2023.07.16 Papa Francisko wakati wa sala ya Malaika wa Bwana. 2023.07.16 Papa Francisko wakati wa sala ya Malaika wa Bwana.  (Vatican Media)

Papa:Wazazi,msichoke kupanda mbegu ndani ya watoto wenu!

Katika tafakari yake kuhusu mpanzi katika Injili ya siku Papa ametoa mwaliko kwa wazazi,mapadre,watawa na walei kudumu katika kuitangaza Injili kwa furaha na ukarimu,bila kufuata mitindo,bila kukatishwa tamaa kwa kuzingatia mafanikio ya haraka.Hasa amewataka vijana kutumia muda vizuri bila kuupoteza katika simu.

Na Angella Rwezaula,- Vatican.

Katika Domini ya 15 ya Mwaka A wa Kanisa, tarehe 16 Julai 2023, Baba Mtakatifu Francisko ametoa tafakari yake kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwa waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican,licha ya Joto kali. Akianza tafakari hiyo kwa kuongozwa na Injili ya siku amesema: “Leo Injili inatuonesha mfano wa mpanzi (Mt 13:1-23). Jambo la kupanda ni mfano mzuri sana na Yesu anautumia kufafanua zawadi ya Neno lake. Hebu tufikirie mbegu.  Ni ndogo, ambayo huwezi kuiona, lakini inafanya mimea kukua na ambayo huzaa matunda. Neno la Mungu liko hivyo na kwa hiyo tufikirie Injili, ambacho ni kitabu kidogo, rahisi na kinachoweza kufikiwa na kila mtu, na ambacho huzalisha maisha mapya kwa wale wanaokikaribisha”, amesisitiza. Akiendelea na tafakari hiyo Baba Mtakatifu ameeleza kwamba ikiwa Neno ni mbegu, sisi ni udongo: tunaweza kupokea au la. Hata hivyo, Yesu, ambaye ni “mpanzi mwema” hachoki kuipanda kwa ukarimu. Anaijua ardhi yetu, anajua kwamba mawe ya kutotulia kwetu na miiba ya maovu yetu (Mt 13, 21-22) yanaweza kulisonga Neno, lakini daima anatumaini, daima anatumaini kwamba tunaweza kuzaa matunda mengi (taz. Mt 13, 8).

Waamini na mahujaji wakisikiliza tafakari kabla ya sala ya Malaika wa Bwana
Waamini na mahujaji wakisikiliza tafakari kabla ya sala ya Malaika wa Bwana

“Kwa hiyo, hivyo ndivyo Bwana anafanya na hili ndilo tunaloitwa pia kufanya, la kupanda bila kuchoka", Papa amekazia. Lakini tunawezaje kufanya hivyo, kupanda kwa kuendelea bila kuchoka?  “Hebu tuchukue mifano fulani. Kwanza kabisa wazazi, wao hupanda wema na imani kwa watoto wao na wameitwa kufanya hivyo bila kukata tamaa ikiwa nyakati fulani wanaonekana hawaelewi na hawathamini mafundisho yao, au ikiwa mawazo ya watu ulimwengu yanafanya kazi dhidi ya”.  Mbegu nzuri inabaki na ndiyo jambo la maana, nayo itakuwa na mizizi kwa wakati ufaao”. Lakini ikiwa, wakitoa nafasi ya kutoaminiana, wanaacha kupanda na kuwaacha watoto wao kwa huruma ya mitindo na simu za mkononi, bila kujitolea muda kwao, bila kuwaelimisha, basi ardhi yenye rutuba itajaza magugu”.  Kutokana na hilo Papa ametoa angalisho: “Wazazi, msichoke kupanda mbegu ndani ya watoto wenu!”

Mahujaji na waamini katika uwanja wa Mtakatifu Petro
Mahujaji na waamini katika uwanja wa Mtakatifu Petro

Kwa kuwageukia vijana Baba Mtakatifu amesema, wao pia wanaweza kupanda Injili katika mifereji ya maisha ya kila siku. Kwa mfano wa sala, maana  ni mbegu ndogo ambayo haiwezi kuonekana, lakini ambayo mtu hukabidhi kila kitu ambacho mtu huishi kwa Yesu na hivyo wanaweza kuifanya kukomaa. Lakini pia Papa amefikiria fursa ya wakati wa kujitolea kwa wengine, kwa wale wanaohitaji sana. Hii inaweza kuonekana kupoteza, lakini badala yake ni wakati mtakatifu, badala ya wakati wa kuridhika kwa matumizi ya hovyo na ambayo yanaacha watu mikono mitupu. Papa amefikiria masomo kwamba ni kweli yanachosha,na si mara moja yanafurahisha, kama vile wanapopanda, lakini ni muhimu kwa kujenga maisha bora ya baadaye kwa wote”.

Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana Dominika tarehe 16 Julai 2023

Baada ya kuwaona wazazi na vijana,  Papa Francisko amewageukia wapanzi wa Injili, kama vile mapadre wema wengi, watawa na walei wanaojishughulisha na kutangaza, wanaoishi na kuhubiri Neno la Mungu mara kwa mara bila kusifia mafanikio ya haraka. “Tusisahau kamwe, tunapotangaza Neno, kwamba hata pale panapoonekana kana kwamba hakuna kinachotokea, kiukweli Roho Mtakatifu anafanya kazi na ufalme wa Mungu tayari unakua, kupitia na zaidi ya juhudi zao. Kwa hivyo, Papa amewahimiza na kuwatia moyo wa kwenda  mbele kwa furaha, kaka na dada wapendwa! Kwa kuongezea amesema:“Tuwakumbuke watu waliopanda mbegu ya Neno la Mungu katika maisha yetu: kila mmoja wetu afikirie “jinsi imani yake ilianza”. Labda ilichipuka miaka mingi baada ya kukutana na mifano yao, lakini shukrani ilifanyika kutoka kwao!

Sala ya Malaika wa Bwana 16 Julai 2023
Sala ya Malaika wa Bwana 16 Julai 2023

Kwa kuzingatia haya yote, Papa amesema "tunaweza kujiuliza: je, ninapanda mema? Je, ninajishughulisha tu na kuvuna kwa ajili yangu mwenyewe au pia kupanda kwa ajili ya wengine? Je, ninapanda mbegu fulani za Injili katika maisha ya kila siku: kusoma, kufanya kazi, wakati wa kupumzika? Je, ninavunjika moyo au, kama Yesu, ninaendelea kupanda, hata kama sioni matokeo ya haraka? Bikira Maria tunayemuheshimu leo ​​hii kama Bikira Mbarikiwa wa Mlima Karmeli, atusaidie kuwa wapandaji wa Habari Njema,  wakarimu na wenye furaha”, amehitimisha.

ANGELUS PAPA 16 JULAI 2023
16 July 2023, 13:10