatimaye, amani ya kudumu iweze kupatikana nchini Ukraine. Baba Mtakatifu Francisko “anakumwa” kutafuta amani ya kudumu nchini Ukraine kwa kutumia mbinu mbalimbali ili kuwezesha majadiliano ya amani yawezekane kwa kuhamasishwa na kanuni kwamba, “Kanisa halipaswi kutumia lugha ya siasa, bali lugha ya Kristo Yesu inayosimikwa katika upendo, haki na maridhiano.
Kumbe, jitihada za Baba Mtakatifu za kutafuta haki, amani na maridhiano “si kutwanga maji kwenye kinu”, bali ni kutaka kuifumbua macho Jumuiya ya Kimataifa ili iweze kufahamu yale yanayoendelea kujiri kwenye vita kati ya Urusi na Ukraine. Ifahamike kuwa Urusi ni nchi mchokozi, iliyochokoza na hatimaye, kuivamia Ukraine na ukweli huu unafamika kwa wengi kwenye Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu ameendelea kumwonesha mchokozi na Ukraine kuwa ni mwathirika wa “vita hii isiyokuwa na kichwa wala miguu.” Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, anakaza kusema ishara na maneno ya Baba Mtakatifu Francisko si usemi wa maneno ya amani tu bali ni unabii wa amani, wenye nguvu na shupavu unaopinga uwepo wa vita. Unabii hata hivyo, badala ya kukubaliwa na kuungwa mkono ili uweze kutekelezwa kwa urahisi, unakataliwa na kulaaniwa. Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Ukraine ameendelea kuwemo nchini humo kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Baba Mtakatifu Francisko miongoni mwa watu wa Mungu nchini Ukraine. Huu ni ushuhuda kwamba, Kanisa linataka kusimama kidete kupinga mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Ukraine na hivyo kuonesha ukaribu wa Kikristo kwa mashuhuda wa imani, ili amani iweze kupatikana. Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele kushughulia waathirika wa vita kati ya Urusi na Ukraine. Hii ni huduma ya kibinadamu inayoonesha mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu. Majadiliano ya kiekumene pamoja na liturujia takatifu imeendelea kudumishwa nchini Ukraine.
Mashirika mbalimbali ya misaada ya Kanisa Katoliki, Caritas yamekuwa yakipeleka misaada ya hali na mali nchini Ukraine, bila kusahau safari za kikazi zilizotekelezwa na Kardinali Konrad Krajewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo, ambaye pia ni Msimamizi mkuu wa Sadaka ya Kitume. Matukio yote haya ni kielelezo cha mshikamano wa upendo wa udugu wa kibinadamu, Baba Mtakatifu anapenda kuwakumbatia watu wa Mungu nchini Ukraine katika kipindi hiki kigumu cha historia na maisha ya nchi yao. Kumbe ni jukumu la Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inatoa huduma na msaada kwa wananchi wa Ukraine pamoja na kujielekeza zaidi katika kutafuta suluhu ya kudumu ya Vita Kuu ya Tatu ya Dunia inayopiganwa vipande vipande, kumbe utafutaji wa muafaka kwa vita hii ni mchango mkubwa. Askofu mkuu Paul Richard Gallagher anakaza kusema kuna haja kwa baadhi ya watu kubadili misimamo na mitazamo yao ili kujizatiti zaidi katika kutafuta, kuambata na kudumisha amani duniani, ili hatimaye, kuondokana na mantiki ya vita ambayo kwa bahati mbaya sana inaendelea kutawala ili kunogesha biashara ya silaha duniani. Jambo la msingi kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kutafuta suluhu ya migogoro na changamoto mbalimbali za maisha kwa njia ya majadiliano na diplomasia ya Kimataifa ili kuepuka majanga yanayotokana na vita duniani. Dhana ya watu kuheshimiana na kuaminiana ni hatua kubwa katika mchakato wa kutatua changamoto na migogoro ya kivita sehemu mbalimbali za dunia. Na kwa njia, kuna uwezekano mkubwa wa kutekeleza mipango ya kiutu na kibinadamu, kwa kubadilishana wafungwa na mateka wa vita; usafirishaji wa ngano nje ya nchi pamoja na harakati za kuwarejesha watoto waliopotea katika mazingira ya vita majumbani mwao. Kimsingi haya ndiyo anayojaribu kufanya Kardinali Matteo Maria Zuppi, Mwakilishi wa Baba Mtakatifu Francisko huko Ukraine na Urusi. Lakini vita kati ya Urusi na Ukraine lazima ikomeshwe haraka iwezekanavyo kabla mambo hayajaaribisha vibaya.