Papa: Siku ya urafiki duniani &Siku dhidi ya biashara haramu ya binadamu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya sala ya Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana na Baraka, kwa waamini na mahujaji wengi waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro, Vatican, Dominika tarehe 30 Julai 2023, Baba Mtakatifu amesema kuwa: “Leo tunaadhimisha siku mbili za dunia zilizoandaliwa na Umoja wa Mataifa: Siku ya Urafiki na Siku dhidi ya biashara haramu ya binadamu. Ya kwanza inahamasisha urafiki kati ya watu na tamaduni; Ya pili Siku hiyo inapambana na uhalifu unaowafanya watu kuwa bidhaa.”
Siku dhidi ya biashara haramu ya binadamu 2023
Katika muktadha huo Papa Franciskp amekazia kusema kuwa: “Usafirishaji haramu wa binadamu ni ukweli wa kutisha, unaoathiri watu wengi sana: watoto, wanawake, wafanyakazi…, watu wengi walionyonywa; wote wanaishia katika hali zisizo za kibinadamu na kuteseka kutojali na kukataliwa na jamii. Kuna biashara nyingi sana duniani leo hii. Mungu awabariki wale waliojitolea kupambana na biashara haramu.”
Wito Papa kwa Mamlaka ya Urussi
Baba Mtakatifu bado ametazama nchi ya Vita kwamba: “Tusiache kuiombea Ukraine iliyopigwa, ambapo vita huharibu kila kitu, hata nafaka. Hili ni kosa kubwa kwa Mungu, kwa sababu ngano ni zawadi yake ya kuwalisha wanadamu; na kilio cha mamilioni ya kaka na dada wanaoteseka na njaa kinapanda hadi Mbinguni. Ninatoa wito kwa ndugu zangu, mamlaka ya Shirikisho la Urussi ili mpango wa Bahari Nyeusi urejeshwe na nafaka iweze kusafirishwa kwa usalama.”
Kumbukumbu ya Mlipuko wa bandari Lebanon
Baba Mtakatifu amesema kwamba: “Tarehe 4 ijayo Agosti itaadhimishwa miaka mitatu tangu kutokea kwa mlipuko mkubwa katika bandari ya Beirut. Ninasasisha maombi yangu kwa waathiriwa na familia zao, ambao wanatafuta ukweli na haki, na ninatumaini kuwa shida ngumu ya Lebanon itapata suluhisho linalostahili historia na maadili ya watu hao. Tusisahau kwamba Lebanon pia ni ujumbe”.
Siku ya vijana WYD Lisbon 2023 na kuwakabidhi kwa Maria
Baba Mtakatifu akifikiria siku ya vijana inayokuja amesema “Ninawaomba mnisindikize kwa maombi yenu katika safari yangu ya kuelekea Ureno, ambayo nitaifanya kuanzia siku ya Jumatano ijayo, katika kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani. Vijana wengi, kutoka mabara yote, watapata furaha ya kukutana na Mungu na kaka na dada zao, wakiongozwa na Bikira Maria, ambaye baada ya Tangazo la Malaika “alisimama na kwenda kwa haraka” (Lk 1:39). Kwake yeye, nyota angavu ya safari ya Kikristo, anayeheshimiwa sana nchini Ureno, ninawakabidhi mahujaji wa WYD na vijana wote wa ulimwengu.
Papa awasalimia mahujaji
Na sasa ninawasalimu ninyi, Warumi na wasafiri kutoka Italia na kutoka nchi nyingi. Hasa, ninawasalimia kwaya ya watoto ya Veliko Tarnovo, huko Bulgaria, na kikundi cha vijana wa Mexico; pamoja na vijana wa Biadene na Caonada. Na ninawasalimu Vijana wa Bikira Maria Msafi wa Moyo. Kwa kuhimitimisha amewatakia Dominika Njema, lakini wasisahau kusali kwa ajili yake.